Ticker

6/recent/ticker-posts

JE WEWE NI MTU WA DINI AU NI MTU WA UFALME?


 JE WEWE NI MTU WA DINI AU NI MTU WA UFALME?

Wengi wetu tuna sifa za kuwa watu wa dini tu na sio kuwa wana wa Ufalme. Tunasahau kwamba dini ni juhudi ya mwanadamu katika kumtafuta Mungu, wakati wokovu ni mpango wa Mungu katika kumtafuta mwanadamu. Bwana Yesu hakuleta dini duniani! Alicholeta ni wokovu.

Tofauti ya Adamu na Yesu Kristo

Adamu wa kwanza alikuwa nafsi iliyo hai (living being) wakati Adamu wa mwisho (Yesu) ni roho yenye kuhuisha (life-giving Spirit).1 Wakorintho 15:45 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.”

Kazi kubwa aliyokuwa amepewa Adamu sio kuabudu bali ni KUTIISHA DUNIA NA KUTAWALA VIUMBE. Mwanzo 1:28 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”

Bwana Yesu alikuja kutangaza UREJESHO WA UTAWALA AU UFALME WA MUNGU DUNIANI baada ya Adamu kutuuza kwa shetani. Luka 8:1 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye.”

Ndiyo maana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake waombe kwamba UFALME WA MUNGU UJE DUNIANI – yaani, tumpokonye shetani utawala na kuurudisha kwa Mungu. Mathayo 6:9,10 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje. Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.”

Maana ya WOKOVU

Maana halisi ya kuokoa (sozo) ni kumfanya mtu awe mzima katika maeneo yote ya maisha na sio kiroho peke yake. Mungu anataka tufanikiwe kiroho, kihisia, kimwili na kimaisha. 3 Yohana 1:2 “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.”

Kimsingi, wokovu sio kuhama kutoka dini moja kwenda nyingine bali ni kutoka katika ufalme wa giza na kuingia katika Ufalme wa Mungu. Tuna watu baadhi ya waumini kwenye makanisa yenye imani sahihi ambao bado hawajahama kutoka ufalme wa giza na kuingia katika Ufalme wa Mungu. Wengine waliongozwa sala ya toba lakini moyoni hawajatubu badoo. Wakolosai 1:13 “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.”

Utajuaje kwamba wewe ni mtu wa Ufalme?

Utaona kwamba unamiliki hapa duniani na kugusa maisha ya watu bila mipaka ya kidini na kimadhehebu. Ufu 5:10 “ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Tofauti ya dini na ufalme

1. Dini inatafuta kumfikia Mungu, Ufalme wa Mungu unatafuta kumfikia mwanadamu.

2. Dini inatafuta kuepuka dunia, Ufalme unatafuta kuibadilisha dunia.

3. Dini inamuandaa mtu kuondoka duniani, Ufalme unamuandaa kutawala dunia.

4. Dini inalenga zaidi mbinguni, Ufalme unalenga zaidi duniani na mbinguni. 

Kwa kifupi mtu anaweza kuingia katika dini na awe bado hajaingia katika Ufalme wa Mungu. Lakini pia mtu anaweza kuwa kiongozi wa dini na awe anawazuia watu kuingia katika Ufalme wa Mungu. Mt 23:13-15 13 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. 14 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi. 15 Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. 

Hitimisho:

Tafadhali msininukuu vibaya kwamba nimesema dini haina maana. Nimependa tu kukukumbusha kwamba unaweza kuwa maskini na kukosa ufanisi kama utajali tu kuwa mtu wa dini na kusahau kuwa mtu wa Ufalme. Lakini pia unaweza kukosa thawabu kwa sababu unasubiri kwenda mbinguni na kusahau kazi uliyopewa ya kumiliki na kutawala dunia.

Hii ndiyo sababu inayonifanya nishirikiane na serikali, jamii, mashirika na taasisi za dini katika maeneo ambayo tunakamilishana.

Dr. Lawi Mshana, 0712-924234