TUNAWEZAJE KUWANUSURU WACHUNGAJI WASIPATE MAUMIVU KATIKA MAISHA YAO? (Sura ya 3)
Naendelea na muhtasari wa sura ya tatu ya kitabu cha Kilio cha Wachungaji
Sura ya Tatu (kwa muhtasari)
Kuwanusuru Wachungaji kutoka katika Maumivu
1.
Mateso yanaporuhusiwa na Bwana, yanaweza kumuimarisha mchungaji. 1 Pet
5:10 ‘Na Mungu wa neema yote, aliyewaita
kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda
kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu’. Mchungaji anatakiwa kuyapokea mateso ya
kimungu kwa mtazamo mzuri ndipo yatatumiwa kama mawe ya kumsaidia kuvuka
ng’ambo ya pili (stepping stone). Mungu haruhusu mateso kwa ajili ya kumvunja
moyo mtumishi wake. Kinachoweza kumuumiza mchungaji, ni namna yeye mwenyewe
anavyoyatafsiri au kuyapokea mateso anayoyapata. Akiwa tayari kujifunza kusudi
la Mungu ndani ya mateso hayo, yatakuwa baraka kwake. Lakini akilalamika na
kuhamishia lawama kwa watu wengine, mateso hayo yatamfanya awe mchungu.
Ukiitikia vyema (respond) mateso, yanaweza kukufanya uwe mzuri (better) lakini
ukiitikia vibaya (react), yanaweza kukufanya uwe mchungu (bitter). Kuna mfano
mzuri wa watu wawili waliowahi kutukanwa kwamba ni mbwa. Mmoja akasema najua
hata siku moja siwezi kubweka hivyo akapuuzia lakini mwenzake akawaza sana mbwa
alivyo na mdomo mrefu na jinsi alivyofananishwa naye, akaamua kupambana.
Kinachotuathiri na kutuumiza mara nyingi sio maneno yanayosemwa juu yetu bali
ni namna tunavyoyatafsiri maneno hayo.
2.
Mchungaji anahitaji kupata malezi kutoka kwa watu anaowatumikia. Ili
mchungaji aifurahie kazi yake, anahitaji kanisa analolisimamia liweze
kutosheleza mahitaji ya msingi ya familia yake. Mchungaji anajisikia vizuri
sana anapoona kwamba anamudu kujikimu kwa sababu ya utoaji wa kanisa lake
kuliko kwa kufanya kazi zake binafsi. Hapa sina maana kwamba ni vibaya
mchungaji kuwa na shughuli binafsi inayomuongezea kipato. Mchungaji anaweza
kuwa na shughuli ya kuongeza kipato kama mtume Paulo alivyoshona mahema (Mdo
18:2,3) ili mradi shughuli hiyo isimchukulie muda wa kumtumikia Mungu katika
wito wake. Mchungaji ambaye anaishi kwa kutegemea zaidi kazi zake binafsi
anaweza kukosa mzigo na muda wa kulea kanisa analochunga. Hata hivyo, mchungaji
asijisahau pale kanisa linapojitahidi kumtunza. Aonyeshe shukurani hata kama
kanisa halijafikia matarajio yake bila kusahau kwamba hakuajiriwa na kanisa
(washirika) bali ameajiriwa na Mungu ambaye ana njia nyingi za kumbariki. Hata
Bwana Yesu, si kila aliyemhudumia kiroho alihusika katika kutimiza mahitaji
yake ya kimwili. Maandiko yanataja watu wachache tu ambao walimhudumia Bwana
Yesu kwa mali zao (Lk 8:3).
3.
