KWANINI WAKRISTO WANAOA ILHALI YESU KRISTO HAKUOA?
Hivi karibuni mke wangu aliulizwa swali hili wakati
akishuhudia kuhusu wokovu ulioletwa na Yesu Kristo. Hivyo akaniomba nimpatie
ufafanuzi zaidi. Nimeona umuhimu wa kuandika jibu la swali hili kwa kirefu kwa kutumia
Maandiko Matakatifu (Biblia).
Ili kulijibu vizuri swali hili lazima tujue tofauti ya kazi
aliyopewa Adamu wa kwanza (Adamu wa Edeni ya duniani) na Adamu wa mwisho (Yesu
wa Edeni ya mbinguni au Peponi/Paradiso). Adamu wote wawili wana sura ya Mungu.
Mwanzo 1:26a “Mungu akasema, Na tumfanye
mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu.” 2 Wakorintho 4:4 “ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini,
isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”
Kuwa na sura ya Mungu kunamaanisha kwamba mtu amepewa
‘utashi’. Uwezo huu wa kuhisi, kufikiri na kuamua tumepewa sisi wanadamu lakini
malaika hawakupewa. Wana nguvu kuliko sisi lakini wanasubiri tu maelekezo na
maagizo. Ndiyo maana mwanadamu anabuni na kugundua vitu vingi na anaweza
kuchagua kumkataa na kumtukana Yesu leo na asifanywe chochote mpaka siku ya
hukumu ndipo atashughulikiwa. Tumepewa uhuru wa kuchagua aina ya maisha
tunayotaka na kuwa tayari kwa matokeo yake (consequence). Kum 30:19 “Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi
leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua
uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako.”
Tofauti
ya Adamu wa kwanza na Adamu wa mwisho
1. 1 Wakorintho 15:45 “Ndivyo
ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni
roho yenye kuhuisha.”
Andiko hili lina maana kwamba Adamu wa kwanza alikuja kama
NAFSI ILIYO HAI (living being) yaani ‘kiumbe mwenye uhai’ wakati Adamu wa
mwisho, yaani Yesu Kristo alikuja kama ROHO YENYE KUHUISHA (a life-giving
spirit) yaani ‘roho anayetupatia uhai.’ Kwa lugha rahisi, Adamu wa kwanza ni
MWILI WENYE ROHO wakati Adamu wa mwisho ni ROHO YENYE MWILI. Adamu wa kwanza ni
mwili uliopuliziwa pumzi ya Mungu (Mwa 2:7) wakati Adamu wa mwisho ni Mungu
aliyefanyika mwili (Yn 1:14).
2. Adamu wa kwanza aliumbwa aishi duniani maisha yake yote
wakati Adamu wa mwisho alikuja duniani kwa muda maalum na kwa misheni maalumu.
Maisha Yake ya milele yako mbinguni. Yesu hakuja duniani kuleta amani bali
kumpokonya shetani watu anaowatesa na kuwapeleka mbinguni. Luka 12:51 “Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta
amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.” 1 Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu
mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”
Kwa mujibu wa Biblia, sifa ya kwanza ya mpinga-Kristo ni mtu anayekataa
kwamba Kristo ni Mungu aliyekuja duniani katika mwili (incarnation). 1 Yohana 4:2.3 “Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho
ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na
kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga
Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.”
3. Adamu wa kwanza alipewa kazi ya KUZAA NA KUONGEZEKA
wakati Adamu wa mwisho alikuja KUMNUNULIA MUNGU WATU waliokuwa wameuzwa kwa
shetani.
Mwanzo 1:28a “Mungu
akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na
kuitiisha.” Ufu 5:9 “Nao waimba
wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri
zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila
na lugha na jamaa na taifa.” Usisahau pia kwamba Mungu aliagiza watu
waongezeke kabla ya anguko la dhambi ya Adamu na Hawa na baada ya kuangamiza
wenye dhambi kwa gharika kipindi cha Nuhu (Mwa 9:1). Moyo wa Mungu ni kutaka
waongezeke wenye haki na sio wenye dhambi.
Kwa hiyo Bwana Yesu hakuja kuonyesha namna ya kuoa na
kuzaa. Hiyo kazi ilikuwa ya Adamu wa kwanza na alishaifanya na bado inaendelea.
Kazi iliyomleta Yesu duniani ni kumsaidia mwanadamu awe na sifa za kuingia
mbinguni. Tambua kwamba mwanadamu hakuumbwa kwa ajili ya kwenda mbinguni wala
kwenda Jehanum. Alikusudiwa kukaa duniani milele. Ndiyo maana ilibidi mambo
kadhaa yafanyike baada ya anguko la dhambi:
1. Mwanadamu asamehewe dhambi na kuandaliwa kuwa na maisha
matakatifu ya viwango vya mbinguni (yenye utukufu wa Mungu).
Warumi 3:23 “kwa
sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” Waefeso
5:27 “apate kujiletea Kanisa tukufu,
lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo
na mawaa.” Hakuna kinyonge kitakachoingia mbinguni. Ufu 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote
kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa
katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.”
Wengi watataka kuingia katika Ufalme wa Mungu lakini hawataweza kwa vile wanategemea matendo yao mazuri badala ya kuipokea neema ya Mungu kupitia Yesu Kristo. Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.” Efe 2:8,9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”
2. Makao yaandaliwe mbinguni kwa ajili ya wale walioamua
kumuishia Mungu.
Yohana 14:2,3 “Nyumbani
mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda
kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena
niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.” Watakaoenda mbinguni hawatafanana.
