Ticker

6/recent/ticker-posts

Kwanini maombi yako mengi hayana majibu dhahiri?


 Kwanini maombi yako mengi hayana majibu dhahiri?

Pengine umekata tamaa kwamba Mungu hajibu hata unapomtumikia kwa kufunga na kuomba. Napenda kukupa somo muhimu la kukusaidia. Nimemuona Mungu akijibu baada ya kufanyia kazi vizuizi mbalimbali.

1. Usijihesabie haki na kuwahukumu wengine

Lk 18:11-14 “Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

Mungu anataka tufunge na kuomba lakini si kwa dharau na kujihesabia haki. Tabia yako ya kujiona uko viwango vya juu kuliko waumini wa madhehebu mengine ndiyo inakuponza. Acha kuwanyoshea kidole watu ambao hujui kwanini Mungu aliwaumba na kwanini pamoja na makosa yao makubwa Mungu hawaangamizi. Waombee bila kusahau kutengeneza maisha yako binafsi. Usipokuwa makini utashangaa usiowatarajia  wakijibiwa kabla yako kwa vile wao wamepondeka mioyo na hawatafuti dhambi za watu wengine.

2. Kuna dhambi unaijua lakini hutaki kuiungama na kuiacha

Zab 66:18-20 ‘Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia. Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake’. Usidhani kosa linaitwa dhambi unapofumaniwa. Mungu anaiona dhambi kuanzia moyoni. Unapokusudia mabaya, hata kama hutayafanya kimwili, tayari umeshaanguka. Ili mradi unahukumiwa moyoni kwamba umemkosea Mungu, kubali na kutubu hata kama wanaokuzunguka hawajui. 1 Sam 3:13 ‘Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.’

Hutapata mafanikio unayoyangojea kama unajaribu kuficha dhambi zako. Acha kuilea dhambi. Huwezi kumficha Yesu wala shetani hata kama unatuficha sisi. Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

3. Unaabudu sanamu katika moyo wako

Eze 14:3 ‘Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?’ Usikubali kitu chochote kichukue nafasi ya Mungu katika moyo wako. Mungu hawezi kumvumilia mtu ambaye hajampa nafasi ya kwanza. Je nafasi yako ya kwanza ni Mungu au ni mke/mume, mpira, mpenzi, kazi, huduma, askofu, dhehebu, dini, pesa! Anza kujichekecha maana vitu hivyo vikiwa kipaumbe chako kuliko Mungu vinakuwa kizuizi. Kumbuka baraka za mtu wa Mungu SIO KUMILIKI PEKE YAKE BALI NI KUFURAHIA ANACHOKIMILIKI. Baraka za Mungu hazichanganyiki na huzuni. Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.” Unapokuwa na mali halafu zinakupa tu umaarufu lakini huzifurahii, bado katika uchumi wa Mungu hujabarikiwa bali umelaaniwa. Ngoja nikupe andiko linaloonyesha kwamba unaweza kumiliki vitu vizuri na bado uwe umelaaniwa kwa vile umezuiwa kuvifurahia. Sio lazima laana ikuzuie kupata. Unaweza kupata na usifurahie unachokimiliki. Kum 28:30 “Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.”

4. Wewe ni bahili na mchoyo

Mit 21:13 ‘Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa’. Unapuuza mahitaji ya wengine ambayo unaweza kuyatimiza. Hakuna mtu ambaye hawezi kumbariki mwingine kwa kitu fulani. Ukikosa kitu cha kutoa, tumia nguvu zako kumsaidia mwingine kazi lakini usione kwamba ni wewe tu mwenye haki ya kusaidiwa. Tafuta unachoweza kumsaidia mwingine kwa kiwango chako hata kama ni kumnunulia chungwa au kumsaidia kazi za nyumbani. Mdo 20:35 “Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”

5. Kuna mtu umekataa kumsamehe na una uchungu moyoni

Mt 6:14-15 ‘Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.  Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.’

Unapofungua mlango ili kumsamehe mtu fulani, tayari umefungua mlango ili Mungu aingie nyumbani kwako. Usijidanganye kwamba uko salama kwa kumtumikia Mungu wakati kuna mtu husalimiani naye. Unashauriwa uache kwanza utumishi wako, ukatengeneze na yeye.

Mt 5:23-26 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”

6. Huombi katika mapenzi ya Mungu

Yakobo 4:3 “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”

Mungu anataka uombe vitu ambavyo ni mahitaji yako halisi. Usiombe kwa tamaa kwa vile tu umeona mtu fulani anacho au unataka kushindana naye. Ridhika na aina ya maisha aliyokupangia Mungu. Mungu atakuinua kwa wakati wake.

1 Yn 5:14 -15 ‘Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.”

Maombi ya leo

1. Ee Mungu naomba uondoe tabia ya kifarisayo ndani yangu ya kujiona ni wa maana kuliko wengine.

2. Ee Mungu naomba uondoe tabia ya kujidanganya kwamba nimekuficha dhambi zangu kwa vile kwa kufanya hivyo ninalaani mafanikio yangu.

3. Ee Mungu naomba uondoe ibada ya sanamu ndani ya moyo wangu ili niweze kukuabudu Wewe peke Yako.

4. Ee Mungu naomba uondoe ubahili na uchoyo ndani yangu ili ninapolia unisikie.

5. Ee Mungu naomba uniwezeshe kuwasamehe wote walionikosea na nisiwe na uchungu na mtu yeyote moyoni mwangu

6. Ee Mungu naomba uniwezeshe kuomba maombi yenye kibali mbele zako ili nisipoteze muda wangu.

Naomba Mungu akusaidie kupitia ujumbe huu uijue dhambi yako na kuishinda ili ufikie kusudi la Mungu kwa ajili ya maisha yako.

Lawi Mshana, +255712-924234, Tanzania