Mchungaji anahitaji kutambuliwa kibinadamu (human understanding) kama walivyo
waumini. Mchungaji anaweza kuwa mpweke katika kundi lake mwenyewe
kama hakuna mtu anayetambua hisia zake. Mtu mwenye ufahamu wa rohoni akimwona
mchungaji wake anakuwa mkali kupita kiasi, hatalaumu na kutafuta kuhama kanisa
bali atatafuta kujua nini kinaendelea katika maisha ya mchungaji wake. Kama
mchungaji ameshindwa kulipa ada ya mtoto wake au amelala njaa, hawezi kuwa na
mahubiri yenye baraka. Kanisa lina wajibu wa kujua changamoto anazopitia
mchungaji wake na kuzitafutia ufumbuzi hata kwa maneno tu ya kutia moyo. Maneno
yanayotia moyo wachungaji ni maneno kama vile kazi yako ni njema, uwe na moyo
mkuu na maneno mengine kama hayo. Tusiwe na macho yanayoona madhaifu ya
wachungaji peke yake bali pia tuone uwezo wao au mazuri yao. Na hata kama
wamekosea leo, tusisahau walivyowahi kutusaidia kabla hawajakosea. Hata kama
baba yako mzazi atakosea leo, bado utaendelea kumuita baba. Mbona baba zetu wa
kiroho tunawasahau mapema sana? Paulo alipokataliwa kama mtume alisema wengine
wanaweza kunikataa lakini sio ninyi. 1 Kor 9:2 ‘Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu
ninyi’. Usipende kufuata mkumbo katika kumkataa mtumishi wa Mungu ambaye
amewahi kuwa hazina kwako.
4.
Mchungaji anahitaji washirika wampende, wajitiishe katika uongozi wake na
wamuombee. 1 The 5:12,13 ‘Lakini,
ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia
ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya
kazi zao’. Mchungaji akifanyiwa
matendo ya upendo naye ataitikia kwa huduma yenye upendo. Ingawa mchungaji
amepewa huduma hii na Bwana, bado anahitaji mwitikio mzuri wa watu
anaowaongoza. Tusione ni wajibu wake kututumikia hata kama hatuonyeshi matendo
ya huruma na upendo kwake. Kama anaagiza jambo na wewe ukashindwa kulitekeleza,
jifunze kumjulisha mapema au kumuomba samahani ili asikudhanie kwamba
umemdharau. Hata kama umemzidi umri,
elimu au kipato; jifunze kujitiisha kwake kwa vile hutapoteza chochote kwa
kufanya hivyo. Kama unashindwa kumheshimu kwa sababu zingine, mheshimu tu kwa
ajili ya kazi yake aliyopewa. Kumbuka mchungaji akitumika kwa huzuni, kanisa
linakosa baraka. Ebr 13:17 ‘Watiini wenye
kuwaongoza na kuwanyenyekea …ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa
kuugua; maana isingewafaa ninyi’. Ingawa mchungaji amepewa mamlaka na
wajibu wa kuwaombea wengine, anahitaji pia kuinuliwa kwa maombi kutoka kwa watu
anaowahudumia.
Kipindi
kijacho utajifunza kuhusu MAOMBI KWA AJILI YA MCHUNGAJI NA FAMILIA YAKE
Mwaliko
Tunajiandaa kumaliza mwaka
na kuanza mwaka mwingine. Huduma tunayofanya inagusa na kujengea uwezo jamii
bila kubagua dini wala dhehebu. Tunakualika uungane nasi kama rafiki-mwenza au
mdau (partner) kwa mwaka 2025. Sio mpango wa Mungu umtumikie kiroho peke yake.
Wewe una ujuzi, uwezo na uzoefu mkubwa ambao huutumii kwa ajili ya ufalme wa
Mungu bali unautumia tu kazini kwako na katika maisha yako binafsi. Zipo huduma
unazoweza kuzifanya hata kama uko mbali nasi. Shiriki katika maono haya yanayogusa
ulimwengu mzima. Yapo mataifa ambayo haingekuwa rahisi kuyafikia lakini kupitia
maono haya tumeweza kuyafikia.
Njia rahisi kuwasiliana nasi
kwa ajili ya ufafanuzi zaidi kupitia hapa chini kwenye tovuti (angalia sehemu
yenye kichwa cha WASILIANA NASI) au baruapepe (info@lawimshana.com) au
kupitia Whatsapp (0712-924234).
Wewe ni mtu muhimu sana
kwetu na mbele za Mungu.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234, Korogwe,
Tanga, Tanzania


