Ticker

6/recent/ticker-posts

Uanafunzi (sehemu ya tatu)

II. UMEJIANDAA KUSAIDIA WAAMINI WAPYA? Pengine unajiuliza. ‘Nani? Mimi? Sijui la kusema; sijawahi kusoma shule ya Biblia; hakuna mtu amewahi kunifundisha jinsi ya kufanya hivyo’. Kumbuka Yesu aliwatumia watu wa kawaida wasio na elimu ya shuleni. Mdo 4:13 ‘Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu’. Hatuhitaji kuwa wakamilifu ndipo tuanze kazi hii. Mungu alimuahidi Musa, ‘Nitakuwa pamoja nawe’ (Kut 3:12). Na Yesu aliwaahidi wanafunzi wake, ‘mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari’ (Mt 28:20). Wanafunzi wake hawakuwa shujaa sana ndiyo maana walikimbia Yesu alipokamatwa katika bustani ya Getsemane. Lakini walipojifunza kwamba Yesu yuko pamoja nao, wakawa tayari kufanya lolote alilowataka wafanye. Mungu ndiye anayetupa uwezo, hekima na ujasiri ili tumalize vyema.1 The 5:24 ’Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya’. Hata hivyo, kuna mambo kadhaa yanayopaswa kuonekana katika maisha yetu kama tunataka kusaidia wengine wakue katika maisha yao ya Kikristo. 1) Tuwe na maisha ya ushindi katika majaribu na dhambi (1 Pet 2:12). Tutaishi maisha ya ushindi tukiwa na uhusiano wa upendo na ushirika na Yesu Kristo na tukiwa tumejazwa Roho Mtakatifu. 2) Tuwe tayari kujitoa kwa ajili ya mwingine anayetaka kukua. Uanafunzi unahitaji muda. Wanafunzi wajue kwamba wanaweza kutujia wakati wowote wanapotaka kutushirikisha mawazo yao na matatizo yao. 3) Tujue kwamba tunatakiwa kutunza siri za yale wanayotuambia bila kuyasema kwa wengine. Wanahitaji kujua kwamba hata kama watatushirikisha ugumu wowote au dhambi ya siri, hatutawahukumu. Wanahitaji kujua kwamba wana thamani kwetu. 4) Tuwe tayari kuomba msamaha tunapowakosea. Wanahitaji kujua kwamba hatujafikia ukamilifu lakini tunapitia magumu wanayoyapitia. 5) Tuwe jasiri kusema ukweli ili kuwakemea na kuwaonya wanafunzi wetu wakiendelea na mwenendo mbaya (Lk 17:3). Lakini wakati wote tujitahidi kuongea katika upendo (Mit 17:17a). 6) Tuwe tayari kuacha kufanya jambo ambalo tunaona kwamba linamsababisha mwanafunzi ajikwae (Rum 14:1-3, 13-15, 19-21). Mambo muhimu ya kukumbuka kuhusu uanafunzi: 1) Ni Mungu anayefanya kazi ya kuwabadilisha wanafunzi. Roho Mtakatifu analitumia Neno la Mungu kuwabadilisha watu. (Fil 2:13; 1 Kor 3:6). 2) Tusiwe wakubwa sana kwa wanafunzi wetu. Badala yake tuwe watumishi wa kiroho. Wajifunze kufanya analotaka Mungu na sio tunanalotaka sisi wala wanalotaka wao. Kol 1:28. 3) Tunaweza kutoa mafunzo kwa maneno yetu, lakini mfano wa kuigwa ni muhimu pia. 4) Kumsaidia mwingine akue kunahitaji uhusiano. Mwalimu asijione kwamba ni muhimu kuliko mwanafunzi wake. 5) Uanafunzi ni urafiki, kwanza na Mungu na kisha na waamini wengine. III. MOYO WA ‘MFANYA UANAFUNZI’ 1) Moyo wa maombi 1 The 1:2-3 Paulo aliombea wengine. Yn 17 Yesu aliombea wanafunzi wake, na sisi tumejumuishwa. Kol 4:12 Epafra aliwaombea kwa bidii. Hebu angalia Paulo alivyoombea: Efe 1:15-18; Fil 1:3-11; Kol 1:3-14. 2) Moyo wa ushujaa 1 The 2:2 Paulo hakusubiri waamini wapya wamjie kwa ajili ya kuomba msaada. Aliwaendea ingawa alipata mateso mengi huko Filipi. 3) Moyo wa mama 1 The 2:7 Waamini wapya wanahitaji upole na huruma. Yaani, tuwasikilize vizuri kabla ya kuongea na tuonyeshe upendo badala ya hukumu. 4) Moyo wa baba 1 The 2:11-12 Wakati mwingine tunatakiwa kuwafundisha mambo magumu ili wajifunze kuwa jasiri na kusimama katika imani yao. Tuwafundishe kujitegemea. Wakati mwingine tuweke wazi udhaifu wao na dhambi zao. 5) Moyo wa kushirikisha nafsi 1 The 2:8 Waamini wapya wanahitaji mambo mengine zaidi ya mafunzo peke yake. Tunatakiwa tushirikishe maisha yetu yote kwao. Mfano: a) Kuwa tayari kuwashirikisha magumu tunayopitia bila kusahau ushindi tunaoupata. b) Fanya matembezi nao. Nendeni dukani pamoja, kuchota maji na hata kutembelea wagonjwa. c) Wakaribishe nyumbani kwako. Wanahitaji kuona jinsi tunavyoishi. Wanahitaji kuona kwamba si kila kitu ni kamili katika nyumba zetu. Wanahitaji kuona tunavyohusiana na wenzi au watoto wetu. Wanahitaji kuona tunaadibisha vipi watoto wetu. 6) Moyo usio na lawama. 1 The 2:10 Tukumbuke kwamba tunayotenda yana sauti zaidi kuliko tunayosema. 1 The 2:3-6. IV.UTEKELEZAJI 1.Jiandae vizuri. Msikilize Roho akuongoze kwamba uanze na somo gani. 2.Uwe na lengo kichwani kwa ajili ya mwanafunzi wako. 3.Uwe na maandiko ya kutumia. Usitumie maandiko mengi sana kwa wakati mmoja. 4.Uwe na mifano hai ya kuelezea unachofundisha. 5.Uwe na andiko la kukumbuka. Likariri pamoja naye ili aone kwamba hata wewe unapenda kuliweka Neno moyoni mwako. USHAURI Ndugu msomaji/mwanafunzi, napenda kukutia moyo kwa utayari wako wa kujifunza masomo haya ya kufanyika mwanafunzi wa Yesu. Mpango wa Mungu kwako si kuwa mshirika wa kanisa tu, bali kuwa mwanafunzi wa Yesu (Mt 28:19) Jitahidi kumaliza masomo yote (kozi nzima) ya uanafunzi ili ufae kufundisha na wengine (2 Tim 2:2). Dr Lawi E. Mshana, Box 554 Korogwe, Tanga, Tanzania.