UNAJUA KWAMBA UNAWEZA KUJENGA NYUMBA BINAFSI BILA MKOPO?Leo nimeendelea na harakati za kutembelea na kuombea wapendwa waweze kujenga na kukamilisha ujenzi wa nyumba zao binafsi. Kabla ya kuweka mikakati tunatakiwa kuanza na Mungu anayetoa UPENYO (BREAKTHROUGH). Tambua kwamba MAOMBI HAYAFANYI KILA KITU, LAKINI MAOMBI NDIYO MWANZO WA KILA KITU.
Ushuhuda wangu nilivyoweza kujenga bila mkopo:
Nilimuomba Mungu halafu siku moja nikasikia sauti ikisema, START SMALL! Maana yake ni ANZA NA VITU VIDOGO UNAVYOWEZA, USISUBIRI UPATE PESA NYINGI. Nikatafakari na kuifanyia kazi sauti hii.
(i). Nikagundua kwamba kwa kipindi hicho sina milioni za pesa kwa ajili ya kiwanja. Hivyo nikasema moyoni mwangu, Kwani nikipata kiwanja si itabidi nitafute vifaa ndipo nijenge? Kwani siwezi kuanza na vifaa kabla ya kiwanja kwa hii pesa ndogo ninayopata? Nikaanza kununua mabati kidogokidogo. Nikajikuta nina mabati 80 ya geji 28 ndipo nikapata kiwanja. Wakati huo bei ya bati imeshapanda sana. Hata wewe kama unayo nia ya kujenga unaweza kuanza kununua hata misumari kwa vile haiozi!
(ii). Nikaamua kuwa na ramani ambayo naweza kukamilisha vyumba vichache kwa wepesi ili akae mtu ndipo nijipange kwa ajili ya nyumba kubwa. Uamuzi huu ulinisaidia kwa ajili ya usalama wa vifaa na kupima nguvu yangu. Daudi alijiridhisha kwamba atampiga Goliathi kwa vile aliwahi kumuua simba na dubu. Usilazimishe imani ambayo haijawahi kutenda kazi. Imani inakua kama mtu anavyokua. 1 Samweli 17:36 “Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.”
(iii). Nilitafuta mtaalamu anipigie gharama za jengo zima ili nisinunue vifaa vingi vikabaki wakati nina upungufu katika upande mwingine. Mara nyingi tunakwepa wataalamu hawa na kujikuta tukiingia gharama kubwa au kushindwa njiani. Unakuwa umeshamlipa fundi pesa nyingi na vifaa vimekuishia ghafla. Au vifaa vya aina moja vimebaki vingi sana wakati upande mwingine hujamaliza. Hujawahi kuona mtu amenunua zikabaki trip 10 za mawe lakini hana tofali za kumalizia nyumba yake?
Bwana Yesu aliwahi kutoa maelekezo ya kuhakikisha unahesabu gharama na kulinganisha na nguvu yako kabla ya kujiingiza kwenye mradi au utekelezaji. Alisema unaweza kuchekwa kama huna mpango unaotekelezeka. Luka 14:28-30 “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.”
Tatizo tulilo nalo leo hatuhamasishwi tena kuweka akiba. Tunataka tuonekane tumefanya mambo makubwa kwa haraka. Matokeo yake tunaishi kwa hofu siku zote. Tungeweza kila mwezi kutenge kiasi kidogo na kununua vifaa kadhaa.
Maandiko yametuagiza kwamba kama hatuelewi watu wakitushauri na kutufundisha, tuwatembelee sisimizi ili tujifunze jinsi wanavyoweka akiba. Mithali 6:6-8 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.”
Mungu akufungue fahamu zako ili ufanye maamuzi makini yasiyo na majuto huku ukijifunza kuanza na Mungu, kuishi kwa imani, kutoiga maisha ya wengine, kuwa na mikakati inayotekelezeka na kuanza na hichohicho kidogo ulicho nacho!
Dr Lawi Mshana - Empowerment facilitator