Ticker

6/recent/ticker-posts

(Maswali na Majibu) Na 4 Tufanyeje ili tuepuke njia za uzazi wa mpango zenye madhara kiroho na kiafya?


 (Maswali na Majibu) Na 4. Tufanyeje ili tuepuke njia za uzazi wa mpango zenye madhara kiroho na kiafya?

Mimi binafsi siamini mambo yafuatayo:

1. Siamini kwamba Mungu anataka tuzae watoto kwa kiwango cha kuhatarisha usalama wa mama na mtoto wake au familia nzima. Ni muhimu kujali muda wa mtoto na mtoto (spacing) na muda wa afya ya mama kurejea.

2. Siamini kwamba tunatakiwa kuzaa watoto kwa kuongozwa na mifumo ya dunia (mifumo ya dunia inaweza kukutaka kuzaa watoto wawili hata kama una uwezo wa kulea watoto sita. Lakini pia mifumo ya dunia inahamasisha utoaji wa mimba).

3. Siamini kwamba Mungu hawezi kutuwezesha kuzaa watoto katika utaratibu tunaomuomba na kutujulisha pale anapotaka kufanya tofauti na tulivyoomba. Tatizo ni kwamba tumeamua kuchagua maeneo ambayo tunamshirikisha Mungu na mengine tumeamua kuwakimbilia wanadamu. Kama Mungu alisema na wewe kuhusu wito wako, nani atakakuwa mwenzi wako wa maisha, kazi au biashara itakayokupa mafanikio, Je, anashindwa kukuongoza upate watoto katika utaratibu fulani?

4.  Siamini kwamba Mungu anataka tukose kiasi kwenye tendo la ndoa kiasi cha kujiletea madhara katika maisha yetu.

5. Siamini kwamba Mungu anataka wanandoa waishi kama wapangaji ambao hawafurahii tendo la ndoa na maisha kwa ujumla.

Matatizo ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango

1. Zipo njia za uzazi wa mpango ambazo zinafanya kazi baada ya utungisho wa mimba. Zinachozuia ni upandikizaji kwenye uterusi kwa hiyo ni sawa na kutoa mimba. Hazizuii mimba kutungwa.

2. Zipo njia za uzazi wa mpango ambazo zinazuia mimba kwa kubadili mfumo wa uumbaji wa Mungu. Mfano, kuzuia yai kutoka kwenye ovari, kubadili ukuta wa ndani wa uterasi, kuua mbegu, kuzuia mbegu zishindwe kulifikia yai nk

Kum 23:1 “Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa Bwana.” Mungu alikataa kuwahasi wanaume.

3. Zipo njia ambazo zinawafanya wanandoa washindwe kuwa na kiasi au nidhamu (tunda la roho) na kuongozwa na tamaa mbaya. Mungu hataki mume amtamani mkewe kiasi cha kutothamini utu wake bali anataka ampende mkewe. Mtu anaweza kutumia njia ambazo ni za kujifurahisha yeye mwenyewe bila kumjali mwenzake mfano, kulazimisha tendo la ndoa wakati anaumwa au yuko kwenye hedhi. 1 Wakorintho 7:5 “… mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”

4. Zipo njia ambazo zinaondoa hisia ya kike na hisia ya tendo la ndoa hivyo kuzuia kufurahia tendo la ndoa kama Mungu alivyokusudia. Matokeo yake wanandoa wananyimana tendo la ndoa na kusababisha msongo, chuki, na hata kufungua mlango wa zinaa. Tendo la ndoa linawaunganisha wanandoa wahitajiane na kupendana.

Kut 21:10 “Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia.” (haki ya ndoa)

TUFANYEJE ili tuepuke njia zenye madhara kiroho na kiafya na wakati huohuo tuwe na mpangilio mzuri wa watoto?

1. Tuongozwe na Roho Mtakatifu katika mambo yote ikiwa ni pamoja na tendo la ndoa. Wanandoa wengi wanaombea chakula mezani lakini hawaombei tendo la ndoa. Matokeo yake shetani anajihudhurisha. Yohana 16:24 “Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.”

2. Tusitawaliwe na tamaa mbaya (lust). Msukumo wa tendo la ndoa usitokane na pepo la tamaa mbaya bali upendo wa Mungu kwa hisia alizoweka Mungu katika mwili (sexual desire). Mtu mwenye tamaa ya mwili ya kawaida (ashiki) akioa au kuolewa atatulia na kama ni kijana ataweza kusubiri. Lakini kama ana tamaa mbaya (lust) hataweza kutulia kabla ya ndoa wala akiwa ndani ya ndoa. Mwenye tamaa mbaya hataweza kujizuia siku ambazo mimba inaweza kushika. 1 Wathesalonike 4:5 “si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.”

3. Tuwe na tunda la roho (kiasi au uwezo wa kujitawala). Mke sio chombo cha kujifurahisha wakati wote. Ndiyo maana Neno linasema kila mmoja apate haki yake ya ndoa (conjugal rights). Hivyo hakuna mwenye haki ya kumlazimisha mwenzake hata kama ni wanandoa. Wagalatia 5:22,23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” 1 Wathesalonike 4:4 “kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima.” Mungu ametupa uwezo wa kujizuia. Nini kinamfanya mzinzi aweze kujizuia kumbaka mtu hadharani mpaka usiku? Angeamua kuacha kabisa tabia hiyo angeweza pia.

4. Tuzielewe kwa kina njia za uzazi wa mpango za asili na kuzitumia. Njia hizi hazibadili mpangilio wa homoni au vichocheo kwenye mwili. Zinafanya kazi ili mradi wanandoa wawe wafuatiliaji kila siku na kutawala hisia zao (nidhamu).

Mifano ya njia za asili ni kuhesabu siku kwa kutumia kalenda, kupima joto la mwili kila asubuhi, kutambua kiwango cha utelezi wa ute, na kunyonyesha peke yake kwa miezi sita au hadi hedhi ya kwanza.

5. Tuwe tayari pale matokeo yanapotofautiana na mpango wetu. Watoto pia ni zawadi kutoka kwa Mungu. Zab 127:3 “Tazama, wana ndio urithi wa Bwana, Uzao wa tumbo ni thawabu.” Kutoa mimba ni dhambi ambayo ina hukumu kubwa. Tusikose imani kiasi hicho wala tusione aibu kwa watu kiasi cha kuamua kujipeleka kuzimu kwa kutoa mimba.

Dr. Lawi Mshana, 0712-924234, Tanzania