Ticker

6/recent/ticker-posts

USIRUHUSU WATU WAKUPANGIE MAISHA. MUNGU ANATUMIA RASLIMALI ULIZO NAZO KUKUBARIKI.


USIRUHUSU WATU WAKUPANGIE MAISHA. MUNGU ANATUMIA RASLIMALI ULIZO NAZO KUKUBARIKI.

Watu wengi wamelemazwa na mfumo wa kutegemea elimu peke yake kwa ajili ya kufanikiwa kimaisha. Wanashindwa kuelewa kwamba kusudi la elimu sio kupata ajira peke yake bali ni kukuza uwezo wa kutawala mazingira. Ndiyo maana unaweza kuwa na elimu na uwe bado hujaelimika. Tulizoea kusema KNOWLEDGE IS POWER lakini tumegundua kwamba kuna watu wana ujuzi lakini hawautumii kubadilisha maisha yao. Hivyo sasa tunasema APPLIED KNOWLEDGE IS POWER tukimaanisha kwamba UJUZI UNAOTUMIWA UNAWEZA KUMPA MTU MATOKEO MAZURI

Napenda kukupa maswali ya kujihoji kibinafsi ili kukusaidia. Nitatumia maisha ya Musa ambaye alitumiwa na Mungu kuwatoa Wana wa Israeli katika utumwa na kisha kusafiri nao katika safari yenye upinzani mwingi. Itakusaidia kujua siri ya mafanikio yake.

1. Una kitu gani kilicho karibu na wewe?

Kutoka 4:2 “Bwana akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo.”

Mungu anatumia ulicho nacho kwa ajili ya kupata unachohitaji. Jigundue vizuri kwamba una nini ambacho Mungu anaweza kukitumia. Hata mwanamke mwenye madeni yasiyolipika alipomuendea nabii wa Mungu, aliulizwa ana nini nyumbani. 2 Wafalme 4:2 “Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.”

Unapomuambia Mungu kwamba huna chochote, maana yake umejiandaa KUFILISIKA. Hakuna mtu ambaye hana chochote mbele za Mungu. Mathayo 25:29 “Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.”

2. Una mtu gani karibu na wewe?

Kut 4:14 “Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake.”

Kuna watu wengi karibu na wewe ambao wangeweza kukusaidia pale ambapo huwezi. Hapa sizungumzii wafadhili wa kukupa pesa bali KUKUKAMILISHA katika kusudi la Mungu kwako. Musa alikuwa na wito lakini ana kigugumizi. Mungu akamwambia kwamba Haruni atakuwa msemaji wake. Sina uhakika kama unawajua vizuri majirani zako kazini, kanisani na nyumbani wanavyoweza kukuunganisha na fursa mbalimbali. Wewe unawajua tu kama wapendwa wa kushirikiana maombi ya kufunga! Mtambue Haruni wako leo wa kusaidia kigugumizi chako.

3. Una uzoefu gani?

Kutoka 2:10 “Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini.”

Musa alikuwa na uzoefu wa kulelewa na familia yake utotoni kama Muisraeli na kisha akalelewa kama mtoto wa mfalme wa Misri. Kwa hiyo alijua mengi kuhusu Ikulu ya Farao na watendaji wakuu walimfahamu. Usipuuzie uzoefu wowote ulio nao hata kama umeajiriwa na kupata mshahara. Mungu anaweza kutumia uzoefu wako kukupeleka mbali zaidi. Haingekuwa rahisi mtu tofauti na Musa kutumwa kwa Farao. Musa alijulikana Ikulu hivyo hawakuwa na maswali mengi juu yake.

4. Una elimu gani?

Matendo ya Mitume 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa maneno na matendo.”

Musa alifundishwa elimu yote ya Wamisri ikiwa ni pamoja na miungu yao. Ndiyo sababu Mungu akatumia muujiza wa fimbo kuwa nyoka. Unadhani ilikuwa rahisi kushika mkia wa nyoka. Kut 4:3,4 “Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake.)”

5. Una tabia gani?

Hesabu 12:3,7 “Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.”

Musa alikuwa na sifa ya upole na uaminifu. Hakuna mtu katika kipindi chake alimfikia katika tabia ya upole na uaminifu. Sijui wewe una tabia gani nzuri kushinda wengine ulio nao. Hata kama una shahada au karama kubwa hutaenda mbali kama una tabia mbaya. Tabia yako njema inaweza kukufungulia fursa nyingi. Jifunze kujali na kuheshimu watu hata kama huwajui na hawana cha kukupa.

