Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini inakuwa vigumu leo kupata mke/mume sahihi (sehemu ya kwanza)


KWA NINI INAKUWA VIGUMU LEO KUPATA MKE/MUME SAHIHI (SEHEMU YA KWANZA) 

Vijana wa kike na wa kiume wanakuwa na wakati mgumu sana kipindi hiki katika kupata mwenzi sahihi wa maisha. Wengine wanaomba Mungu awape mchumba badala ya mwenzi wa maisha. Matokeo yake wanachumbiana kila kukicha bila kufikia ndoa takatifu. Uchumba ni mchakato tu kuelekea kwenye ndoa kamili. Mungu hajaahidi popote kwamba atakupatia mchumba mwema bali mume au mke mwema.

Nitatumia ndoa ya Isaka na Rebeka ilivyokuwa tangu uchumba hadi ndoa. Hata hivyo ninapozungumzia MWENZI SAHIHI sina maana ya MWENZI MKAMILIFU. Bado mwanadamu ana mapungufu yake ambayo yanaweza kutumiwa kama fursa za kuhitajiana. Mungu anaunganisha watu ili wakamilishane (complement each other).

Nimepata msukumo wa kuisoma Mwanzo 24 kiufunuo ili kukupa kanuni za msingi za kukusaidia. Sio lazima zimfae kila mtu. Bado wapo wenye maisha mazuri bila kanuni hizi zote. Huu ni mwongozo tu kwa wacha Mungu (wanaomhofu Mungu kuliko kufuata tamaa zao za mwili na wanaojua kuna siku tutatoa hesabu ya matendo yetu mbele za Mungu). 

NB: HII NI SEHEMU YA KWANZA. SOMO HILI LITAENDELEA SEHEMU YA PILI NA YA TATU.

Sababu za ugumu wa kupata mwenzi sahihi:

1. Wazazi kuona ndoa ni mtaji wa kiuchumi na vijana kutojiandaa mapema

Mst  1: “Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote.”

Wakati Ibrahimu anahitaji mwanae apate mke sahihi alikuwa ameshabarikiwa kiroho na kiuchumi. Hapakuhitajika mkaza mwana kwa sababu za kiuchumi bali za kimahusiano. Wapo wazazi wamewatumbukiza watoto kwenye matatizo kwa sababu tu ya njaa au kuthamini pesa kuliko upendo na mahusiano. Wapo wanaotaja mahari kubwa sana ambayo inapelekea vijana wasiomjua Mungu kuamua kutoroshana au uchumba kuvunjika.  Kuna wazazi walimkatalia binti yao kuolewa na kijana ambaye hana pesa. Wakampangia kuolewa na kijana mwenye pesa. Alipoolewa ikawa saa ya chakula mume anamwambia yeye ale chakula akiwa ameketi chini sakafuni. Mume akawa anamwambia, Unajua sofa wewe? Kaa chini! 

Lakini pia wapo vijana wengi ambao wametanguliza zaidi uchumi kuliko mahusiano na matokeo yake wanapishana na mpango wa Mungu. Hata hivyo mtu ambaye hajajiandaa kimaisha kiasi cha kuweza kukaa na mkewe peke yao hapaswi kuoa kwa vile Biblia imeagiza mtu amuache baba yake na mama yake. Mwanzo 2:24 “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.” Haikubaliki kuoa na kuishi na wazazi kwa vile hamtaweza kuwa huru kama familia. Wazazi wataendelea kukuona ni mtoto na kusahau kwamba umeoa. Hivyo wanaweza kukutuma bila kutegemea ukajadiliane kwanza na mkeo. Mnatakiwa muwe na kwenu ndipo muwachukue wazazi na kuwalea inapobidi.

Unapokuwa hujajiandaa kwa mahitaji ya msingi ni rahisi kuuza zawadi mtakazopewa siku ya arusi yenu. Mungu alihakikisha anampa Adamu BUSTANI kabla ya kumpa MKE. Mwanzo 2:15 “Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.”  Mwa 2:18 “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.” Tatizo vijana wengi wanaandaa zaidi arusi na kusahau maisha. Wanawaza uchumba hadi siku ya arusi badala ya kuwaza zaidi kwamba maisha yatakuwaje baada ya ndoa kufungwa. Badala ya kufanya arusi za kifahari afadhali tupunguze gharama na kuwanunulia mahindi ya kuanzia maisha ili wasiuze zawadi zao. Sio lazima uwe tajiri ndipo uoe lakini lazima uwe na vitu vya msingi kv kipato fulani, chakula, chumba, kitanda, godoro, viti au vigoda nk. Vinginevyo jipange kwanza upate bustani ndipo uoe. 

2. Kutoshirikisha wazazi kabla ya kuanzisha mahusiano

 Mst 2: “Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu.”

