Ticker

6/recent/ticker-posts

UNAJUA KWANINI BAADHI YA VIONGOZI WA IMANI WANA MAUMIVU KATIKA MAISHA YAO? (Kilio cha Wachungaji, Sura ya 2)


 UNAJUA KWANINI BAADHI YA VIONGOZI WA IMANI WANA MAUMIVU KATIKA MAISHA YAO? (Kilio cha Wachungaji, Sura ya 2)

Utangulizi

Pengine unajisemea moyoni kwamba ujumbe huu haukuhusu kwa vile wewe sio mchungaji. Napenda ujue kwamba mtumishi wa Mungu akihuzunika kwa sababu yako unakaribisha laana katika maisha yako. Waebrania 13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.”

Ni ukweli usiopingika kwamba wakosoaji wakuu na wanaonyoshea kidole madhaifu ya viongozi wao wa imani HAWAJAWAHI KUWAOMBEA WALA KUTAFUTA NJIA YOYOTE YA KUWASAIDIA. Wanawachukulia wakati wote kwamba wanawakosea kwa makusudi.

Nitaeleza sura za kitabu hatua kwa hatua kwa kifupi. Lakini unaweza kusoma kwa kina zaidi kwa kununua kitabu cha karatasi za kawaida (hardcopy) au kitabupepe (ebook).

Sura ya Pili (kwa muhtasari)

Sababu Kuu za Maumivu ya Wachungaji

Kuingia katika utumishi bila wito maalum, mifumo mibovu na kandamizi ya madhehebu na makanisa wanayoyachunga, kuandaa kanisa kiroho na kusahau kuliandaa kijamii na kiuchumi, kutosheka na maisha ya chini ya kiwango, waumini kutotambua maumivu ya familia za wachungaji wao na kupata upinzani usiokoma katika huduma.

Yapo mambo mengi yanayosababisha maumivu kwa wachungaji. Nitazungumzia sababu kadhaa nilizogundua kwamba zinachangia zaidi maumivu hayo:

1. Kuingia katika utumishi bila wito maalum:.

Katika utumishi kuna makundi makuu matatu.

·       Kundi la kwanza ni la watumishi ambao wametumwa na watu. Watumishi hawa wameingia katika utumishi kwa msukumo wa watu wengine bila wao wenyewe kupata uthibitisho wowote mioyoni mwao. Wanatumika kwa hofu ya kibinadamu bila hofu yoyote ya Mungu. Hivyo wanachotafuta ni kulipendeza dhehebu hata kama jambo wanalolifanya liko kinyume na maagizo ya Mungu.

·       Kundi la pili ni la watumishi waliojituma wenyewe. Watumishi hawa wameingia katika huduma kwa kujitolea wenyewe kwa kuona hitaji bila kusikia msukumo wowote wa Kimungu mioyoni mwao. Watumishi hawa wameamua kuingia katika huduma kwa vile wanawahurumia watu au kwa vile wana muda wa kufanya huduma hiyo. Ni rahisi sana watumishi wa aina hii kuchoka mapema kwa vile wanachunga kanisa kwa kutumia karama ya masaidiano badala ya huduma ya kichungaji. 

·       Kundi la tatu ni la watumishi waliotumwa na Mungu. Watumishi hawa wamesikia wito mioyoni mwao wenyewe na kupata uthibitisho kwa njia kadhaa kama vile kupitia katika Neno la Mungu, watu wengine, maono na unabii.

Kama mtumishi wa Mungu atagundua ametumwa wapi, wakati gani na kwa kundi gani lazima huduma hiyo itafanikiwa. Hata hivyo, mafanikio ya huduma hayapimwi kwa vipimo vya kibinadamu bali kwa viwango Mungu alivyomuwekea mtumishi wake. Ndiyo maana Mtume Paulo alisema mwendo nimeumaliza wakati katika kipindi chake hakufika Tanzania. Alijua kipimo alichopimiwa na Mungu.