USHUHUDA WANGU BINAFSI

Mungu amenisaidia mapema kugundua nina kitu gani tofauti na mambo niliyosomea. Vitu hivyo tofauti na elimu yangu rasmi vimeniwezesha kufanya makubwa zaidi na kuwafikia hata watu wa nchi za mbali. Mfano, kuna vitu nimefanya nikapata kipato bila kuwa na cheti chake kv kufundisha lugha, kufundisha kompyuta, kutafsiri, kuedit video, kuwezesha mada za kijamii kv UKIMWI, jinsia, afya ya uzazi nk.

Nimejitahidi sana kujua uwezo wa watu walio karibu na mimi na jinsi tunavyoweza kushirikiana. Unaweza kudhani mtu fulani anajua kufundisha tu kwa vile anaitwa mwalimu. Ukiwa karibu naye kimalengo utagundua kwamba kumbe pia ni daktari au mpishi mzuri sana.

Nina uzoefu wa kufanya kazi na watu wa dini na madhehebu mengi kiasi kwamba sipati shida kushirikiana na watu tofauti kwa yale ambayo yanatuunganisha bila kuathiri imani binafsi. Unapojali mambo yanayokutofautisha na wengine hutaweza kuishi hata na mkeo au mumeo maana mna tofauti nyingi za kimalezi, kielimu, kimaumbile nk.

Nimejitahidi sana kuhakikisha nasomea vitu ninavyotaka kufanya ili nivifanye kwa uhakika na kwa kujiamini zaidi. Mfano, nilisoma shahada ya uzamivu (udaktari) ya Theolojia na Menejimenti kwa miaka 10. Lakini nikasoma kozi mbalimbali kv Personnel Management (diploma), Project Management, Knowledge Management, HIV and Gender for Interfaith groups nk

Pia nimejifunza kwamba pesa zinapatikana ukiwa na tabia ya kujali wengine kuliko kujijali wewe mwenyewe. Nimewahi kujitolea kuhudumia vikundi vya watu wanaoishi na VVU kwa pesa yangu kidogo. Matokeo yake nikapata ruzuku kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) kwa ajili ya kufikia viongozi wa dini, wanawake na vijana. Wale niliowasaidia waliongeza wasifu wangu wa kuaminiwa pale walipoulizwa ni nani anawasaidia halafu wakanitaja. Huwezi kujua mtu unayemsaidia leo atakuwa nani kesho au anajuana na nani.

Maombi ya wiki hii

1. Ee Mungu naomba unifungue macho nigundue na kutumia raslimali zinazonizunguka kwa ajili ya kubadili maisha yangu.

2. Ee Mungu naomba uniongoze namna ninavyoweza kutumia elimu na uzoefu wangu katika kufikia hatua nyingine ya maisha yangu.

3. Ee Mungu naomba unipe moyo mwema wa kuthamini na kujali maisha ya wengine ili niwe mkono wako wa kuwabariki wengine.

Usisahau kwamba Mungu haleti baraka kwa ajili ya maisha yako mwenyewe. Anataka pia kukufanya baraka kwa wengine. Mwanzo 12:2 “nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka.” Ndiyo sababu tunagusa maisha ya wengine. Jiunge na group letu la USIMAMIZI WA MAJANGA NA UHATARISHI uwe sehemu ya mpango huu. 2 Wakorintho 8:4 “wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.” Bofya kiungo hiki (2) Vulnerability and Disaster Management (Kukabiliana na uhatarishi & majanga) | Facebook

Ushuhuda: Hivi karibuni kupitia shirika letu la Beyond Four Walls tumemsaidia kijana ambaye amekuwa akinyanyaswa kijinsia na mwanamke fulani kiasi cha kupigwa kama mtoto mdogo na kuchukuliwa mshahara wake wote. Tulimfikisha dawati la jinsia maana alikuwa hajui kuna taasisi ambazo zinawasaidia watu wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia. Ofisi yetu ya kujengea uwezo vijana na walezi/wazazi iko stendi mpya Korogwe chumba namba 84.

Lawi Mshana, 0712-924234.