Vijana wengi wanaotaka mwenzi wa maisha, hawatafuti ushauri na baraka za wazazi kabla ya kumuona wanayempenda. Wanasubiri mpaka wamuone ndipo wanawaona wazazi ili kuwashawishi wamkubali. Mimi nilichunga kanisa kwa miaka kumi nikiwa sijaoa lakini nilipotaka kuoa nikawaona wazazi wangu na kuwaomba nipige magoti waniombee. Na kweli wakaniwekea mikono na kuniombea. Niliwaomba kwamba waniombee nipate mke ambaye atawapenda wao pia badala ya kunijali mimi peke yangu. Na ndivyo alivyofanya Mungu. Mke wangu yuko karibu na ndugu wa upande wetu kuliko mimi mwenyewe. Yeye ndiye ananikumbusha tusaidie ndugu zangu. Pia Mungu ametenda hivyohivyo kwa upande wao. Baba mkwe yuko karibu na mimi kuliko mke wangu ambaye ni mwanae wa kumzaa. 

Ukisubiri wazazi wakuachilie siku ya arusi wakati hukuwashirikisha kabla ya kupata mke au mume, kuna baraka utazikosa. Hamuwezi kufanikiwa kwa kuishi kama kisiwa bila mahusiano na ndugu. Kuna changamoto za maisha ambazo watu wengine wanaweza kukukimbia lakini ndugu wakakabiliana nazo hata kama wako mbali kwa vile damu ni nzito. Wapendwa makanisani wana sehemu yao lakini hawawezi kuchukua nafasi ya ndugu wa damu. Ni mara chache sana mtu atalazwa hospitalini halafu wapendwa wakabiliane na gharama za dawa. Mara nyingi watamuombea na kumalizia na UBARIKIWE NA BWANA au MUNGU AKUTIE NGUVU bila kutia mkono mfukoni na kutoa chochote.

3.  Kutojua mwenzi wako anatakiwa kutoka kwenye kundi la aina gani

Mst 3,4 “nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao. bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.” 

Mungu alimbariki Ibrahimu katika nchi ya Wakanani lakini alikumbuka agano la Mungu kwamba alikuja Kanani kuinuliwa kiuchumi na sio kuoana na Wakanaani. Ezra 9:12 “Basi, msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana wenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele.” Kuna vigezo vya jumla na vigezo binafsi. Vigezo vya kuzingatiwa na kila muumini wa kweli ni lazima aoe au aolewe na muumini wa kweli. Hakuna ndoa inayoweza kubadili tabia ya mtu. 2 Wakorintho 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?” Kujidanganya kwamba unaoa mtu au unaolewa na mtu fulani halafu utamuombea abadilike ni kujidanganya na kujitia jela mwenyewe. Lakini pia kabla ya kumuona msichana au mvulana yeyote unatakiwa kuwa na mwongozo wa nani atafaa kuziba pengo ulilo nalo na wewe kuziba la kwake. Mimi sikuwa na tabia ya kuwapigia wasichana mahesabu kwa vile nilipata ufunuo wa kuandaa mwongozo niliouita MISS RIGHT. Mwongozo huo haukuwa wa kificho bali niliwapa waombaji waniombee. Pia haukuwa wa kumlazimisha Mungu bali ilikuwa ni mapendekezo tu na nilikuwa tayari kwa lolote. Nilijua kwamba kuna sifa zingine zinaweza kuonekana baada ya kuoa na sio kabla. Ndoa ni chuo kisicho na mahafali (graduation). Dada mmoja aliomba Mungu ampe mume ambaye ni mchungaji na ambaye hana kitambi. Kwa hiyo kila alipoona wanafunzi wa chuo cha Biblia wametembelea kanisani akawa anawapigia mahesabu. Kilichotokea akachumbiwa na mtu ambaye ni mfanyakazi na ana kitambi kikubwa. Akajisikia moyoni kwamba Mungu anataka aolewe naye lakini akakemea sana kwa vile hana vigezo alivyotaka. Baadaye akakubali kuolewa na huyo ndugu. Kilichotokea baadaye Mungu akamuita huyo mume wake kuwa mchungaji na kitambi kikafyekwa na majukumu ya utumishi. Kwa hiyo sifa zingine zinaweza kukamilika baada ya kuoa au kuolewa. 

Hata hivyo ujumbe huu hauwezi kutekelezeka kama upo kwenye kanisa ambalo uongozi ndio unaopanga nani amuoe nani au aolewe na nani au kanisa ambalo lazima mwenzi atoke humohumo kanisani. Sidhani lipo kanisa la mahali (local church) ambalo lina uwiano mzuri kati ya wavulana na wasichana waliofikia umri na utayari wa ndoa. Labda maombi ya kufunga yafanyike ili wavulana waletwe kuziba pengo lililopo. Vinginevyo baadhi ya waumini watakuwa na majuto na uchungu usio na sababu. La msingi vigezo vya kibiblia vizingatiwe. 

