Ticker

6/recent/ticker-posts

ZINGATIA MAELEKEZO YA MUNGU KULIKO MATAKWA YAKO AU YA WATU


ZINGATIA MAELEKEZO YA MUNGU KULIKO MATAKWA YAKO AU YA WATU

Hivi karibuni nimepata maono kuhusu mtu fulani ambaye analazimisha kutumika mahali fulani na kwa watu fulani wakati watu hao hawaonyeshi kuguswa na huduma yake.

Nitatumia ushuhuda wa mtume Paulo kuelezea maono hayo kupitia Mdo 22 kuanzia mstari wa 12.

1. Thibitisha kwamba Mungu amekuita kwa ajili ya huduma unayoifanya. Usitegemee kutumwa na watu au kujitolea mwenyewe peke yake.

Mdo 22:12-15 “12 Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, 13 Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. 14 Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. 15 Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.

Tunaona mtume Paulo akitoa ushuhuda wake jinsi alivyokutana na Yesu na namna Bwana Yesu alivyochagua kumtumia Anania kumuandaa na kumpatia taarifa zingine za ziada kuhusu utumishi wake. Mungu hapendi tuwe na kiburi cha kumsikia Yeye tu bila uthibitisho kupitia kwa watumishi Wake wengine. Hata alipomtuma Bwana Yesu duniani aliwatumia manabii wengi na malaika kuthibitisha yale aliyokusudia kumtumia Bwana Yesu kuyafanya. Hakikisha kuna mashahidi waaminifu wa yale unayosema umeambiwa na Mungu na ambao wanaweza kuendeleza maono uliyopewa. 2 Wakorintho 13:1 “Hii ndiyo mara ya tatu ya mimi kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.” 2 Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

Hivyo Mungu alimwambia Anania kuhusu makundi ya watu ambayo mtume Paulo ametumwa kuyafikia. Mdo 9:15 “Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.”

Je wewe umetumwa hasa kulenga kundi gani? Uko chini ya viongozi wanaotambua na kuthamini kusudi la Mungu kwako?

Paulo alipoenda kutambulisha maono yake kwa mitume walimuelewa, wakampa mwongozo na kumuunga mkono. Wagalatia 2:9,10 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara. ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya.”

2. Timiza matakwa yote ya utambulisho wako katika huduma – hata watumishi wa dunia hii hawafanyi kazi bila kitambulisho cha kazi

Mdo 22:16 “Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.”

Hata kama umemsikia Mungu akisema na wewe, hakikisha unatimiza vigezo vyote vya utumishi wako. Kuna watu wanadhani kwa vile Mungu anawapa mafunuo na kuwatumia kwa miujiza hawana haja ya kutimiza matakwa muhimu. Bwana Yesu hakuwa na dhambi lakini alijua anawajibika kutimiza haki yote. Hivyo hakukubaliana na wazo la Yohana Mbatizaji kwamba yeye hahitaji ubatizo wa maji. Mt 3:13-15 “Wakati huo Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohana ili abatizwe. Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.”

 3. Usilazimishe kuwafikia watu ambao Bwana hajakupa kibali kwao

Mdo 22:17,18,21 “Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho, nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu. Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.

Mtume Paulo alipewa ujumbe kwamba atafikia makundi makuu matatu (Mataifa, Wafalme na Waisraeli), lakini hakujua utaratibu utakuwaje na anatakiwa aanze na kundi gani. Matokeo yake akaingiza ubinadamu kwa kulenga zaidi ndugu zake Waisraeli kabla ya wakati wake. Kilichomsaidia ni kwamba aliendelea kuisikia sauti ya Mungu na kuitii. Hakikisha unamsikia Mungu unapokuwa katika maombi ili ufuate maelekezo Yake kwa wakati.

Mambo ambayo Bwana Yesu alimwambia Paulo katika roho akiwa anaomba:

1. Huduma yako Yerusalemu haitakuwa na matokeo ninayoyataka hivyo uondoke upesi. Hawataikubali huduma yako wakati huu. Sijakupa kibali cha kuwafikia kwa sasa. Kama angelazimisha, angekufa kwa ujinga ingawa tungesema amekufa kama shahidi.

2. Watu wa Mataifa wataipokea huduma yako na italeta matokeo ninayoyataka. Ina maana ni watu ambao hawako katika mpango wako kwa sasa lakini wataipokea huduma yako.

Hitimisho

Usipuuze maelekezo unayopewa na Roho wa Mungu hata kama watu hawatakuelewa.  Hima toka hapo katika mazoea yako (comfort zone), usije ukapata mateso ambayo hayatakupa thawabu mbele za Mungu.

Lakini pia usipime matokeo kwa macho ya kibinadamu. Mtume Paulo aliposema ameumaliza mwendo, hakufika Tanzania. Alijua ukubwa na mipaka ya huduma yake na kuitimiza. 2 Timotheo 4:7 “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda.”

Tambua Bwana alikukamata kwa ajili gani ili usije ukadhani umefanikiwa kwa kutimiza vigezo vya dhehebu lako na kumbe hujaanza ile kazi maalum unayotarajiwa na Mungu. Wafilipi 3:12 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu.”

Bwana atakayetulipa siku ya mwisho atujalie kufanya kazi anayotutarajia.

Barikiwa na Bwana.

Dr Lawi Mshana, 0712-924234