USING’ANG’ANE KUPATA VITU AMBAVYO SIO
VYA KWAKO
Leo saa 10
usiku nikiwa jijini Dodoma nimepata ujumbe huu: Nimeona nikifundisha semina kanisani nikawa naonya kwa sauti kubwa
nikisema, “Using’ang’ane kupata vitu ambavyo sio vya kwako. Mtu mmoja akataka
nipunguze sauti ili watumishi wanaosoma chuo pembeni wasisikie bali waendelee
na darasa lao. Nikasema moyoni kwamba nashukuru wamesikia nilichosema.”
MAANA YAKE
1. Mungu
anasema kuna watu wa Mungu wanalazimisha kupata vitu ambavyo Mungu hajawapangia.
Biblia imetuagiza kwamba TUHAKIKI NI NINI IMPENDEZAYO BWANA. Waefeso 5:10 “mkihakiki ni nini impendezayo Bwana.” Rum
12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia
hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya
Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Kabla ya kufanya maombi ya
kung’ang’ana hakikisha kitu hicho ni mpango wa Mungu kwako. Mungu anafanya kazi
pamoja na watu wake kwa kuzingatia kusudi lake. Lazima ujue kusudi la Mungu
kwako kabla ya kutaka kufanya kazi PAMOJA na Mungu. Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote
Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa
kwa kusudi lake.”
Usimtumikie
Mungu kwa mazoea. Mfalme Daudi hakutumia kanuni hiyohiyo kwa nyakati tofauti.
Alitafuta mwongozo kwa kila aina ya vita na kupewa maelekezo tofauti. Siku moja
alipouliza kwamba aende kupigana Wafilisti na kama Mungu atawatia maadui zake
chini yake, alikubaliwa kupanda. 2 Sam 5:19 “Basi Daudi akauliza kwa Bwana, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti?
Utawatia mkononi mwangu? Naye Bwana akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika
nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Kipindi kingine akapewa mkakati
tofauti kwamba asipande bali azunguke nyuma yao ingawa maadui ni haohao. 2
Samweli 5:23 “Naye Daudi alipouliza kwa
Bwana, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi.”
Acha kumzoea Mungu katika utumishi wako kama unataka mafanikio.
2. Kuna
watumishi ambao wamenga’ng’ana na elimu kiasi kwamba hawampi Mungu nafasi ya
kuzungumza nao. Mungu anapewa nafasi kubwa kwenye SEMINA lakini anakosa nafasi
kwenye baadhi ya VYUO. Tusisahau kwamba kanisa la Laodikia lilijisahau kiasi
kwamba lilibaki kujiona lina utajiri wakati Bwana Yesu yuko nje ya kanisa.
Ilibidi aliambie kanisa hilo kwamba wamfungulie aingie maana hayuko ndani yao
ingawa ibada zilikuwa zinaendelea. (Ufu 3:14-22) “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya
kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na
kipofu, na uchi….Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu,
na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja
nami.” Usitegemee elimu hata kama ni ya Theolojia kuliko Mungu mwenyewe. Kuna
watumishi katika mji huu ambao wamemkataa Mungu katika fahamu zao. Warumi 1:28 “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu
zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.”
Elimu ni ya
muhimu sana maana hata mimi nimesoma shahada ya udaktari wa masuala ya
theolojia kwa miaka mingi (2002-2012) na hata kuja kwangu hapa Dom kipindi hiki
nimekuja kufanya maandalizi ya tathmini ya mahitaji ya jamii (needs assessment)
kwa ajili ya NGO yetu. Elimu ni ya muhimu sana. Hata Hivyo tuwe waangalifu
elimu yetu isitupe kiburi bali itupe unyenyekevu zaidi. 1 Kor 8:1 “…Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi
huleta majivuno, bali upendo hujenga.”
Tuna tabia ya
kunukuu na kutafsiri vibaya (misquote and misinterpret) maandiko ili
kuhalalisha au kutetea mambo tunayotaka kufanya (eisegesis) badala ya kuliacha
Neno lijisemee lenyewe na sisi kulifuata kama lilivyo (exegesis). Mfano, kwa
kila aina ya elimu tunapenda kusema, Biblia ilisema usimuache elimu aende zake.
Na kwa kila maarifa hata yasiyo na maana kwa Mungu, tunasema, Watu wanaangamia
kwa kukosa maarifa. Lakini swali la kujiuliza, Je ni kweli hiyo elimu na hayo
maarifa tunayotaka kuyasapoti kwa nukuu za maandiko yanakubaliana na Biblia Takatifu
au ni kinyume kabisa (out of context)?
Namaliza kwa
kusema, TUNAOMBA NA HATUJIBIWI KWA VILE TUNAOMBA KWA NIA MBAYA (WRONG MOTIVE). WAKATI
MWINGINE HUNA HITAJI HILO LAKINI UNATAKA KULAZIMISHA ILI TU UFANANE NA JIRANI
YAKO. LAKINI PIA HATUJIULIZI KAMA MUNGU ATAPATA UTUKUFU WOWOTE NDANI YAKE. Yakobo
4:3 “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa
tamaa zenu.”
Mungu akusaidie na kukurudisha kwenye mstari wewe ambaye leo Mungu amenipa ujumbe huu kwa ajili yako.
Lawi Mshana, 0712924234; Tanzania