Huduma sio cheo au wadhifa bali ni moyo wa Mungu kwa ajili ya kuhudumia watu wake. Mtu anapopewa huduma ya kitume anapewa moyo wa tofauti na mtu mwenye huduma ya kichungaji. Kama mtu hajui wito wake maalum anaweza kutumika katika wito ambao Mungu hakumpa na hivyo kukosa baraka zilizokuwa zimeandaliwa na Mungu kwa ajili yake. Hata hivyo, wapo watumishi wengine ambao Mungu amewapa huduma zaidi ya moja.  Ni wajibu wa mtumishi wa aina hiyo kutambua huduma iliyo kubwa zaidi ndani yake ili atumike zaidi katika huduma hiyo ndipo atapata upenyo mkubwa zaidi. 

 2. Mifumo mibovu na kandamizi ya madhehebu na makanisa wanayoyachunga.

Yapo madhehebu ambayo hayana mfumo mzuri wa kujali maisha ya watumishi wake. Viongozi wake wakuu wanajali tu makanisa yakue kiidadi ili mapato ya dhehebu yaongezeke bila kupitia upya kiwango cha maisha na posho za watumishi wake. Hata huo ukuaji wenyewe haufanyiwi tathmini. Ukifuatilia sana sio ‘ukuaji wa kanisa’ bali ni ‘ukuaji wa dhehebu’ kwa vile wengi wanaojiunga walishaokoka huko walikotoka. Na kibaya zaidi hawakuletwa na Bwana ili wapate malezi bali ni ushawishi wa makusudi uliowafanya wahamie kanisa hilo jipya. Na wengi wao tangu wahamie hadi leo hawajapokea yale waliyoahidiwa kwamba watayapata. Tunapolazimika kuhamia kanisa jingine tuwe na sababu za msingi mioyoni mwetu. Vinginevyo, tushirikiane tu na huduma zingine na kurudi kwetu kwa vile kila kanisa la mahali (local church) ni kiungo tu katika mwili wa Kristo (universal church) hivyo haliwezi kumtosheleza mtu kwa kila kitu.

Makanisa pia yana mikakati ya mamilioni ya kuendeleza majengo na kununua vyombo vya muziki wakati mahitaji ya familia za wachungaji hayashughulikiwi. Baadhi ya viongozi wakuu wanaona kama mchungaji kulala njaa ndio wito wake. Hivyo, fedha nyingi zinapelekwa ngazi za juu za dhehebu na kumuacha mchungaji bila kitu. Nimeshuhudia washirika kadhaa katika semina ninazofundisha wakisema wameamua kukiuka utaratibu kandamizi wa madhehebu yao.

Hutashangaa pia kuona mkutano wa injili ukiandaliwa kwa mamilioni ya fedha ambapo wahubiri na waimbaji wakija wanalala vyumba vya watoto wa mchungaji vyenye vyandarua.  Watoto hao wanalazimika kuwapisha wageni na kulala sebuleni ambapo wanaumwa na mbu au kulala kwa shida usiku kucha.

Ni makanisa machache yanayojali kuwawekea akiba ya uzeeni wachungaji wake. Makanisa mengine yanakata posho za wachungaji wake lakini fedha hizo hazipelekwi katika mfuko wa hifadhi ya jamii bali zinaliwa na wajanja.

3. Kuandaa kanisa kiroho na kusahau kuliandaa kijamii na kiuchumi.

Yapo makanisa ambayo yana mikakati mizuri sana ya maisha ya kiroho ya washirika wake. Hata hivyo, mikakati yao haina matokeo mazuri kwa vile haiwaandai waumini katika maeneo mengine ya maisha. Huduma ya Yesu akitembea duniani iligusa maeneo yote ya maisha ya mwanadamu (holistic ministry). Hatuna budi na sisi pia kujitahidi kugusa maeneo yote ya maisha ya mwanadamu, yaani, mwili, nafsi na roho.

