Ticker

6/recent/ticker-posts

KUTAMBUA DALILI NA ATHARI ZA MTOTO ALIYEBAKWA



 KUTAMBUA DALILI NA ATHARI ZA MTOTO ALIYEBAKWA

Ubakaji wa mtoto kitendo cha mtu mzima kumchukua mtoto na kufanya naye ngono au vitendo vya kingono kama vile kumuingilia mtoto kingono, kushikashika sehemu za siri za mtoto; mtoto kuchezea sehemu za siri za mtu mzima; kumuonyesha mtoto picha za ngono nk.

Kumbuka mtu mzima hayuko salama kwa kusema mtoto ndiye alimshawishi kwa vile mtoto anachukuliwa kwamba hajakomaa kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yake. Hivyo mtu mzima lazima atawajibika hata kama mtoto ndiye alimshawishi kufanya hivyo. Anahesabika kwamba ni yeye amemrubuni mtoto. Ni wajibu wa mtu mzima kujiwekea mipaka na kumsaidia mtoto kutambua makosa ya kisheria na kimaadili. Baadhi ya watu wazima wamejiingiza katika matatizo kutokana na kuamini misemo kama vile ‘umri ni idadi tu,’ ikimaanisha kwamba umri sio kikwazo cha kuwa na mahusiano ya kingono.

Usisahau kwamba kwa nchi yetu mtu mwenye umri chini ya miaka 18 ni mtoto hata kama ukimtazama kimwili anaonekana ameshakuwa mtu mzima. Mtu anaweza kubalehe au kuvunja ungo akiwa na miaka kati ya 10-15 lakini akili inaendelea kukua hadi umri wa miaka 25 ndipo ubongo umekomaa vizuri. Kwa hiyo mtu anaweza kubeba au kutia mimba lakini hajakomaa bado kiakili kukabiliana na changamoto za kifamilia.

Mara nyingi watoto wa kike na wa kiume hunajisiwa na watu wanaowafahamu – mfano, baba mlezi, mama mlezi, mjomba, shangazi, kaka, dada, ndugu wengine, mfanyakazi wa nyumbani, au majirani.

Sababu ziko nyingi lakini baadhi ni kuwa na ukaribu usio na mipaka (mazingira hayaruhusu kujiheshimu kimavazi), watoto kulala chumba kimoja na wageni, kutojali kujua mazingira tunapowaruhusu watoto watembelee ndugu (wanalala chumba kimoja bila kujali umri na jinsi), migogoro ya ndoa, vifungo vya mapepo (mtu anawakwa tamaa na kushindwa kujizuia), kutafuta utajiri kwa masharti ya kichawi nk

Kisa cha kweli:

Siku moja mwanamke fulani alishangaa usiku akiwa amelelala kuona mtoto wake mdogo akimpapasa sehemu za siri ili amsugue (amsage). Alipofuatilia kujua amejifunzia wapi aligundua kwamba amefundishwa na mfanyakazi wa ndani anayemuacha amlee mtoto yeye akiwa ameenda kazini.

Baadhi ya dalili za mtoto aliyebakwa ni hizi zifuatazo:

1. Mtoto anakuwa na tabia ya kuwaogopa watu mf hawezi tena kubadili nguo mbele ya wenzake

2. Mtoto anakuwa na mabadiliko ya ghafla ya tabia – kama vile kuanza kutokwa na haja kubwa bila udhibiti nk

3. Mtoto anajaribu kuwashawishi watoto wenzake wafanye naye ngono

4. Mtoto anapenda kuzungumza masuala ya ngono

5. Mtoto anapenda kuchora watu wakifanya tendo la ngono

6. Mtoto analalamika kwamba ana maumivu katika sehemu zake za siri

7. Mtoto anakuwa na michubuko sehemu za siri

8. Mtoto anashindwa kutembea kutokana na maumivu

9. Mtoto anakosa raha na kupenda kujitenga

10. Mtoto anajiepusha kutazamana usoni na mtu yeyote

Baadhi ya athari za mtoto aliyebakwa

1. Mtoto kuwa mwoga

2. Mtoto kushindwa kuwaamini watu

3. Mtoto kujisikia mnyonge, asiye na thamani

4. Mtoto kujaa hisia za uchungu na kulipiza kisasi

5. Mtoto kupata hisia za kujiua

6. Mtoto kupata VVU au magonjwa mengine ya ngono

7. Mtoto kuwa mraibu wa ngono (sex addict) akizoea hali hiyo

Tutaendelea kujifunza mengine zaidi.

Jisajili (subscribe) kama una barua pepe (email) ili kila tukiandika Makala mpya uipate moja kwa moja.

Dr. Lawi Mshana, Mkurugenzi, Beyond Four Walls