Unajua kwa nini watoto wanalawitiwa na kufundishwa tabia hizo?
Nawashukuru wazazi na walezi ambao waliwaruhusu watoto na vijana wao wenye miaka kati ya 10 na 24 kuja kwenye mafunzo ya kushinda vishawishi na uhatarishi. Tulifunza aina za stadi za maisha, sababu za vijana kujihusisha na ngono mapema, sababu za baadhi ya vijana kutojihusisha na ngono, ushoga na madhara yake, mbinu za kushinda changamoto za ngono, maneno yanayotumika kuwahadaa au kuwalaghai vijana wajihusishe na ngono na utunzaji wa sehemu za siri. Pia tuliangalia video kuhusu kushinda ukatili wa kijinsia na kufahamu afya ya hedhi.
Ziko sababu nyingi za watoto kunajisiwa na kulawitiwa. Napenda
kukupa sababu chache kati ya hizo ili tusaidiane kuchukua tahadhari. Lakini pia
tutambue kwamba tunapaswa kuripoti bila kujali aliyefanyiwa unyanyasaji ni mtoto
wa kumzaa au la. Namba mojawapo ya bure ya kuripoti kuhusu masuala ya ukatili
wa kijinsia ni namba 116.
Baadhi ya
sababu za watoto kulawitiwa na kufundishwa tabia hizo ni:
1. Wazazi kuruhusu watoto wa kiume walale na wageni wasiowajua wakijifariji
kwamba ni wanaume wenzao. Baadhi ya wageni hao ni ndugu wa karibu kama vile
wajomba nk. Wageni hao wanajenga ukaribu na watoto hao na kuwatoa (kwenda nao ‘out’)
na kuwapa zawadi. Wanawapa huduma ambazo ni nadra sana kwa wazazi/walezi
kuwapatia watoto wao. Hali hii inawafanya watoto wawaamini na kuwapenda zaidi hao
wageni na mwishowe wanatumbukia katika majanga.
2. Wazazi/walezi kutofuatilia kwamba watoto wakitembelea ndugu zao
wakati wa likizo wanalala katika mazingira gani. Wanachojali tu ni kwamba mtoto
amefika salama na kupokelewa. Kuna msichana alienda kufanya kazi za ndani mji
fulani akashanga wanalala kitanda kimoja na (sio tu chumba kimoja) watoto wa kiume
na wa kike kutokana na ufinyu wa vyumba vya kulala. Tujiulize nyumba ina vyumba
vingapi na familia ina watu wangapi kabla ya kuwaruhusu watoto kwenda matembezi
ya likizo kwa ndugu au marafiki wa familia.
3. Wazazi/walezi kuwa wakali sana kiasi kwamba mtoto hawezi kutoa
maoni au kupinga wazo lolote. Mtoto anaweza kukataa akitumwa dukani usiku
lakini mzazi hataki kumdodosa. Kumbe kuna watu wabaya anaokutana nao na
kumnajisi na kisha wanamuonya asimwambie mtu. Mtoto anaposhindwa kupatiwa taulo
za kike na wazazi wake, jamii itamsaidia lakini itadai sadaka ya shukrani
kutoka kwake.
4. Watoto wa kiume mara nyingi ni wakimya kuliko wa kike. Hivyo wanapofanyiwa
ukatili wanaweza kunyamaza bila kumwambia mtu yeyote. Wanaona aibu kusema na
baada ya muda wakizoea mchezo huo wanajikuta wameupenda. Watoto hawa wameanza
mtindo mashuleni wa kuomba wakajisaidie kumbe wanaenda kulawitiana vyooni. Na wakati
huohuo mikakati mingi iliyopo ni ya kumlinda mtoto wa kike zaidi. Watoto wa
jinsi zote sasa wako hatarini na inawezekana watoto wa kiume ndio wako hatarini
zaidi.
5. Hata watoto wa kike wanalawitiwa kwa vile mhalifu anataka
aepuke kumpa mimba. Anadhani kwa kufanya hivyo uhalifu wake hautagundulika. Kibaya
zaidi wazazi wengi tunajali zaidi kulinda mtoto asipate mimba na kusahau kwamba
wahalifu wamebadilisha mbinu. Kama msichana atazoea mtindo huu hata akiolewa
anaweza kumshinikiza mumewe. Tumekutana na ndoa kama hizi ambazo mmojawapo analalamika
kwamba analazimishwa kujamiiana kinyume na maumbile na anaambiwa kama anakataa atatoka
nje kutafuta ambao wako tayari.