Hatukutumwa kuhubiri mikutano ya Injili peke yake bali pia kukemea ubadhirifu wa fedha za makanisa na za wananchi zinazotolewa na wahisani, mashirika, serikali na jamii. Lazima tuwe na mikakati ya kufikia makundi yanayoishi katika mazingira magumu kama vile watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, watoto, vijana, wazee na walemavu kwa kuwapa mafunzo, kutetea haki zao na kuwapa misaada mbalimbali. Kutojali mahitaji ya kimwili na kihisia kunaweza kutufanya tuikose mbingu hata kama tunatoa vizuri huduma za kiroho.

Wapo wanaodai kwamba mafundisho kuhusu mafanikio wameyapa kipaumbele kikubwa. Lakini ukifuatilia sana mkazo wa mafundisho yao, ni kuhusu ‘utoaji’ peke yake. Kumbuka somo la utoaji linalenga kuwasaidia watu wawe waaminifu katika kumtolea Mungu katika kile walicho nacho, wakati somo la uchumi linawasaidia watu wawe na kipato kizuri na matumizi mazuri ili wamzalie Mungu matunda na kuishi maisha bora.

Kama hatuko tayari kushirikiana na watu wengine, tunajifungia nje ya baraka za Mungu na matokeo yake ni kuwabebesha mzigo waumini tunaowachunga zaidi ya uwezo wao. Kimsingi, ugumu unaowapata wachungaji wengi, unatokana na ubaguzi wa kimadhehebu unaowafanya wawe wenyeji wa makundi yao wanayoyachunga peke yake.

4. Kutosheka na maisha ya chini ya kiwango.

Wapo wachungaji ambao wanadhani utumishi ni kuteseka wakati wote. Kwa hiyo, kwa upande wao maisha ya raha ni anasa na ni dhambi. Wapo tayari kujitesa hata pale ambapo Mungu anataka kuwatia moyo na kuwaburudisha. Biblia inatuagiza turidhike na vitu tulivyo navyo (1 Tim 6:6) lakini hii haimaanishi tutosheke na vitu tulivyo navyo.

Ni vizuri zaidi kwa mchungaji na mwenzi wake (mkewe au mumewe) kutambua kiasi cha fedha kinachohitajika kwa mwezi kwa ajili ya familia na kisha kumwambia Mungu aliyewaita badala ya kusubiri kumshukuru Mungu kwa chochote watakachokipata. Katika hili hatuhitaji kuangalia uwezo wa kiuchumi wa waumini tunaowachunga bali ukubwa wa mahitaji yetu na uwezo wa Mungu. Lazima pia tutambue kwamba Biblia haisemi fedha yenyewe ni mbaya bali inasema kibaya ni ‘kupenda fedha’.

5. Waumini kutotambua maumivu ya familia za wachungaji wao

Waumini wengi hawatambui maumivu na mateso ya wachungaji wao. Wanafunzi wa Yesu hawakutambua kwa nini Yesu amechagua kwenda nao katika maombi. Hawakujua kinachoendelea moyoni mwake. Wachungaji wakipata matatizo ni watu wachache sana makanisani wanaoonyesha kujali na kama watajali ni kwa mchungaji peke yake na si kwa mkewe na watoto wake. Mzigo wa huduma waliokuwa nao awali kwa ajili ya wachungaji wao umepungua kama sio kutoweka kabisa.

Zipo sababu mbalimbali zinazowafanya waumini wapoteze shauku. Mojawapo ni kwamba kadiri kanisa linavyokua, ndivyo majukumu ya mchungaji yanavyoongezeka na kumfanya mchungaji ashindwe kuwatembelea washirika mara kwa mara kama walivyokuwa wamezoea. Pia hali ya mchungaji kimaisha inapoanza kuwa nzuri au Mungu anapomuinulia watu wanaomjali, wapo waumini wanaoanza kumuonea wivu badala ya kufurahia mafanikio yake. Mt 26:8,9 ’Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini’. Kuna watu wakiona mchungaji amefanikiwa, wanaamua kuacha kutoa zaka (sehemu ya kumi ya mapato yao) katika kanisa analochunga ingawa bado wanahitaji mafundisho yake, maombi yake na ushauri wake. Kufanya hivi ni kutafuta laana na kusahau kwamba si kazi ya muumini kupanga matumizi ya zaka bali jukumu lake ni kumtolea Mungu kama Neno lilivyoagiza. Kama mtu ameona hakubaliani na utaratibu wa utoaji uliowekwa na kanisa husika, asiyaasi maono wakati bado anaendelea kupokea msaada wa kiroho kupitia huduma hiyo. Labda tu kama amepata maelekezo maalum kutoka kwa Mungu kutokana na ubadhirifu wa fedha uliopo au kutokana na sababu za Mungu mwenyewe ambazo zinampa amani moyoni na ambazo hazipingani na Neno la Mungu.

Mchungaji anaweza kusafiri kwa muda mrefu na washirika wasikumbuke kuiangalia familia yake aliyoiacha nyumbani. Wanashindwa hata kutembelea tu familia ya mchungaji wao ili kuijulia hali. Wanasubiri wasikie mchungaji amerudi ndipo wafike kumuona, tena kwa ajili ya kumshirikisha matatizo yao tu. Wakati mwingine waumini wajifunze pia kushirikisha baraka wanazopata ili wasiwachoshe watumishi wa Mungu. Gal 6:6 ’Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote’. Mchungaji pia kama mtu mwingine yeyote anahitaji kuwa karibu na familia yake mara tu anaporudi safari. Hata kama yeye mwenyewe haoni hilo, mkewe na watoto wanamuhitaji. La kushangaza unaweza kukuta washirika wanapomtembelea mchungaji wanaongea naye hadi usiku wa manane na kusahau kwamba wanainyang’anya familia yake faragha. Lazima busara itumike katika mahusiano yetu na familia za wachungaji ili tuwe baraka badala ya kuwa kero. Wajibu wa kwanza wa mchungaji, ni kwa Bwana; wa pili, ni kwa familia yake na wa tatu, ni kwa kanisa. Mungu alianzisha familia kabla ya kuanzisha kanisa hivyo tuheshimu mpangilio wake. Hivyo, tunapomkuta mchungaji anaongea na mkewe au watoto wake tutambue kwamba yuko pia katika kazi ya Mungu.

Ni wachache wanaotambua kwamba mchungaji anachoka baada ya huduma hivyo anahitaji kupumzika. Unagundua udhaifu huu kwa kuona jinsi watu wanavyokuwa wengi wakimsubiri mchungaji baada ya ibada kwa matatizo ya kawaida badala ya kuomba wapangiwe siku ya kumuona katikati ya wiki. Washirika wengine wanaona kwamba katikati ya wiki hawataweza kuvunja shughuli zao kuja kumuona mchungaji. Hivyo wanataka wamalizane naye siku hiyohiyo ya ibada kuu.

Ni lazima tuwe na huruma na tutambue muda unaofaa kumshirikisha mchungaji masuala nyeti. Si wakati wote unafaa kumshirikisha mchungaji kila jambo. Mhu 3:1 ’Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu’. Tuombe hekima ya Mungu kama malkia Esta ili tujue wakati  muafaka wa kushirikisha masuala nyeti. Sio busara kumshirikisha mchungaji suala nyeti la kiroho wakati umemkuta anasikiliza taarifa ya habari au anakula chakula. Soma mazingira na nyakati kabla ya kushirikisha mahitaji yako yanayohitaji majibu makini.

