Mtetezi wako yu hai, hutaonewa tena!
Mwisho
wa kuonewa kwako umefika. Mungu amekuona. Kama ulikuwa unasikia tu watu
wakisimulia kwamba Mungu anaweza, SASA jicho lako mwenyewe litaona Mungu
akikupigania. Ayubu 42:5 “Nilikuwa
nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio; Bali sasa jicho langu
linakuona.”
Mungu
anasema nawe mambo yafuatayo:
1. Kilio chako kimefika
kwa Mungu
Mungu
amesikia kuugua kwako na amekumbuka agano lake alilokuwa amefanya kuhusu uzima
wako. Sasa sio tu kwamba anakuona, bali ANAKUANGALIA.
Kut
2:23-25 “Hata baada ya siku zile nyingi
mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa,
wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. Mungu
akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na
Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.”
2. Mungu anataka kuwa
mtetezi wako
Umekuwa
kama mtu asiye na mtetezi? Mungu anataka kukufuta machozi. Atashuka Mwenyewe
hadi hapo kwenye vita zako.
Zab
74:21,22 “Aliyeonewa asirejee ametiwa
haya, Mnyonge na mhitaji na walisifu jina lako. Ee Mungu, usimame, ujitetee
mwenyewe, Ukumbuke unavyotukanwa na mpumbavu mchana kutwa.” Mungu anataka
kutoka kwenye kiti chake mbinguni na kushuka hadi hapo ulipo ili akutetee. Ayubu
19:25 “Lakini mimi najua ya kuwa
Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.”
3. Utakuwa mbali na
kuonewa
Hakuna
kitu kitakachoweza kukutia hofu tena. Waliochezea maisha yako kwa muda mrefu
hutawaona tena. SASA utapata amani tele! Isaya 54:14 “Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana
hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.” Kutoka 14:13,14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni
tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona
leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”
4. Yesu alikuja duniani
kwa ajili ya watu wanaoonewa
Sasa
utajua kwamba Yesu hakuja duniani ili tu umuabudu bali alikuja pia kwa ajili ya
kukutoa katika uonevu wa shetani. Mdo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho
Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya
wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”
5. Mungu anataka kuwa
ngome na kimbilio lako.
Kuanzia
sasa hutawakimbilia wanadamu bali Mungu aliyekuleta duniani. Waliokuwa
wamekushika na kukufanya kama msukule, hawataweza kukushika tena. Bwana wa
majeshi ni Mkombozi wako. Zaburi 9:9 “Bwana
atakuwa ngome kwake aliyeonewa, Naam, ngome kwa nyakati za shida.” Yer
50:33-34 “Bwana wa majeshi asema hivi,
Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua
mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha. Mkombozi wao ni hodari; Bwana wa
majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi,
na kuwasumbua wakaao katika Babeli.”
Wiki hii mshukuru Mungu
hivi:
1.
Ee Mungu nakushukuru kwamba sasa sio tu kwamba unaiona bali umeniangalia kwa
karibu kama mtoto wako unayempenda.
2.
Ee Mungu nakushukuru kwamba umeamua
ushuke mwenyewe na kunitetea katika mappito yangu.
3.
Ee Mungu nakushukuru kwamba umewatowesha wote waliokuwa wanatishia maisha yangu
Hivyo amani yako itathibitika kwangu.
4.
Ee Mungu nakushukuru kwamba sitaendelea kuwa muumini aliyezoea kuonewa na
ibilisi bali sasa niko huru kabisa.
5.
Ee Mungu nakushukuru kwamba sasa WEWE ndiye kimbilio langu kwa hiyo sitaishi
tena kama mateka au msukule. Nitaona nikinufaika na kazi zangu
ninazozitaabikia.
Mungu
aione shukrani yako kwake wiki hii na kukupa thawabu ya majibu dhahiri katika
Jina la uweza la Yesu Kristo!
Lawi
Mshana, 0712-924234