6. Watoto wa kike wanaotoka familia ambazo zinakagua zaidi kama
ameanza kutembea na wanaume au la bila kutoa elimu ya maadili, haziwasaidii
sana. Watoto wanahitaji elimu na ushauri nasaha zaidi kuliko MAKATAZO YASIYO NA
SABABU ZILIZOJITOSHELEZA. Niliwahi kupata kisa fulani kwamba msichana alitoka
eneo ambapo mwanamke hawezi kuolewa bila kukaguliwa kwanza. Msichana huyu
alipofikia kuolewa akakaguliwa na kugundulika kwamba ana sifa kwa vile hajawahi
kukutana na mwanaume. Walipopima VVU akagundulika ameambukizwa. Walipofuatilia
wakagundua amefanya sana ngono kwa njia ya haja kubwa. Alipoulizwa mazingira
gani hatarishi amepitia akasema, “Nilipoenda nje ya nchi kusoma, niliwaomba
wapenzi walinde sana ubikira wangu ili nisije nikashindwa kuolewa nikirudi
nyumbani. Hivyo wamefanya sana ngono na mimi kwa njia ya haja kubwa.” Kumbuka njia
ya haja kubwa ni rahisi zaidi kupata maambukizi ya VVU kwa vile ni rahisi
kuchanika na kuruhusu VVU kuingia katika mkondo wa damu kwa kupitia michubuko.
(Hata hivyo mtu anaweza kutofanya ngono na bado akawa sio bikira kwa sababu
aliwahi kufanyiwa matibabu, kushiriki michezo mbalimbali nk Lakini wakati
huohuo hapo kuna ubaguzi wa kijinsia kwa vile kijana wa kiume yeye hakaguliwi).
7. Wazazi wanaolala chumba kimoja na watoto wakubwa na ambao
hawajali faragha wanachangia pia kuwaharibu watoto. Siku moja walionekana watoto
wakifanya igizo la kujamiiana. Walipoulizwa wakasema waliona wazazi wao wakifanya
hivyo usiku. Pamoja na kwamba watoto hawa waliwaona wazazi ambao ni baba na mama,
wanaweza kufanya igizo wakiwa wote ni watoto wa jinsi moja au jinsi tofauti.
8. Wazazi/walezi kukosa muda wa kufuatilia mahusiano ya wadada wa
kazi na watoto wao. Hata wanapokuwa nyumbani siku za wikiendi wako busy na
shughuli zingine. Mama mmoja alishangaa mtoto wake mdogo sana akimpapasa usiku
ili amsugue sehemu za siri. Akagundua kwamba dada wa kazi amekuwa akimtumia
mtoto huyo kumfanyia kitendo hicho mara kwa mara. Huyo mama akaweka mtego na
kugundua kwamba kweli msichana huyo anamtumia mtoto wake kufanya kitendo hicho
kwa vidole vyake.
9. Walimu katika shule fulani walishangaa mbona mwanafunzi fulani
ana maisha magumu sana lakini anafanana na mama fulani tajiri katika mji huo. Walipomuita
mama yake mzazi akawapa kisa hiki: “Nilikuwa msichana wa kazi kwenye familia ya
huyo mama tajiri. Nikawa namchezea mtoto niliyekuwa namlea tangu akiwa mdogo
mpaka alipobalehe. Nikashangaa nimepata mimba. Hivyo nikatoroka.” Kijana huyo
akiwa mkubwa akashangaa kwamba ana mtoto bila kujua na wala kudhamiria.
10. Kukataza watoto wasiguse simu badala ya kuwapa mafunzo ya
matumizi sahihi ya simu. Hata kama utamnyima mtoto simu yako anaweza kutumia
simu ya rafiki yake. Hivyo njia bora zaidi ni kumfundisha mtoto matumizi sahihi
ya simu yako kama vile tovuti za masomo ya kujisomea nk na wakati huohuo
ukifuatilia kujua kama aliangalia vitu vingine visivyofaa kwa vile simu inaacha
kumbukumbu. Ukigundua hali isiyo ya kawaida utaweza kumsaidia mapema ili
akawasaidie na wenzake wanaotaka kumpotosha. Kipindi hiki cha teknolojia ya
kidijitali kinahitaji STADI ZA MAISHA kuliko MAKATAZO.
Haya ni machache kati ya mengi ambayo unaweza kuyapata kupitia mafunzo
na ushauri tunaotoa kwenye jamii. Tunafanya warsha na kambi zinazolenga
wanandoa, vijana, wanafunzi, wanawake, wababa, viongozi wa dini, na viongozi wa
jamii bila mipaka yoyote ya kidini.
Katika mpango huu wa vijana unaoitwa NITATOBOA tunalenga
kuwasaidia vijana balehe na vijana wadogo katika masuala ya afya ya uzazi,
teknolojia na uchumi.
Download &
Install app | Lawi Mshana (https://www.appcreator24.com/app2584201-q514wi) ili iwe rahisi kupata mafunzo mengi
kwa maandishi, audio na video. Ukiwa na hii APP utaweza kupata huduma zote bure
kupitia sehemu moja kama vile Blog yangu, TLMC, BFW, Youtube, TikTok, SoundCloud
na Watch & Downlod (utaweza kudownload ninapoweka video hapo).
Dr Lawi Mshana, 0712-924234