USITAFUTE KUPENDEZA WATU UNAPOTAFUTA MWENZI WA MAISHA
Kosa ambalo watu wengi wanafanya wanapotaka kuoa au kuolewa ni
kujaribu ku-impress (kupendeza) marafiki, majirani, wapendwa, ndugu na
washirika wenzao. Hakuna mtu atatosheka na chaguo lako. Unajua kwanini? YEYE
SIO WEWE NA HAKUJUI VIZURI! Wewe ndiyo unajua pengo ulilo nalo katika maisha
yako na ungependa lijazwe na mtu wa aina gani. Wakati watu wanapokulinganisha
na yeye wanaangalia mambo mengi kv elimu, umbile, rangi, urefu, umri, uchumi,
huduma, umaarufu nk. Lakini hivi vyote havina uhusiano wa moja kwa moja na pengo
ulilo nalo ingawa vinaweza kuwa na mchango fulani. La msingi tu usikubali
kupofushwa na kigezo kimoja na kupuuza vingine vya muhimu. Pengo lako
linahitaji kujazwa kiakili, kiroho, kimwili na kihisia – hivyo hakikisha moyoni
mwako unaridhika kuishi na mtu kwa uwiano mzuri. Kuna mtu aliamua kujali tabia
ya kiroho peke yake na kupuuza vigezo vingine. Matokeo yake ikamgharimu. Aliamua
kumuoa msichana kwa vile tu ana sauti nzuri ya kuimba kanisani ingawa alikuwa
havutiwi na sura yake. Walipoishi pamoja akawa na wakati mgumu kwa vile hawezi
kuimba mara kwa mara nyumbani na wakati huohuo hampendi katika maeneo mengine. Ilibidi
awe anamuomba wakati mwingine aimbe pambio ili avute hisia zake za upendo (mvuto
wake wa awali uje tena). KWA HIYO USIPENDE KUJIDANGANYA MWENYEWE. Mpende unayetaka
kuishi naye katika maeneo yote muhimu bila kusahau kumuomba Mungu akuongoze
katika upendo wako ili usiwe upendo wa bandia. Hata Neno la Mungu linakutaka
uishi kwa furaha na mke umpendaye na sio mke anayefaa kuonyesha watu. Utajuta
pale watu watakapokudhania una-enjoy sana kuishi naye kwa mtazamo wa nje,
wakati nyumbani unaishi na ‘mwiba.’Mhubiri 9:9 “Uishi
kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili,
ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako
ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.”
Hata hivyo, hakuna kanuni maalum za mvuto unazoweza kuzitumia pale unapokutana na mtu ambaye ni chaguo lako (There is no rules of attraction when it comes to meeting your match). Wakati mwingine hata wewe mwenyewe hujifahamu vizuri lakini Mungu aliyekuumba anajua kilicho bora zaidi kwa ajili yako. Inapotokea hivyo (kuvutiwa bila sababu zinazoeleweka kibinadamu), muombe Mungu ugundue sababu iliyojificha. Ila usikubali kulazimishwa na zawadi au watu wakati MOYO WAKO UNAKATAA. Hakuna mbadala wa ndoa, hivyo kuwa makini sana! Wanaoshindwa kutulia leo walishindwa kukutana na mtu wa kuziba pengo lao au wameshindwa kutambua vizuri wamepungukiwa nini. Upungufu mwingine ulio nao moyoni hauhitaji upendo wa kimwili (mapenzi) bali upendo wa Mungu umiminwe moyoni mwako. Warumi 5:5 “na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.”
Lawi Mshana