Mara nyingi unatawaliwa na matatizo yasiyoisha kwa vile hujagundua chanzo halisi cha matatizo yako. Ni kweli kwamba adui mkuu wa vita zetu ni shetani lakini sio mara zote anatushambulia moja kwa moja. Hasa anapogundua kwamba una nguvu za Mungu hakusogelei kichwa kichwa. Hivyo njia mbadala anayotumia ni kuangalia unazungukwa na watu wa aina gani. Mika 7:6 “Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe.”
Maadui walifanya hivyohivyo wakati wa kutafuta kumuua Yesu. Walihitaji mtu wa karibu naye ili wapate taarifa sahihi kwamba yuko wapi, anafananaje na wasishtukiwe. Maadui hawangejua kirahisi ratiba ya Yesu kuwa mlima wa Mzeituni na pengine walikuwa hawamjui vizuri sura yake. Hivyo walihitaji mmoja wa wanafunzi wake awape data za kutosha na mwongozo. Ukifuatilia utagundua kwamba Yuda alienda kumbusu Yesu kama wanafunzi wa Yesu walivyokuwa wamezoea kusalimiana naye ili amtofautishe Yesu na wanafunzi wengine waliokuwepo. Mtu anayetaka kukusaliti lazima awe ni mtu wa karibu na wewe ambaye anakujua na nyendo zako zote. Ni mtu ambaye akisema lolote kuhusu wewe ni rahisi kuaminika maana aliwahi kuwa karibu na wewe. Mathayo 26:48-50 “Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu.Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu.”
Mtu anayekusaliti ili amchukue mumeo, mkeo, rafiki yako au kazi yako LAZIMA AKUBUSU KINAFIKI. Unajua kwa nini? Ili usimshtukie na umpe uhuru mkubwa iwezekanavyo. Hata hivyo Bwana Yesu aligundua nia ya Yuda na kwa vile alijua anatimiza andiko hakumuona kama adui bali alimwambia, RAFIKI, FANYA ULILOLIJIA. Luka 22:48 “Yesu akamwambia, Yuda, wamsaliti Mwana wa Adamu kwa kumbusu?”
BIBLIA INASEMAJE KUHUSU HUU USALITI
1. Kuna mchawi aliokoka lakini akaendelea na uchawi wake kanisani
(i). Huyu Simoni alikuwa mchawi mkubwa akaamua kuokoka
Hakuokoka na kubaki nyumbani bali aliamua kubatizwa na kisha akaambatana na wapakwa mafuta wa Bwana.
Mdo 8:9,13 “Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.”
(ii). Huyu Simoni ingawa aliokoka alitaka kuendelea na uchawi katika staili ya kilokole (charismatic witchcraft) – kutaka azipate karama za Mungu kwa kuzinunua na azitumie kwa umaarufu wake na sio wa Yesu. (Je hatuna hawa watumishi ambao wameenda kwa wachawi kununua upako bandia ili wafanye miujiza ya kiini macho ambayo imevuta na kudanganya hata wateule wa Mungu). Marko 13:22 “kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule.”
Mdo 8:18,19 “Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.”
(iii). Mtume Petro alimkemea na kumuonya ATUBU kutokana na fikra hiyo ovu sana kuhusu utendaji wa Roho Mtakatifu. Alipoambiwa ATUBU yeye akaomba aombewe na hakuna mahali paliposema kwamba mtume alimuombea. MAOMBI au MAOMBEZI kamwe hayawezi kuwa mbadala wa TOBA.
Mdo 8:20-24 “Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako. Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu. Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja.”
Watu wa aina hii wanahitaji MAONYO na sio MAOMBI. Mungu ametuagiza kuomba lakini kuna maeneo mengine ametuagiza kuonyana. Warumi 15:14 “Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana.”
2. Kuna marafiki wanafiki unaosali nao ambao wanatamani mabaya yakupate
Ukitoa ushuhuda kanisani hawa watu wanaongoza kupiga makofi na vigelegele lakini moyoni hawako pamoja na wewe.
Zab 55:12-14,16 “Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa Mungu pamoja na mkutano. Nami nitamwita Mungu, Na Bwana ataniokoa.”
Ukifuatilia sana hawa watu wanataka kupata kitu kwako lakini hawachangii chochote katika maisha yako. Ni ‘kupe’ ambao wanakufaidi na wakati huohuo wanakusema vibaya kwa watu wengine.
Huwezi kujificha kwa watu hawa hivyo uwe tu makini kwamba si kila anayekuchekea anafurahia maendeleo yako hata kama mnasali naye. Usishirikishe maono na mipango yako kwa kila mtu ukitegemea afurahi. Muulize Yusufu alivyotafsiriwa vibaya na ndugu zake wa damu mpaka wakaamua kumpoteza kabisa. Mwa 37:8,19,20 “Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”
3. Kuna watu ulio karibu nao wanaokuwinda na kukuloga
Pengine unajidanganya kwamba hakuna wachawi. Au unakiri tu kwamba hulogeki wakati humjui Mungu na wala huombi. Sio lazima wanaokuloga wakufanye uwe mgonjwa. Wanaweza kukwamisha maisha yako ingawa kimwili una afya. Watu hawa wako makanisani, maofisini, safarini, majumbani nk
Ezekieli 13:18-20 ”useme, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wanawake wale, washonao hirizi katika viungo vyote vya mikono, wawekao leso juu ya vichwa vya kila kimo, ili wawinde roho za watu; je! Mtaziwinda roho za watu wangu, na kuzihifadhi hai roho zenu wenyewe? Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni kinyume cha hirizi zenu, ambazo kwa hizo mnaziwinda roho za watu kama ndege, nami nitazitoa katika mikono yenu kwa nguvu; nami nitaziachilia roho zile mnazoziwinda kama ndege.”
Mungu akufungue macho ili uwatambue watu wanaoharibu juhudi yako isiwe na matokeo. Mtume Paulo aliwahi kumhubiri mtu habari njema akagundua kwamba jirani yake anamloga ili asiokoke. Alichofanya ni kumshughulikia yule mchawi ndipo aliyekusudiwa akaokoka.
Mdo 13:7-12 “mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza. Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”
Kuna watu kama tutaendelea kuwapuuza, wataharibu kabisa mustakabali wa maisha yetu. Lazima tutumie SILAHA ZENYE UWEZO KATIKA MUNGU. 2 Wakorintho 10:4 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)” Bomoa madhabahu ya adui anayezuia maendeleo badala ya kujiombea wewe mwenyewe tu kila siku (Shambulia na kujilinda). Lakini pia ili tusilogeke maadui wasiwe na sababu (mashitaka ya haki). Mithali 26:2b “Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”
Unaruhusiwa kuuliza swali lolote.