UWE MAKINI NA BAADHI YA MANABII UNAOWAAMINI KUPITA KIASI (HIKI NI KISA CHA KWELI)
Niliwahi kuwa mwanamke mfanyabiashara aliyefanikiwa sana. Nilikuwa tajiri mwenye maisha mazuri sana. Nilikuwa na kila kitu mwanamke anachotamani kuwa nacho. Niliolewa mara mbili lakini ndoa zote zilikufa mapema kwa sababu sikupata ujauzito. Nilitafuta sana kupata mtoto wangu mwenyewe bila mafanikio.
Baada ya kupewa talaka ya pili, rafiki yangu alinikaribisha kanisani kwake ambapo Nabii kutoka nchi fulani (sitaitaja) alinitabiria kwamba mwanaume anayeendesha gari la thamani (BMW) atanichumbia na tutapata watoto mapacha.
Unabii huo ulifuatiwa na kelele za shangwe kutoka kwenye kusanyiko zikisema “Chimbua zaidi baba.” Aliniambia kwamba “nitakutana na mtu huyo wa kunioa miezi sita ijayo.” Akataja mpaka simu ya mtu huyo. Kulikuwa na shangwe na nderemo kanisani na nilifurahi kwamba hatimaye maombi yangu yamejibiwa.
Niliacha kuendelea kusali katika kanisa langu la zamani na kujiunga na kanisa la nabii huyo. Nilijitoa kikamilifu na sikukosa hata ibada moja.
Nilitoa zaka kila wiki na kwa vile nilikuwa kati ya washirika wachache matajiri katika kanisa hilo, kanisa lilinitegemea kwa mahitaji ya kiuchumi yanayojitokeza. Niliombwa kuchangia matangazo ya redio, kodi ya jengo la kanisa na wakati mwingine kodi ya nyumba alipoishi mtu wa Mungu.
Na kweli kama yalivyokuwa maneno ya Nabii baada ya miezi sita nikiwa kwenye duka langu la mapambo nilitembelewa na mwanaume mzuri ambaye alitaka kununua mapambo ya Kimisri lakini kwa bahati mbaya tuliishiwa na aina aliyoiulizia. Kisha aliandika namba yake ya simu kwenye karatasi na kunipatia na kuniomba nimpigie siku tutakapapopata mapambo hayo. Pia aliomba namba yangu ya simu. Nilipompatia namba yangu ya simu alitoka nje na kuingia kwenye gari lake aina ya BMW na kuondoka.
Nilipojaribu kuhifadhi namba yake kwenye simu yangu, nilitambua kwamba ni namba ileile aliyoitaja Mtu wa Mungu kanisani miezi sita iliyopita na akawa anaendesha BMW kama nilivyokuwa nimetabiriwa.
Nilifurahi sana na muda huohuo nikampigia Nabii na kwenda kukutana naye kwenye ofisi ya kanisa. Nabii akaniambia kwamba unabii ulikuwa sasa unatimia na akanishauri kumuachia Mungu mambo yote. Nakumbuka nikampatia k5000 siku hiyo kama shukrani.
Jioni hiyohiyo, yule kijana akanitumia meseji ya simu akaniambia jina lake na kwamba ameniona mimi ni mrembo sana na hivyo ndivyo tulianza mawasiliano. Kisha tukakutana siku iliyofuata hotelini kwa chakula na ndipo tukaanza uchumba. Nakumbuka nilitoa ushuhuda wa nguvu kanisani Jumapili iliyofuata.
Baada siku kadhaa kupita Nabii akaniita na kuniambia kwamba amepata maono kutoka kwa Mungu kwamba niuze baadhi ya mali zangu kwa vile naanza maisha mapya, maisha yaliyothibitishwa na Mungu. Niliambiwa kuuza nusu ya mali yangu na kutoa pesa kanisani. Nikaambiwa kwamba ndani ya miezi mitatu nitapa upenyo wa kujenga majumba makubwa.
Nikafanya kama Nabii alivyonishauri kufanya. Nikauza nyumba zangu tatu kati ya sita na kumpatia Nabii pesa. Baada ya hatua hiyo nikafilisika. Biashara zangu zikafa na nyumba zangu tatu zilizobaki zikachukuliwa na benki kwa kushindwa kurejesha mkopo. Nikashushwa maisha hadi sifuri. Kisha Nabii akanifukuza kanisani akinituhumu kwamba ninatembea na washirika kanisani.
Yule kaka aliyenichumbia naye akaniacha. Baadaye nikagundua kwamba huyo kaka na Nabii ni mtu na mdogo wake. Ulikuwa ni mkakati uliokuwa umepangwa ili kunichukulia mamilioni ya kwacha. Nabii sasa anaishi maisha ya anasa wakati mimi nimefilisika kabisa.
Nimemuachia Mungu kila kitu. Najua kwamba Mungu ninayemtumikia yu hai na kwamba atanipigania vita zangu na kurejeza kila kitu nilichoibiwa.
Ipo siku manabii hawa wa uongo watafichuliwa na kuaibishwa hadharani. Kuwa makini na hawa manabii unaowaamini sana.
Karibu sana utoe maoni hapo chini.