Utangulizi
Hii ni sura ya mwisho ya kitabu cha Kilio cha Wachungaji
Unaweza kununua kitabu hiki kwa Tsh 5,000 (elfu tano tu) pamoja na gharama za kutuma. Pia unaweza kukinunua kwa Tsh 3,000 (elfu tatu tu) kikiwa katika mfumo wa Ebook/Epub ili ujisomee kwenye simu ambapo maandishi yake ni makubwa yasiyoumiza macho.
Sura ya Sita (kwa muhtasari)
Maswali kwa ajili ya Mchungaji Kujihoji Kibinafsi
Haya maswali yanamsaidia mchungaji kuwajibika ili kama kuna
maeneo anapata mateso ambayo hayakuruhusiwa na Bwana, ayafanyie kazi.
1.
Umekuwa ushuhuda kwa ukuu wa Kristo kwa maneno yako na matendo yako? Watu
wanapokusikiliza na kutazama mwenendo na mtindo wa maisha yako wamuone Kristo
ndani yako. Uwe barua yenye ujumbe wa Yesu hata pale unapokuwa huna Biblia
mkononi (2 Kor 3:2,3).
2. Umepungukiwa
uadilifu katika masuala ya kifedha au umetamani kitu chochote ambacho si cha
kwako? Unatakiwa kuwa mwaminifu katika fedha za kanisa na uridhike na vitu
ulivyo navyo. Usijilinganishe na watumishi wa Mungu wengine. Mungu ana mpango
maalum kwa ajili ya kila mmoja wetu (1 Tim 6:6-8).
3. Umeheshimu na kuonyesha kujali katika mahusiano yako wiki
hii? Usizame katika huduma na
kusahau kuwa karibu na familia yako. Unatakiwa kujali familia yako kabla ya
kanisa. Usipojali watu wa nyumbani mwako unakuwa mbaya kuliko watu wasioamini.
Lakini pia usilione kanisa kama shirika au mradi fulani bali kama watu
wanaohitaji uhusiano wa kindugu na kirafiki (1 Tim 5:8).
4. Umetawaliwa na mwenendo usiofaa (addictive behaviour)
wiki hii iliyopita? Sio lazima mwenendo
usiofaa uwe ulevi wa pombe au sigara tu. Unaposhindwa kufanya huduma kwa sababu
ya kuangalia mpira au tamthiliya katika runinga (TV), unakuwa mlevi wa runinga.
Uwe na kiasi katika kila jambo. Hata maombi ya muda mrefu ni mazuri kwa ajili
ya upako lakini usisahau kupatana na mkeo au mumeo kabla ya kufanya hivyo kwa
ajili ya usalama wa familia (1 Kor 7:5).
5. Mtu alikuumiza? Ulimsamehe? Umeendelea kutunza hasira
dhidi ya mtu fulani? Pengine
unaendelea na huduma wakati kuna mtu husalimiani naye na hakuna juhudi zozote
unazochukua. Biblia inasema ukiwa na neno na mtu acha kutoa sadaka ukapatane
naye kwanza ndipo uje kuitoa. Jua lisichwe uchungu haujakutoka kama kweli
unajua kwamba Bwana anaweza kuja kutuchukua wakati wowote. Efe 4:26,27
6. Umemtakia mabaya mtu yeyote kwa siri? Pengine kuna mtu unatamani ungesikia amekufa au
unamuombea afe. Kama unaamini Mungu anaweza kuua, amini pia anaweza kubadilisha
na kuhuisha. Watu wengi wanaotukwaza hawafanyi hivyo kwa kukusudia bali wana
roho chafu ndani yao. Ungana na Bwana Yesu kwa kusema, ’Baba, wasamehe kwa kuwa
hawajui watendalo’.
7. Umeruhusu kutawaliwa na mawazo mabaya kuhusu mtu fulani wiki
hii? Pengine kuna mtu ambaye si mwenzi wako halali
lakini anakutesa sana katika moyo wako. Umeshindwa kumng’oa moyoni mwako. Yesu
aliyesema, Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo nami
nitawapumzisha, anaweza kutua mzigo wako. Wakati mwingine unawawazia vibaya
watu fulani kwamba wametenda dhambi wakati huna ushahidi wowote. Usisahau
kwamba ingawa unatumika, hii kazi ina mwenyewe. Mwachie Mungu mwenyewe ahukumu
watu wake aliowaumba.
8. Umefanya maombi, umesoma neno na kumsikia Mungu kama
inavyotakiwa wiki hii? Mara
nyingi unaomba na kusoma Neno wakati tu unapoandaa ujumbe badala ya kujilisha
Neno ili liwe sehemu ya maisha yako kwanza kabla ya kulipeleka kwa wengine.
Wakati mwingine unajisikia moyoni kwamba ni neema tu ya Mungu inayokuwezesha
kusimama madhabahuni kuhubiri kwa vile huna muda kabisa wa kuomba na kusoma
Neno. Unahitaji kumsikia Mungu kila wakati ili uwe na ujumbe sahihi wa
kuwaambia watu wake.
9. Umekuwa mwaminifu kabisa kwa Mungu? Unajua njia zako kwamba ungekuwa hatarini kiasi gani na
kupoteza heshima yako kama watu wangejua
mambo unayoyafanya kwa siri. Unasahau kwamba Mungu anakuona. Na baya zaidi
unapenda sana kuwanyoshea kidole wengine na kusahau madhaifu yako lukuki. Epuka
kufanya jambo lolote ambalo ungejisikia hatia kama ungeambiwa uombe kwanza
kabla ya kulifanya.
Pamoja na haya yote,
usijisikie kukata tamaa bali utambue kwamba Mungu anatazama nia yako na anataka
kukusaidia ili usije ukahubiri wengine halafu mwishowe wewe mwenyewe ukawa mtu
wa kukataliwa (1 Kor 9:27).
Bei ya kitabu katika mfumo wa karatasi ni Tsh 5,000 na mfumo
wa mtando (ebook) ni Tsh 3,000.
Soma muhtasari wa sura zote
kupitia www.lawimshana.com. Tafuta
sehemu iliyoandikwa ’search’ halafu andika WACHUNGAJI na kutafuta. Utaona
makala zote.
Dr. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, +255712-924234, Korogwe, Tanga, Tanzania