TUNAWEZAJE KUWAOMBEA WACHUNGAJI NA FAMILIA ZAO? (Sura ya 4)
Naendelea na sura ya nne ya kitabu cha Kilio cha Wachungaji kwa muhtasari.
Sura ya Nne (kwa muhtasari)
Kuwaombea Wachungaji na Familia zao
Mungu amemuita mchungaji na kumpaka mafuta kwa ajili ya kuchunga kanisa lake. Mdo 20:28 ‘Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe’. Ufanisi au moto wa huduma ya Mchungaji siku zote unalingana na kiwango cha maombi ya kanisa kwa ajili yake. La kusikitisha ni kwamba washirika wengi ambao wanawanung’unikia wachungaji wao, hawajawahi kuwaombea kwa uzito. Hawajui kwamba roho mbaya zinaweza kuwaingia wachungaji wao kama hawatasimama mahali palipobomoka kwa ajili yao.
Miongoni mwa mambo muhimu katika kumuombea mchungaji ni haya yafuatayo:
1. Siku zote awe na shauku ya kumjua Kristo zaidi. Fil 3:10 ‘ili nimjue Yeye, na uwezo wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake’; Efe 1:17 ‘Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua Yeye’. Mchungaji asipomjua Kristo kwa kina hatakuwa na ushirika wa karibu naye hivyo anaweza kutumia muda mwingi kusoma magazeti na kuangalia televisheni kuliko kutekeleza majukumu yake ya kiroho na kihuduma.
2. Atumike katika roho ya unyenyekevu. Yak 4:10 ‘Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza’; 1 Pet 5:6 ‘Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake’; Zab 25:9 ‘Wenye upole atawaongoza katika hukumu, wenye upole atawafundisha njia yake’. Mchungaji akiwa mnyenyekevu, Mungu mwenyewe atamuinua na kumuongoza. Mchungaji anahitaji kuwa mtumishi-kiongozi. Aweze kuwaelekeza watu na kuwapa majukumu lakini pia aweze kuwatumikia kwa upendo.
3. Atumike katika Roho wa uweza. 1 Kor 2:4-5 ‘Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu ya Mungu’; Rum 15:13 ‘Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu’. Mchungaji amtegemee Roho Mtakatifu katika utumishi wake badala ya kutegemea uzoefu wake na elimu yake ya kidunia au ya kidini. Asipotumika katika uweza wa Mungu, atachoka haraka na kukata tamaa anapokutana na vikwazo vya kiutumishi na pia atashindwa kuwasaidia watu wenye madhaifu mbalimbali ambao ni wengi makanisani.
4. Awe mtu wa maombi na Neno ili aishi maisha safi. Zab 119:10-11, 35-37 ‘Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, usiniache nipotee mbali na maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, nisije nikakutenda dhambi. Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, kwa maana nimependezwa nayo. Unielekeze moyo wangu na shuhuda zako, wala usiielekee tamaa. Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako’. Mchungaji akiwa mtu wa maombi, atagundua kwa wepesi mitego ya adui na vilevile atamsikia na kumuelewa Mungu kwa haraka anaposema naye. Si hivyo tu lakini pia atajua jinsi ya kuyatenda mapenzi ya Mungu na kuinasua mitego ya shetani. Neno la Mungu likijaa kwa wingi ndani yake, litamfanya awe na maamuzi sahihi ya ki-Mungu.
5. Alindwe dhidi ya mashambulizi ya adui. 2 The 3:3 ‘Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu’. Ili mchungaji ashinde majaribu na kuwa na ushuhuda mwema, anahitaji kuzungushiwa wigo wa kumlinda. Anahitaji kulindwa dhidi ya roho za ajali, wachawi, maneno yanayoumiza, magonjwa, dhambi, majambazi na hila zote za shetani. Anahitaji ulinzi akiwa nyumbani kwake, safarini na katika huduma.
6. Familia yake pia ifanikiwe:
(i). Awe kimbilio la watoto wake. Mit 14:26 ‘Kumcha BWANA ni tumaini imara; watoto wake watakuwa na kimbilio’; Zab 34:11 ‘Njoni, enyi wana, mnisikilize, nami nitawafundisha kumcha BWANA’. Baadhi ya wachungaji wanasahau familia zao na kusababisha watoto wao wakose malezi bora na hatimaye kujihusisha na vitendo vya kihalifu. Mchungaji anatakiwa kushirikiana na mkewe au mumewe katika kuwalea watoto. Asiwe baba au mama asiyepatikana kwa watoto wake.
(ii). Abarikiwe na kuwa na furaha. Zab 112:1-2 ‘Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, apendezwaye sana na maagizo yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; kizazi cha wenye adili kitabarikiwa’; 2 The 3:16 ‘Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote’. Mchungaji akiwa na baraka za kimwili na za kiroho, anakuwa na moyo zaidi katika kumtumikia Mungu na kuwatumikia watu wake kuliko akiwa na madeni mengi na akiwa hana uhakika wa kupata mahitaji ya msingi ya familia yake.
(iii). Aongoze familia yake vyema ili watoto wawe na heshima. 1 Tim 3:4-5 ‘Mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)’. Kipimo cha mtu kuwa mchungaji mzuri ni uwezo wake katika kuisimamia nyumba yake na kutiisha watoto wake. Mchungaji aweze kupanga majukumu na kuweka kanuni za nyumba yake. Pia aweze kuwasaidia watoto wake kupambanua jema na baya na kujua mipaka yao wakiwa ndani na nje ya nyumba yake.
(iv). Ampende na kumjali mwenzi wake wa maisha ili maombi yake yasizuiliwe. Efe 5:22,25 ‘Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake’; 1 Pet 3:7 ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’. Mchungaji aweze kuchukuliana na mkewe bila kumdharau wala kumpuuza. Asiwe tu mchungaji mzuri kanisani bali pia awe mume mzuri nyumbani. Wakati mwingine mke akimsikiliza mwenzi wake (mchungaji) akihubiri kanisani anamuona ni mtu tofauti sana na anavyoonekana akiwa nyumbani kama mumewe.
(v). Nyumba yake imtumikie Bwana. Yos 24:15 ‘Ninyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia
BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu
waliitumikia ng’ambo ya mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa
katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA’. Huduma ya
mchungaji iwe na mvuto kwa familia yake ili asitumike peke yake. Familia
ikimuunga mkono katika huduma atafanikiwa zaidi kwa vile familia iko karibu
naye wakati mwingi kuliko kanisa ambalo linakutana tu kwa vipindi vichache kwa
wiki.
Kipindi
kijacho utajifunza kuhusu MATENDO YA KUMTIA MOYO MCHUNGAJI NA FAMILIA YAKE
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania