Ticker

6/recent/ticker-posts

JE NI SAWA KWA WACHA MUNGU KUSHEREHEKEA MWAKA MPYA TAREHE 1 JANUARI?


 JE NI SAWA KWA WACHA MUNGU KUSHEREHEKEA MWAKA MPYA TAREHE 1 JANUARI?

Ni jambo jema mtu kuadhimisha siku muhimu katika safari ya maisha yake. Kwa mfano, Mungu alipowakomboa Waisraeli kutoka Misri kwenda Kanaani, aliwaambia siku hiyo iwe ukumbusho na mwanzo mpya wa maisha yao. Kwa hiyo Pasaka ilikuwa ni mwaka mpya kwao.

Kutoka 12:2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu.”

Hesabu 9:2 “Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa.”

Bwana Yesu naye alipofanyika Pasaka wetu, akatutaka sikukuu yetu kama Wakristo iwe MEZA YA BWANA kama ilivyokuwa PASAKA kwa Waisraeli.

Usisahau kwamba Pasaka sio siku bali ni Kristo. 1 Wakorintho 5:7 “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo.”

Kristo anaanzisha sikukuu kwa ajili ya Kanisa (Wakristo). Luka 22:19 “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

Hata sisi leo tuna matukio mengi muhimu kukumbukwa kwa vile yana maana kubwa kiroho. Mfano, siku ya kuokoka, siku ya kupanda kanisa eneo fulani nk.

Kwanini tumefanya mambo haya kwa muda mrefu bila kuhoji?

1. Sisi sio waungwana kama watu wa Beroya – hatuchunguzi maandiko na kuyahusianisha na mahubiri tunayosikia. Tunawaamini wahubiri wetu kuliko Maandiko Matakatifu. Mdo 17:11 “Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”

2. Tunafuata mapokeo ya kidini badala ya Neno la Mungu

Marko 7:8 “Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu.”

Wakolosai 2:8 “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”

3. Hatuogopi hukumu ya Mungu kwa kuongeza au kupunguza maagizo ya Mungu

Ufu 22:18,19 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”

Je sherehe zetu zinaendana na vigezo vya sikukuu za kipindi cha Biblia?

Ukisoma Law 23:1-44 utaona ‘Sikukuu za Bwana’ ambazo Mungu anazitambua kwa ajili ya Waisraeli kama vile sabato, Pasaka, mikate isiyotiwa chachu, malimbuko, mavuno, baragumu, upatanisho na vibanda.

Maswali ya kujiuliza:

1. Kwa nini baadhi ya sikukuu hatuendelei nazo ingawa zimetajwa kwenye Biblia? Mfano, baragumu, mikate isiyotiwa chachu nk

2. Kwa nini hatusherehekei kama walivyofanya wenzetu? Walifanya kwa ajili ya Mungu na sio kwa ajili yao wenyewe? Leo tunampa Mungu nini katika sikukuu zetu? Sio kwamba tunajipongeza wenyewe kwa vyakula, mavazi, matembezi na anasa na kumsahau Mungu?

Ufafanuzi kidogo:

1. Sikukuu hizi zilikuwa kwa ajili ya Waisraeli na sio Wakristo. Musa aliwaongoza Waisraeli kutoka Misri kwenda Kanaani na Kristo analiongoza Kanisa kutoka duniani kwenda Mbinguni.

2. Kristo alikuja kutimiza hizi sikukuu kwa jinsi ya rohoni. Mfano, Pasaka ameitimiza kwa Yeye Mwenyewe kuwa Pasaka wetu, alitimiza sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu kwa ushindi wa dhambi na mwili wake kutoona uharibifu, malimbuko kwa Yeye Mwenyewe kuwa limbuko (wa kwanza kufufuka), mavuno kwa kushuka kwa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste (siku ya kuzaliwa kwa Kanisa) na sabato kwa kuwa Bwana wa sabato.

3. Sikukuu kadhaa bado Bwana Yesu hajazikamilisha

i. Sikukuu ya Baragumu – ataitimiza siku atakapokuja kulinyakua Kanisa lake ambapo parapanda italia.

ii. Sikukuu ya Upatanisho – ataitimiza kwa kuwapa nafasi watu kupatana na Mungu kwa mateso ya dhiki kuu

iii. Sikukuu ya vibanda – ataitimiza kwa kukaa na watu wake waliomuamini na kumuishia milele na milele. Ameenda kuandaa makao kwa ajili ya watu wake.

4. Kwanini tunaabudu Jumapili badala Jumamosi

Katika maandiko matakatifu, Jumamosi ni siku ya saba (sabato) na Jumapili ni siku ya kwanza ya juma.

i. Sabato ya Jumamosi ilikuwa ya muhimu kabla ya Agano Jipya (kabla ya dhambi kuingia duniani hadi kuja kwa Bwana Yesu). Bwana Yesu aliwaonya viongozi wa kipindi chake kwamba wamshike Yeye (Bwana wa Sabato) kuliko siku (sabato). Kumbuka mpango wa Mungu kabla ya dhambi kuingia duniani ulikuwa kwamba mwanadamu aishi kwa raha duniani MAISHA YAKE YOTE. Hatungekufa na hatungeenda Mbinguni. Dhambi ilitufanya tuhukumiwe kwenda motoni milele. Yesu akafanyika sadaka (kafara) kwa ajili yetu hivyo tukapewa fursa ya kwenda Mbinguni. Bwana Yesu akaenda kutuandalia makao kwa vile hayakuwepo kwa ajili yetu.

ii. Siku ya Jumapili ilikuwa muhimu baada ya Yesu kushinda kifo na mauti (KUFUFUKA KATIK WAFU). Kama Yesu hangefufuka, imani yetu ingekuwa ni bure. 1 Wakorintho 15:14 “tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure” Kwa hiyo sabato ya Jumamosi haingekuwa na maana kama tunamilikiwa na shetani. Ndiyo sababu mitume walianza kukutana siku ya kwanza ya juma (Jumapili) na kuwaachia siku ya Jumamosi watu wa dini ya Kiyahudi. Ni kweli Jumapili ni Sun-day (siku ya mungu jua) lakini jina hilo limekuja baadaye sana. Kipindi cha Biblia iliitwa SIKU YA KWANZA YA JUMA na huo ndio msingi wetu. 1 Wakorintho 16:2 Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja.”

Tuwe waangalifu kuzitambua sherehe ambazo zina uhusiano na miungu au sanamu badala ya Bwana Yesu kwa vile tumeonywa katika amri ya kwanza na ya pili.

Kut 20:3,4 “3 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

Tuzingatie maadili mazuri ya sherehe tunazoshiriki na kuchangia.

Yohana 2:1,2 “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.”

1 Petro 4:3 “Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali.”

NB: Soma makala nilizoandika humu kuhusu Krismasi na Pasaka

Ufafanuzi kuhusu Mwaka mpya

Kibiblia Pasaka ilikuwa ndiyo mwaka mpya kwa Israeli.

Kutoka 12:2 “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu.”

Hesabu 9:2 “Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa.”

Kwa kalenda yetu mwanzo huo wa mwaka ni mwezi gani?

Law 23: 5 “Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana.”

Mwezi wa kwanza (Nisani) siku ya 14 – (kati ya Machi na Aprili). Mungu aliagiza pasaka iwe kwa ajili ya ISRAELI PEKE YAO lakini mgeni na mwajiriwa asile. Haikusherehekewa kama ilivyo leo ambapo hata wanaomtukana Yesu wanasherehekea.

Kwa nini mwaka mpya ukawa Januari 1

Historia fupi ya sherehe za mwaka mpya na asili yake

Desturi ya kusherekea mwaka mpya hasa ilianzia huko Babeli Mesopotamia (kwa sasa ni Iraki) mnamo mwaka 2000 KK.

Kalenda ya mwanzo ya dola la Rumi iliweka Machi 1 kama siku ya mwaka mpya, kwa sababu katika ufalme wa Rumi walikuwa na Kalenda yenye miezi 10 tu, ikianzia Machi hadi Disemba, hivyo mwaka mpya ulikuwa katika mwezi Machi ambao ulikuwa ni mwezi wa kwanza. Mwezi Machi unathibitishwa pia kwa majina ya miezi mingine iliyofuata kuwa ulikuwa ni mwezi wa kwanza kwa sababu mwezi Septemba hadi Disemba katika kilatini ni majina ya “namba”. Kwa mfano; (septem kwa kilatini ni “saba,” octo ni “nane,” novem ni “tisa,” na decem ni “kumi.”); hivyo Disemba ilikuwa ni mwezi wa 10 na Machi ilikuwa mwezi wa kwanza, Kwa hiyo kalenda ya kwanza ya Rumi ilikuwa na jumla miezi 10.

Je “Januari” iliingiliaje katika miezi hiyo na kuwa mwezi wa kwanza?

Kwa mara ya kwanza mwaka mpya ulisherekewa Januari 1 huko Rumi mnamo mwaka 153 KK. Hata hivyo, mwezi Januari awali haukuwepo mpaka mwaka 700 KK, ambapo mfalme wa pili wa Rumi, Numa Pontilius, aliiongeza mwezi wa Januari na wa Februari katika Kalenda ya Rumi. Kwa sababu hiyo mwaka mpya ulihamishwa kutoka Machi 1 na kuwa Januari 1, kwa maana Januari ndio ulikuwa mwanzo wa mwaka katika serikali. Hata hivyo Januari 1 haikujulikana katika maeneo mengi kwa hiyo wakati mwingine Machi 1 iliendelea kuadhimishwa kama mwaka mpya.

Sababu kuu ya mfalme wa pili wa dola la Rumi, Numa Pontilius, kuiweka Januari 1 kama siku ya mwaka mpya; inaaminika kuwa jina Januari lilitokana na jina la mungu wa Rumi mwenye vichwa viwili aliyeitwa “Janus”, mungu huyo alikuwa ni mungu wa “milango” na “mianzo” (beginnings) n.k. Hivyo mfalme Numa Pontilius aliona ni vema kuiweka Januari 1 kama siku ya sherehe ya mwaka mpya na ibada kwa ajili ya mungu Janus.

Kwa kuwa mungu Janus alikuwa mungu wa milango na mianzo, hivyo waliamini kwamba kwa kumfanyia ibada za sherehe mwanzoni mwa mwaka; angewafungulia milango ya baraka kwa mwaka huo wote, na angeanzisha mwaka wenye heri. Hivyo watu walitakiana “heri ya mwaka mpya” (happy new year) wakiamini kwamba mungu wao wanayempa ibada siku hiyo angewajalia mwaka wenye heri. Hii ni ibada ya kipagani na haipaswi Mkristo yeyote mwaminifu akamatwe katika mtego huu wa kusherekea mwaka mpya tena katika siku ileile ya Januari 1.

Katika mwaka 567 BK Baraza la Tours liliivunja Januar1 1 kama siku ya mwanzo wa mwaka. Katika nyakati mbalimbali na maeneo mbalimbali pote katika Ukristo wa Ulaya, siku ya mwaka mpya iliadhimishwa Disemba 25, na kuzaliwa kwa Yesu kuliadhimishwa Machi 1. Miongoni mwa wapagani wa karne ya 7 wa Flanders na Netherlands, ilikuwa ni desturi kupeana zawadi katika siku ya mwaka mpya.” -(Wikipedia the free Encyclopedia, “New Year’s Day”)

Januari 1 ilirejeshwa upya na kanisa Katoliki.

Katika mwaka 1582 utengenezwaji wa kalenda ya Papa Gregorio (Gregory XIII), uliirudisha Januari 1 kama siku ya mwaka mpya. Baadaye mataifa mengi na koloni nyingi zilianza kutumia kalenda hiyo ya Gregorio. Hadi hivi sasa ni nchi chache tu ambazo husherekea mwaka mpya katika siku tofauti na Januari 1, lakini nchi zote zinazotumia kalenda ya Gregorio husherekea mwaka mpya Januari 1 siku ambayo inaaminika ilikuwa maalumu kwa ajili ya mungu Janus.

Maovu gani yanafanyika siku za mwaka mpya

Miongoni mwa mambo yanayofanyika katika mikusanyiko ya mkesha wa mwaka mpya: muziki wa kidunia hupigwa, pombe hunywewa, wanaume na wanawake wanavaa mavazi yasiyo na heshima, fujo hufanyika wanapochoma fataki usiku wa manane nk.

Kalenda ya saa 6:00 usiku na kuisha saa 6:00 usiku ni kinyume na Kalenda ya Biblia (Mwanzo 1:5).

Tunaonywa tusifanane na dunia

Yer 10:2-4 “Bwana asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka. Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike.

Mataifa (heathen) ni watu wanaoabudu vitu vya asili (jua, mwezi, nyota, miti nk) au sanamu zilizotengenezwa na wanadamu au kitu chochote ambacho ni tofauti na Mungu mmoja wa kweli. Watu hawa wanaitwa WAPAGANI.

Upagani ni jambo zito kiasi gani kwa Mungu?

1. Mungu hataki matendo yetu yafanane na ya wapagani wanaotuzunguka

Law 18:3,4 “ 3 Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao. 4 Mtazifanya hukumu zangu, nanyi mtazishika amri zangu, ili mwenende katika hizo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

2. Mungu anawaadhibu watu ambao wanajitia unajisi na kufanya machukizo

Law 18:24-30 “ 24 Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; 25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa. 26 Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu; 27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;) 28 ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu. 29 Kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao. 30 Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

3. Mungu anawahukumu watu wake wanapofanya agano na mataifa

Kum 7:1-5,16 “1 Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; 2 wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; 3 binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. 4 Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi. 5 Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. 16 Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa Bwana, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo.

Zab 106:34-42 “ 34 Hawakuwaharibu watu wa nchi Kama Bwana alivyowaambia; 35 Bali walijichanganya na mataifa, Wakajifunza matendo yao. 36 Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao. 37 Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. 38 Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu. 39 Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao. 40 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake. 41 Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala. 42 Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao.

Danieli alitabiri kwamba shetani atabadilisha majira na sheria akiwatumia mawakala wake.

Da 7:25 “Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.

Dr. Lawi mshana, +255712924234, Tanzania