TUSITAFUTE KUFANANA BALI KUKAMILISHANA
Saa 8 usiku wa
kuamkia Jumapili juzi nilipata ujumbe kwa ajili ya wachungaji nikaweza
kuushirikisha katika ibada ya pamoja ya madhehebu mbalimbali Jumapili hiyohiyo
jioni. Nimeona ni ujumbe unaoweza kukufaa pia wewe kama kiungo katika mwili wa
Kristo: Niliona niko na wachungaji nikasema maneno haya: “Kila mtu kati yetu ana kitu ambacho mwenzake hana. Tofauti zetu
zinakamilishana. Tusitafute kulingana wala kufanana bali kukamilishana. Nikawa
naongoza wachungaji kunyoosha na kukunja kiganja. Tukajifunza kwamba kiganja
kikikunjuliwa, vidole vinapishana sana urefu lakini tukikunja vidole vinaendana
kiasi kwamba tofauti hazionekani sana.” Huu ulikuwa ufunuo mpya kwangu.
Maana yake ni
kwamba: 1. Tofauti zinajitokeza zaidi au zinakuwa kubwa zaidi ukiwa peke yako
kuliko ukiwa na wenzako 2. Ingawa ukinyosha mkono dole gumba limezidiwa urefu
na vidole vyote, ndilo linategemewa kuongeza nguvu wakati wa kushika au kukunja
ngumi. 3. Vidole vidogo havipati sapoti ya dole gumba kama ilivyo kwa vidole
virefu pale unapokunja ngumi. Mungu alipanga vidole virefu visaidiwe zaidi
kuliko vidole vifupi. Vidole vifupi amevipa nguvu ya kutosha kujisimamia. Hata
mguuni kidole kidogo ndicho kinachokusaidia usianguke ovyo (kinakupa ‘balance’),
ingawa pengine hujawahi kukishukuru wala kujua kama ni cha muhimu kiasi hicho.
Kwa kifupi
tunajifunza kwamba TUNAHITAJIANA. Hivyo kila mmoja ajue ana nini na hana nini
na nani ana hicho asichokuwa nacho ili waweze kukamilishana. Hii ina maana
kwamba uhusiano wa mtumishi na mtumishi usiwe wa kukariri wala wa maeneo yote
bali yale ambayo wanaona kwamba wanakamilishana yaani kila mmoja anapata kitu
kwa mwenzake. Ukisoma 1 Kor 12 utaona jinsi mtume Paulo alivyotumia mfano wa
kulinganisha (analogy) kati ya watumishi na viungo vya mwili. Kila mmoja wetu
ni wa muhimu sana katika kuukamilisha mwili wa Kristo. Mdomo wako unauheshimu
sana maana unakuwezesha kula vitu vitamu. Na unaweza kuamua uunyamazishe usile chochote
kwa kipindi kirefu. Hata hivyo kuna kiungo ambacho hatuwezi kukitaja mbele za
watu na wala hatukiheshimu sana lakini kama kikiamua kugoma kufanya kazi yake
kwa muda mfupi tu unaweza kulia kama mtoto mdogo. Mungu atusaidie tuheshimu
viungo vyote katika mwili wa Kristo bila kujali vina heshima au havina.
Barikiwa na Bwana.
1 Kor 12:21-23 “Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.”
Lawi Mshana