4. Kushindwa kusimamia maono

Mst 5-9 “Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko.  Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo.” 

Ibrahimu aliweka wazi kwamba anataka Isaka aoe mtu kutokea wapi lakini pia aliweka masharti kwamba lazima awe tayari kuja Kanani ambapo baraka zao zipo. Kwa lugha nyepesi alimwambia mtumishi wake kwamba akikataa kufuatana na wewe sio chaguo la Mungu kwa ajili ya mwanangu. Kumpenda mtu kusikupofushe macho ukapuuzia mambo ya msingi. Usidanganywe kwamba tofauti zenu zitaisha kirahisi sana. Kama mna tofauti kubwa za kidini zinaweza kuleta ufa mkubwa sana kwenu wenyewe na kwa watoto wenu. Misimamo ya kidini mara nyingi ina mizizi ya ndani sana katika moyo wa mtu. Labda kama mmoja yuko tayari kujiunga na dhehebu la mwenzake kwa sababu za kiroho na sio za kuolewa au kuoa peke yake. Kuna dada fulani alichumbiwa na kijana asiyeamini (mkristo wa dini), akamwambia mimi siwezi kuolewa na mtu ambaye hajaokoka. Yule kaka akaamua KUMUOKOKEA. Akajiunga na kanisa lao na akawa mwimbaji wa kwaya. Baadaye akakubaliwa kwamba ameshaiva kiroho na ndoa ikafungwa. Waliporudi nyumbani yule kaka akavuta kreti la bia chini ya kitanda akamwambi sasa tunywe bia. Dada akagundua kwamba yule kaka HAKUOKOKA bali ALIMUOKOKEA. Hata hivyo kuna kijana alifanya kama huyu lakini yeye akapata fundisho. Ndoa ilipofungwa walipofika nyumbani. Alipofungua bia akidhani amemuangusha kiroho akashangaa bibiarusi akisema hata mimi napenda sana bia nilikuwa nawaza sijui itakuwaje kama hunywi. Ikawa wameoana wasioamini ndani ya kanisa la waaminio. Kama una maono ya kupata mtu wa aina fulani simamia maono yako na kuwa na subira. Unaweza kuchelewa kukutana naye kwa vile bado Mungu anamuandaa ili akufae au bado Mungu anakuandaa wewe usije ukamtesa.   

5. Kutoenda mahali sahihi ambapo mwenzi wa aina unayohitaji atapatikana

Mst 10 “Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori.”

Haikuwa rahisi kwenda kwa usafiri wa ngamia kutoka Kanani hadi Mesopotamia umbali wa kati ya kilomita 600 hadi 1000. Inawezekana Ibrahimu hakutaka Isaka aende mwenyewe kwa vile angeweza kujaribiwa kubakia hukohuko. Kulikuwa na hatari nyingi za baridi, kukosa maji njiani na kuvamiwa na majambazi. Ukizingatia alikuwa na mali nyingi  za thamani. Ni kweli Mungu hangeshindwa kufanya muujiza wa kumleta Rebeka katika nchi ya Kanani. Lakini hatuwezi kufuata au kusubiri miujiza bali miujiza inatufuata sisi pale Mungu anapotaka kufanya hivyo. Kama unataka kuolewa na mtu wa aina fulani lazima ujiulize watu kama yeye wanapatikana wapi. Huwezi kupata mkristo mzuri aliyeokoka kwenye kumbi za disko wala msomi wa chuokikuu katika mazingira yasiyo na kazi za watu wa aina hiyo. Mimi nilioa mke anayeishi umbali wa km zaidi ya 2000 kutoka Korogwe nilipo. Mungu alinikutanisha naye nikiwa umbali wa km kama 1300 kutoka Korogwe nilipo na yeye akiwa umbali wa km kama 1500 kutoka nyumani kwao. Nilikwenda kufundisha semina ya Neno la Mungu na yeye alikuja kusalimia ndugu yake. Tena ilikuwa arudi nyumani kwao kabla sijafika kuanza semina ikatokea tu sababu iliyomfanya aongeze wiki moja nyingine. Hata hivyo huwezi kuzunguka tu miji au vijiji fulani kutafuta mwenzi wa maisha. Unachotakiwa ni kushiriki matukio muhimu ya kukukutanisha na watu kv kambi za maombi, semina, makongamano ambayo washiriki wake ni wa aina mbalimbali nk. Isaka hangempata Rebeka kwa kuomba tu na kubakia Kanani. Gharama ilitumika kumpata Rebeka.

 …………………………………………………somo hili litaendelea (Na 6-10 na 11-16)

Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Korogwe, Tanga, Tanzania