Itategemea uaminifu na utumishi wao ulivyokuwa wakiwa duniani. Watatofautiana
kiwango cha utukufu. 1 Wakorintho 15:40, 41 “Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake
ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine
ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya
nyota na nyota.” Wengine watakuwa hawana fahari yoyote ingawa wako mbinguni
kwa vile hawakumtumikia Mungu ingawa walimwamini Yesu na kumkataa shetani. 1
Wakorintho 3:15 “Kazi ya mtu ikiteketea,
atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”
Mbinguni tutaishi kama malaika. Hakuna kuoa wala kuolewa. Bwana Yesu ametufundisha kwa MANENO na VITENDO kuhusu namna tutakavyoishi baada ya kuondoka katika dunia hii. Marko 12:25 “Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni.”
3. Mwanadamu aliyeamua kumfuata shetani atatupwa motoni
pamoja naye (hata hivyo Jehanum haikutengenezwa kwa ajili ya mwanadamu).
Mathayo 25:41 “Kisha
atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa,
mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake.”
Mungu ana sifa kuu mbili ambazo zinachanganya wengine – NI
MWENYE UPENDO na MWENYE HAKI. Amempenda mwanadamu kiasi cha kumtoa mwanawe
pekee Yesu Kristo ili kila amwaminiye asipotee. Lakini pia ni mwenye haki hivyo
atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. Hivyo kama unasema Mungu mwenye
upendo hawezi kuwatupa wanadamu motoni, endelea kuchezea kipindi hiki cha
upendo wake kwako. Kuna siku hutaipata nafasi hii tena. Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda
ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali
awe na uzima wa milele.” Zaburi 9:8 “Naye
atauhukumu ulimwengu kwa haki; Atawaamua watu kwa adili.” Swali jingine
linaweza kujitokeza kwamba Mungu alimuoa nani mpaka akamzaa Mwanae. Mtu anaweza
kuuliza swali hili kama tu amempa Mungu mipaka kwamba lazima mwanaume na
mwanamke wajamiiane ndipo azae mtoto. Anasahau kwamba kuna wakati anasema
maembe yamezaliwa wakati hawezi kutuonyesha mume wa muembe huo ni nani. Lakini
pia anasahau kwamba Adamu na Hawa hawakuzaliwa bali waliumbwa na Mungu. Hivyo
Mungu hangeshindwa kumzaa Mwanae bila mwanaume kuhusika.
UPENDO WA MUNGU unadhihirika kipindi hiki cha neema. Itakapofika
siku ya hukumu hatakuwa tena MWOKOZI bali atakuwa HAKIMU. Hapo ndipo tutajua
maana ya HAKI YA MUNGU.
MWISHO
Kama mtu anajua kuhusu hii fursa ya
kwenda mbinguni, hawezi kuishi kama watu wa dunia hii. Ni kweli kwamba Mungu
ameahidi kutubariki pia hapa duniani lakini maisha yetu ni mafupi sana hapa.
Hivyo hatupaswi kutumia muda wetu wote na kujilimbikizia mali kiasi cha kusahau
kuwekeza kwa ajili ya umilele wetu. Kila atakayeingia mbinguni, atakaa mahali
panapoendana na uwekezaji wake kwa Mungu alioufanya akiwa duniani. Ingawa katika
Agano la Kale Adamu wa kwanza aliagizwa kuoa, katika Agano Jipya tunaona Bwana
Yesu akiitwa Bwana arusi na kanisa likiitwa bibi arusi. Ufu 19:7,8 “Na tufurahi,
tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na
mkewe amejiweka tayari. Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing'arayo, safi; kwa
maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.” Pia
tunaona mtume Paulo akisema amepewa KARAMA YA KUTOKUOA. Ndoa ina faida zake
tukiwa hapa duniani lakini sio tiketi ya kwendea mbinguni. 1 Wakorintho 7:7,8 “Ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe
kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa
Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane,
Ni heri wakae kama mimi nilivyo.”
Kazi ya kuleta ukombozi ilikuwa ya muhimu kwa Bwana Yesu na kwetu kiasi kwamba kipaumbele cha siku yake ya kuzaliwa hakikuwepo tangu katika kanisa la kwanza. Adamu wa kwanza na wa mwisho, wote walizaliwa. Lakini Adamu wa kwanza alianguka akatuuza kwa shetani na kuleta kifo. Adamu wa mwisho alishinda kifo akawahamisha watakatifu waliokuwa kuzimu (kuzimu ilikuwa na upande wa makao ya wenye dhambi na upande wa makao ya watakatifu) na kuwapeleka Paradiso, yaani Edeni ya mbinguni. Kumbuka Adamu wa kwanza alipotenda dhambi alifukuzwa asile matunda ya mti wa uzima katika Edeni ya duniani. Mwanzo 3:24 “Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.” Kupitia Yesu tunarejezwa tena Edeni. Ufu 2:7b “Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.”
Naamini kwa sehemu maelezo haya yamekupa mwanga kuhusu
sababu za Bwana Yesu kutokuoa alipokuja duniani.
Sala
ya toba
Omba sala hii kwa kumaanisha kama umetambua kwamba
unamuhitaji Yesu awe Bwana na Mwokozi wako.
“Ee Mungu, naomba unisamehe dhambi zangu. Ulimtuma Mwanao mpendwa Yesu Kristo
afe kwa ajili yangu msalabani. Nakubali kumpokea moyoni mwangu ili anipe maisha
mapya. Naomba uandike Jina langu katika kitabu cha uzima na kunipa Roho wako
Mtakatifu aniongoze na kunifundisha. Nashukuru kwa kuniokoa katika Jina la Yesu
Kristo. Amina.”
Kama umeomba sala hii kwa imani, jitambulishe kwa wapendwa
wanaokiri wokovu ili ujengwe kiroho na kusimama imara katika imani uliyoipokea.
Unaweza kuwasiliana nami kama una swali lolote kuhusu
safari yako mpya ya imani.
Lawi Mshana, 0712-924234