Ticker

6/recent/ticker-posts

Njia nyepesi ya kupata pesa ya kuwekeza


Njia nyepesi ya kupata pesa ya kuwekeza

Pengine mapato yako kwa mwezi hayatoshi kutimiza mahitaji yako kwa mwezi. Usipokuwa na ziada, utakuwa katika madeni maisha yako yote na kamwe hutaona ndoto zako zikiwa kitu halisi. Unaweza kupunguza utegemezi wa mikopo katika kuendesha maisha yako. Deni sio kitu cha kawaida katika uchumi wowote na haitakiwi deni liwe kawaida kwa watu wa Mungu. Kukopa kamwe sio mpango bora wa Mungu kwa watu wake. “Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii….Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi WALA HUTAKOPA WEWE.” (Kum 28:1, 12). Katika mwaka wa maachilio (remission), mwaka wa saba, wayahudi walielekezwa kuwaachilia ndugu zao kutoka katika madeni yoyote. Kum 15:1-2 Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio.Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana. Hivyo, madeni yoyote yaliyozidi miaka saba, yalikuwa kwa watu ambao sio wayahudi. Maandiko yanasema wazi kwamba kukopa na kukopeshwa hakukatazwi, lakini miongozo thabiti imetolewa. 

•Kila andiko linalotaja kukopa halionyeshi kupongeza hali hiyo. Mit 22:7 Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye. 
•Mwongozo wa maandiko kuhusu kukopa uko wazi. Unapokopa, unaahidi kulipa. Kwa lugha nyepesi, kukopa ni kuweka nadhiri, na Mungu anataka tutimize nadhiri zetu. 

Ukizingatia vipengele vifuatavyo unaweza kupata pesa za kuwekeza bila kuwa mtumwa wa mikopo. 

1. Badili mtindo wa maisha yako 
Kama u mpangaji, hamia katika nyumba ya gharama nafuu. Jishushe na Bwana atakukweza kwa wakati wake. Usiige watu wenye kiwango cha maisha tofauti na cha kwako. Endelea kutumia chombo chako cha zamani mf baiskeli, gari, simu au kompyuta, kwa miaka mitatu au zaidi. Nunua kitu kilichotumika (second hand). Baadhi ya vitu hivi ni imara sawa na vipya na bei yake ni nusu ya vipya. Epuka kupeleka mtoto katika shule za bei kubwa bila sababu za msingi. Wakati mwingine anaweza bado kufeli kwa vile hapendi shule bali unamlazimisha tu. Badala ya kumpeleka kidato cha tano kwenye shule ya gharama, ungeweza kumpeleka chuo cha ufundi apate ujuzi na kujiajiri mapema zaidi. 

2. Ongeza ujuzi wako 
Soma zaidi upate cheti, stashahada au shahada. Kaa na mtu mwenye ujuzi upate uzoefu zaidi. Unaweza kujifunza kwa njia isiyo rasmi bila hata kupata cheti na bado ukafanikiwa. Pata ujuzi zaidi wa shughuli yako Mf kama wewe ni mama wa nyumbani unaweza kujifunza kupika keki nzuri zaidi ya unazozipika au zinazopikwa kwa sasa. Kwa njia hii unaweza kuvutia wateja zaidi. 

3. Badilisha kazi 
Unaweza kubadilisha kazi. Usiishi kwa mazoea. Inawezekana kuna kazi unayoweza kuifanya yenye kipato kizuri zaidi. Hata hivyo kama kazi hiyo ni ya kutoka kijijini kwenda mjini, unatakiwa kuwa mwangalifu. Mshahara wa sh 300,000 mjini unaweza kuwa sawa na mshahara wa sh 100,000 kijijini. Kubadilisha kazi kunaweza kusaidia kama kazi hiyo ina marupurupu mbalimbali au hakuna gharama za ziada kv usafiri kutoka nyumbani kwenda kazini. 

4. Anzisha shughuli yako 
Shughuli yenye mafanikio ni ile ambayo imeanza na kitu unachokipenda (hobby). Ukipenda kitu utaweza kujitoa kisadaka bila kukata tamaa kwa haraka. Shughuli yako mwenyewe inaweza kuongeza kipato chako kuliko kutegemea kuajiriwa tu kwa vile faida yote inakuwa ya kwako. Unapoajiriwa unamegewa tu sehemu ya faida anayoipata mwajiri. 

5. Pangilia raslimali zako 
Kama una raslimali ambazo hazitumiki ni bora kuziuza ili upate pesa za kuwekeza. Mfano, kama una TV mbili na moja unaitumia mara mojamoja sana. Au una magari mawili na moja unalitumia mara chache sana. Hakuna sababu za kukaa na vitu vyenye thamani nyumbani ambavyo havitumiki wakati unahitaji mtaji wa biashara. 

6. Ongeza kasi ya kulipa deni lako 
Ukimaliza deni mapema utaweza kuendelea na uwekezaji. Ukilipa au kupunguza deni unajenga kuaminika (trust). Lazima uwe na kiwango kila mwezi kwa ajili ya kulipa deni lako. Riba unayolipa kwa kukopa ungeiepuka kama ungewekeza ndipo ugharamie kitu unachohitaji. Kinachotakiwa tu ni subira. Watu wengi wanachagua kukopa badala ya kuweka akiba kwanza kwa vile tu hawana subira. Hawako tayari kusubiri hivyo wanakuwa katika utumwa wa madeni. Wengine mpaka wanastaafu bado hawajamaliza madeni. 

7. Geuza ongezeko liwe uwekezaji 
Mara nyingi ongezeko la mshahara na mapato halitumiki vizuri. Ni bora kulitumia ongezeko hilo kwa ajili ya uwekezaji wa muda mrefu. Jiulize baada ya kuongezewa mshahara au kipato, umeweza kuongeza kitu gani kinachoonekana. Kama hakuna, ulichoongeza ni matumizi tu. Kumbuka kuna watu wenye kipato kidogo kuliko wewe lakini wanafanya mambo makubwa kuliko wewe. 

8. Jipatie kipato cha ziada 
Pamoja na kazi au shughuli yako ya sasa unaweza kufanya kazi nyingine kv kufundisha tuisheni baada ya muda wa kazi, kuuza magazeti nk Ili mradi kutafuta pesa kusiwe badala ya muda wa mahusiano na familia. Kuna watu wanatafuta pesa mpaka familia inavunjika. Lazima tujue kwamba pesa tunazotafuta ni kwa ajili ya kuijenga familia. 

9. Epuka gharama zisizo za lazima 
Piga simu zisizo za lazima muda wa usiku. Huna sababu ya kupiga simu mchana wakati ambapo gharama inakuwa juu. Lakini pia huna sababu ya kumpigia simu mtu anayekaa nyumba ya pili (jirani yako). Hakikisha bomba halivuji maji. Unaweza kuongeza bili zisizo za lazima. Tumia balbu za watts ndogo kama sio chumba cha kusomea. Taa za energy saver au za mshumaa (fluorescent tubes) zinakula umeme robo ya ulaji wa balbu. 

Nunua vitu vizuri vilivyotumika badala ya vipya ili mradi uzingatie ubora wake. 

Kumbuka haya yote ni kwa ajili ya kukuandaa uwe na maisha bora hata kama kipato ni kidogo. Matajiri wanajinyima sana mwanzoni na kisha badae wanaishi kifahari. Lengo la makala hii sio kukufanya uishi maisha duni siku zote. 

Kumbuka kujisajili (subscribe) katika tovuti hii ili uendelee kupata mafunzo mbalimbali ya kukujengea uwezo.

Dkt. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania