Ticker

6/recent/ticker-posts

UNAJUA MAUMIVU WANAYOPITIA BAADHI YA VIONGOZI WA IMANI? UNAJUA MADHARA YAKE KWAKO? (Sura ya 1)


UNAJUA MAUMIVU WANAYOPITIA BAADHI YA VIONGOZI WA IMANI? UNAJUA MADHARA YAKE KWAKO? (Sura ya 1)

Mwezi Novemba na Desemba 2024 nitautumia katika kuzungumzia kwa muhtasari ujumbe ambao Mungu alinipa mwaka 2011 na kunielekeza kuandika kitabu wakati huo kinachoitwa KILIO CHA WACHUNGAJI. 

Kitabu hicho kina sura zifuatazo:

Sura ya 1: Aina za Maumivu ya Wachungaji

Sura ya 2: Sababu Kuu za Maumivu ya Wachungaji

Sura ya 3: Kuwanusuru Wachungaji kutoka Katika Maumivu

Sura ya 4: Maombi kwa Ajili ya Mchungaji na Familia yake

Sura ya 5: Matendo ya Kumtia Moyo Mchungaji na Familia yake

Sura ya 6: Maswali kwa Ajili ya Mchungaji Kujihoji Kibinafsi

Pengine unajisemea moyoni kwamba ujumbe huu haukuhusu kwa vile wewe sio kiongozi wa imani. Napenda ujue kwamba mtumishi wa Mungu akihuzunika kwa sababu yako unakaribisha laana katika maisha yako. Waebrania 13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.”

Ni ukweli usiopingika kwamba wakosoaji wakuu na wanaonyoshea kidole madhaifu ya viongozi wao wa imani HAWAJAWAHI KUWAOMBEA WALA KUTAFUTA NJIA YOYOTE YA KUWASAIDIA. Wakati wote wanawachukulia kwamba wanawakosea kwa makusudi.

Unajua kama mnazungumzia udhaifu wa mchungaji wenu halafu baada ya hapo mkamuombea, mkamshauri au kumtahadharisha, hamjakosea? Mnakosea pale mnapozungumzia udhaifu wake halafu baada ya hapo mnatawanyika bila mkakati wowote wa kumuombea wala kumsaidia. Najua sio viongozi wote wako tayari kushauriwa au kutahadharishwa lakini wewe timiza wajibu wako ila hakikisha unaongea nao kwa hekima. Wakolosai 4:6 “Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” Mithali 12:15 “Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.”

Nitaeleza sura za kitabu hatua kwa hatua kwa kifupi. Lakini unaweza kusoma kwa kina zaidi kupitia kwenye tovuti yangu (www.lawimshana.com).

Sura ya Kwanza (kwa muhtasari)

Aina za Maumivu ya Wachungaji

Kukosa walezi wa kiroho na kihuduma, kukosa usalama wa maisha ya familia zao, upweke na uchovu, kushindwa kufikia matarajio, na kusalitiwa

1. Kukosa walezi wa kiroho na kihuduma

·       Wapo wachungaji wengi ambao wana viongozi wanaowasimamia lakini hawana baba wa kuwalea na kuwashauri. Mtu anaweza kuwa kiongozi wako na asiwe mlezi wako.

·       Wachungaji wengi hawana mtu wanayeweza kumwonyesha hisia zao za kuchoka na kukata tamaa. Hivyo wana maumivu mengi yaliyovia ndani ambayo yanawafanya wawe na uchungu mioyoni na kukosa maneno yanayobariki. Dalili hizi zinajidhihirisha katika mahubiri yao yasiyo na shukrani, yaliyojaa lawama na yenye matamshi ya kulaani hasa pale uwajibikaji wa waumini wao unapopungua.

2. Kukosa usalama wa maisha ya familia zao.

·       Wachungaji wengi wanamtumikia Mungu lakini hawana uhakika wa maisha ya baadae ya familia zao hasa wakati wakichoka au wakipumzishwa na Bwana.

·       Upo tu utaratibu mzuri wa kanisa katika kumiliki mali kama vile majengo na viwanja. Ni vyema pia mchungaji akaandaliwa kumiliki vitu vyake mwenyewe ili akimaliza muda wake wa utumishi asitelekezwe, asiwe ombaomba wala asililemee kanisa bali aweze kujitegemea.

·       Kama kweli mchango wa huduma ya mchungaji unathaminiwa, kanisa linapaswa kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadaye ya mchungaji wao. Kanisa linaweza kumsaidia katika ujenzi wa nyumba yake binafsi au kumuwekea fedha katika mfuko wa hifadhi ya jamii wakati bado analitumikia kanisa. Ni aibu kwa kanisa kuwa na wachungaji waliochoka na ombaomba baada ya kumaliza muda wao wa utumishi wa miaka mingi.

·       Wakati mwingine wahubiri wageni wanaotembelea kufanya semina na mikutano ya injili ndio wanaonufaika na michango mikubwa kuliko wachungaji wenyeji kwa sababu washirika hawatambui uzito wa huduma za wachungaji wao.

3. Upweke na uchovu.

·       Wachungaji wengi wamelemewa na mizigo ya washirika wao inayozidi uwezo wao wa kuibeba. Wakati huohuo wachungaji hawa, hawana watu waliowazunguka wanaoweza kuwatia moyo. Ingawa wapo wazee wa Kanisa, baadhi yao hawaoni kwamba kumhudumia mchungaji na nyumba yake ni kazi ya Mungu pia.