6. Kupata upinzani usiokoma katika huduma.

Wapo waachungaji ambao wamepata upinzani katika huduma kwa miaka mingi kiasi kwamba wamepoteza imani na viongozi wakuu wa madhehebu yao. Wengine wametengenezewa kesi ili tu wafukuzwe halafu wengine wachukue nafasi zao. Tena wamefukuzwa kwa kazi ambazo waliwekeza nguvu zao na mali zao kwa miaka mingi na kusahau hata kujenga nyumba zao binafsi. Kilio hiki kiko kwa wengi na kimechangia sana kuwa na utitiri wa madhehebu ambayo ukifuatilia sana yana imani moja na mfumo mmoja. Kwa vile madhehebu mengi hayakuandaliwa kupokea maono mapya, hayana fursa ya kuingiza maono mapya kutoka kwa Bwana. 

Kwa wengine, vita inaanzia ndani ya kanisa hasahasa kwa wale ambao wanafurahia kupokea vikundi vinavyojimega kutoka kanisa jingine. Mara nyingi kikundi kilichojimega kutoka kanisa jingine, kinakuja na mchungaji wake wa siri. Siku huyo mchungaji wa siri akiasi maono aliyoyakuta, kikundi hicho kinaweza kutoka naye na kubeba wengine kadhaa ambao kiliwakuta.

Wakati mwingine vita ya ndani inaanzishwa na mchungaji mwenyewe kwa kuweka matajiri katika uongozi hata kama ni wachanga kiroho au wamehamia tu siku za karibuni kutoka mahali pengine na hawajayaelewa vizuri maono ya kanisa hilo. 1 Tim 3:6 ‘Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi’. Mchungaji anaweza kudanganyika kwamba kwa kuwapa majukumu wageni hao matajiri, atawafanya wadumu katika kanisa lake bila kuhamia kanisa jingine.  Anasahau kwamba kanisa linakuzwa na Bwana na sio kwa ujanja. Pia anasahau kwamba mtu ambaye hujawahi kumuona akiwa amekasirika, hujamfahamu bado. Ni vigumu kujua mgeni ataitikaje siku atakapokemewa kwa kosa alilolifanya. Tunahitaji muda wa kutosha katika kufahamu vizuri uwezo na udhaifu wa mgeni kabla ya kumuingiza katika maeneo nyeti ya huduma.

Vita nyingine inaweza kuanzia ndani ya familia ya mchungaji. Kama huduma ya mchungaji haikamilishani na ya mkewe bali zinashindana, ni rahisi kushindwa kuinuana katika utumishi. Ikiwa mchungaji na mwenzi wake wote ni wahubiri, kila mmoja anaweza kuangalia makosa ya mwenzake na kujisemea moyoni, ‘Kama angenipisha nihubiri mimi, ningetumiwa na Mungu zaidi kuliko yeye’. Hivyo anakosekana wa kumuombea mwenzake. Badala yake, kama huduma zinakamilishana (complementary), mmoja anajisikia fahari anapomuona mwenzake akitumika hivyo anamtia moyo zaidi na kumuombea. Mchungaji anahitaji kutiwa moyo na watu wa nyumbani mwake. Mchungaji anapotiwa moyo na watu wengine kuliko mwenzi wake wa maisha, upendo wake unaweza kuhamia kwa watu wengine na kufungua mlango wa dhambi. Wanandoa wanapaswa kulindana kwa kuonyeshana upendo kwa vitendo badala ya kutumia maandiko ya Biblia peke yake katika kudai upendo. Mtu yeyote anayetaka kupendwa, anatakiwa kupendeza na kujali mahitaji ya mwenzake na sio kudai peke yake wala kulaumu.

Kipindi kijacho utajifunza kuhusu KUWANUSURU WACHUNGAJI KUTOKA KATIKA MAUMIVU

Soma kwa kina utangulizi hadi sura hii kupitia kiungo hiki https://www.lawimshana.com/p/books-vitabu.html

Nakukaribisha kutoa sadaka yako ya upendo kwa ajili ya kuwezesha huduma hii tunayoitoa bure ingawa inalipiwa mtandaoni

TigoPesa: +255 712 924234

Mpesa: +255 754 653217

CRDB Bank: 0152219784300

Dkt. Lawi Mshana