·       Wachungaji wanapokosa watu wa kuwainua katika maombi, wanachoka na kuzimia. Matokeo yake waumini wa makanisa yao wanashindwa katika majaribu na kuanguka. 

·       Vilevile, kuna wachungaji wanadhani kwamba ni dhambi kwa mtumishi wa Mungu kupumzika akiwa bado duniani. Wanasahau kwamba kupumzika sio uvivu bali ni agizo la Bwana. Tena sio mwanadamu peke yake anayetakiwa kupumzika bali hata mashamba.

·       Unapofanya huduma bila kujali kupumzika unakosa maono mapya, unamtumikia Mungu kwa mazoea, unazoeleka mbele za watu kupita kiasi na unapungua katika ufanisi na ubora wa huduma yako. Hata wanasayansi wamefanya majaribio wakagundua kwamba mnyama anayetengewa muda wa kupumzika, anafanya kazi kwa ufanisi zaidi kuliko yule ambaye hapewi muda wa kupumzika.

4. Kushindwa kufikia matarajio.

·       Mchungaji anaumia moyoni anapoona kwamba pamoja na juhudi anazofanya hafikii matarajio yake binafsi, ya kanisa analochunga na ya uongozi wa juu wa kanisa lake. 

·       Anaumia zaidi anapokuwa ametumia muda mrefu kuandaa ujumbe wa Neno la Mungu halafu anapofika ibadani anakuta watu wengi hawajafika tena bila taarifa yoyote. Anajisikia kwamba huduma yake na taabu yake haitambuliwi wala haithaminiwi.

·       Wakati mwingine waumini wanafika ibadani wakiwa wamevaa nguo za thamani kubwa lakini hawana Biblia, daftari wala kalamu. Wanaitikia mahubiri kwa kutikisa tu vichwa, lakini hawaandiki chochote.

·       Lakini pia inaumiza mchungaji anapotarajiwa kutoa michango mingi katika ngazi za juu za dhehebu lake wakati ameshindwa kutimiza mahitaji muhimu ya maisha kama vile kulipa ada ya mtoto wake. Anavunjika moyo anapoona kwamba hakuna anayejali hata kumuuliza tu kuhusu maendeleo ya familia yake. Wakati mwingine sio tu wasimamizi wake wanaomsahau lakini pia hata washirika anaowachunga. Jambo hili linachangia kuwafanya watoto wa wachungaji kuidharau kazi ya uchungaji.

·       Mchungaji anaposhindwa kutimizia mahitaji ya msingi ya familia yake, anavunjika moyo na kupoteza heshima kwa familia yake. Mwenzi na watoto wake hawawezi kumuelewa Mungu kupitia mahubiri ya kanisani ambayo hayaendani na hali halisi ya maisha ya nyumbani. Tusiwalazimishe watoto kuingia katika wito ambao hawakuitiwa!

5. Kusalitiwa

·       Mchungaji pia anaumia sana anapowekeza mambo mengi katika mioyo ya kondoo zake halafu wengine wanamsaliti kwa kuamua kuhamia huduma nyingine bila sababu yoyote ya msingi na bila kumuaga. Hata hivyo, pamoja na kuwa na sababu yoyote nzuri, mtu hapaswi kuondoka vibaya kanisani kama anataka kubarikiwa huko aendako.

·       Wakati mwingine Mchungaji anaweza kumuandaa mshirika wake mmojawapo ili amsaidie huduma halafu baadaye mshirika huyo anatumia ujuzi huohuo kumpindua au kummegea kanisa. Mara nyingi adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe.

·       Sio wakati wote kukimbiwa na washirika kunatokana na tatizo la kiongozi. Wakati mwingine, washirika wenyewe hawako tayari kujifunza mafundisho yanayohitaji kujikana nafsi. Tukiogopa kukimbiwa, tutachunga hata wajumbe wa shetani ambao mwisho wake wataturarua sisi wenyewe.

·       Wapo wachungaji waliowapeleka vijana wao kusoma chuo cha Biblia na waliporudi wakasahau walikotoka na kuanza kuwakejeli wachungaji wao na kupandikiza mbegu mbaya kwa waumini wenzao.

·       Wapo pia wachungaji waliowapokea watumishi wageni na kuwapa nafasi kuhubiri katika makanisa yao halafu baadaye watumishi hao wakamega kundi na kufungua kanisa jirani nao.

·       Hata hivyo wachungaji tusifanye makosa katika kuchagua watu wa kuwaandaa kwa ajili ya huduma.  Tukumbuke kwamba chuo cha Biblia hakimpi mtu huduma bali kinaweza kumsaidia mtu ambaye tayari amepewa huduma na Bwana. Tunapaswa kuona huduma ya mtu kwanza kabla ya kutafuta kumuendeleza ili tuweze kuchagua vizuri aina ya mafunzo yanayomfaa. Lakini pia tusiangalie tu karama za roho na kusahau tunda la roho. Tujiulize kama mshirika tunayetaka kumuendeleza kihuduma ana tabia inayofaa kuigwa.

Kipindi kijacho utajifunza kuhusu SABABU KUU ZA MAUMIVU YA WACHUNGAJI

Angalia mahali palipoandikwa Books (Vitabu), kisha bofya ‘Kilio cha Wachungaji,’ utaweza kusoma utangulizi na sura hii kwa kina.