Usiku wa kuamkia jana niliona nikimwambia mtu fulani hivi: “Pamoja na changamoto za ujauzito hakuna anayefurahia kujifungua baada ya miezi mitatu hata kama hali hiyo inamchosha kwa vile anataka matokeo mazuri.”
Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba mjamzito anapitia magumu mengi lakini anajua kwamba hawezi kupata matokeo mazuri kama hatafikisha miezi 9. Yuko tayari kupambana na changamoto za kula udongo, kuchukia mume wake, kula vyakula ambavyo awali hakuvipenda, kushindwa kufanya kazi zake vizuri nk. Kamwe hatamani muda wake wa kujifungua upungue kwa vile anataka matokeo mazuri.
Maana ya ujumbe huu ni kwamba tatizo lako kubwa sio umasikini au kupungukiwa pesa kama unavyodhani. Hata ukipata pesa hufanikiwi kwa kiwango kinachoendana na pesa zako. Tumeshuhudia hata wastaafu waliopata mamilioni ya pesa wakifilisika baada ya muda mfupi sana. Tatizo lako kubwa ni KUKOSA SUBIRA. Mipango yako mingi haina tofauti na mimba iliyotoka kabla ya wakati wake. Unawakemea wanaotoa mimba lakini hata wewe umetoa mimba nyingi za mipango yako iliyokuwa mizuri (aborted plans).
Hata Neno la Mungu linasema subira ndiyo itatuponya nafsi zetu. Luka 21:19 “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.” Hatutakuwa salama kama tutaendelea na hii tabia ya kulazimisha mambo ya miaka ijayo yafanyike leo wakati mambo ya mwaka huu hayajafanyika.
Ayubu alipoteza kila kitu kuanzia mali zake, watoto wake, afya yake na ndoa yake (maana hata mke alimshauri amkufuru Mungu ili afe haraka kuliko kuendelea kuuguza majipu). Hata marafiki zake walimhukumu kwamba ametenda dhambi fulani. Kilichomsaidia Ayubu katika mazingira hayo ni SUBIRA. Yakobo 5:11 “Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Subira ya Ayubu ilimfanya apokee baraka mara dufu baadaye. Ayu 42:10 “Kisha Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; Bwana naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.” Miongoni mwa baraka alizopata Ayubu ni mali nyingi na watoto wa kike wenye sura nzuri ajabu ambao aliamua kuwapa urithi bila ubaguzi wa kijinsia. Ayubu alitekeleza sheria hii bila shuruti miaka mingi sana iliyopita wakati sisi leo ndo tunaanza kutambua haki za mtoto wa kike. Ayu 42:15 “Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume.”
Hata Methali za Kiswahili zinathibitisha umuhimu wa kuwa na subira. Mfano, Subira yavuta kheri au haraka haraka haina baraka.
Mambo gani yanaashiria kwamba umekosa au kupungukiwa na subira?
1. Umechoka kutenda mema
Wagalatia 6:9 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.”
Kuna huduma nyingi ulikuwa unazifanya bila kusukumwa na sasa umeziacha. Tabia hii ya kuzimia roho imesababisha hupati mavuno katika maisha yako ya kiroho na kimwili. Kususia au kulipiza kisasi kwa kugoma kazi ya Mungu kutakugharimu sana kama hutachukua hatua kuanzia leo. Watendee watu mema bila kutafuta shukrani au upendeleo kutoka kwao. Tabia hii itakuongezea miaka ya uheri na furaha.
2. Hutaki kujifunza maisha ya aina zote
Wafilipi 4:12 “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.”
Mtume Paulo hakubabaishwa na njaa wala utajiri. Pesa nyingi au kupungukiwa havikumfanya amkosee Mungu. Sio dhambi kukopa ili mradi ukikopa ujue kwamba lazima utatakiwa kulipa deni. Wengi wataikosa mbingu kwa kutolipa madeni kwa vile hawajui andiko linavyotuonya. Zaburi 37:21 “Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu.” Hata hivyo wakati mwingine tunakopa kwa kukosa subira. Tunataka kumiliki kitu fulani leo ambacho Mungu alitaka tukimiliki mwaka ujao. Mwingine yuko tayari kuuza utu wake ili tu apate ajira. Anasahau kwamba wazazi waliomlea au majirani zake hawakuajiriwa lakini Mungu amewalisha hadi leo. Ridhika na vitu ulivyo navyo na wakati huohuo ukijituma kuyabadilisha maisha yako kwa kufanya kazi za halali. Usijilinganishe na mtu mwingine. Ishi maisha uliyopangiwa na Mungu na kuyafurahia. Furaha haitegemei mali ulizo nazo bali kuishi katika kusudi la Mungu kwako!
3. Unatafuta utajiri isivyo haki
Mithali 28:20 “Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.”
Unadhani kwamba raha yako duniani itatokana na kujilimbikizia mali za hapa duniani bila kujali kazi ya Mungu na watu wenye uhitaji. Matokeo yake unaishi kwa mashaka, upweke na huzuni ya moyo hata kama kwa nje unaonekana kama mtu aliyefanikiwa. Na baada ya maisha ya hapa duniani ndipo utagundua kwamba ulikuwa mpumbavu sana. Ulijiwekea akiba za duniani na kusahau kwamba kuna maisha mengine. Luka 12:20 “Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?”
Sisi pia tuna mahitaji mengi lakini tumegundua kwamba tusipojali maisha ya wengine hasa wanyonge tutaaibika baada ya maisha haya. Pengine ukisikia tunatoa misaada unadhani tuna pesa za ziada au tunajipendekeza. Leo nimekumbusha watu kanisani kwamba unapotoa nguo zako ambazo huzivai kwa sasa ili tuwasaidie wahitaji, unaandaa kupata thawabu yako mbinguni. Ukisubiri uondoke duniani kisha ndugu zako wagawane, hutapata thawabu tena. Kifaa chochote ulicho nacho ambacho hukitumii lakini kinafanya kazi unaweza kukitoa kisaidie jamii. Ukweli ni kwamba hatukuitwa kutoa huduma za kiroho peke yake. Tukiendelea kutoa huduma za kiroho peke yake na kusahau mahitaji ya wanyonge na wasiojiweza tunaweza kupoteza roho zetu. Jisomee mwenyewe andiko hili la Mathayo 25:41-46 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake. kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama. Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie? Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
4. Hutaki kuteseka kwa ajili ya Mungu
Ufu 14:12,13 “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu. Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.”
Pengine unasubiri kwamba kuna siku utakuwa na pesa za kutosha ndipo uanze kumtumikia Mungu. Kama Mungu ana shida ya pesa angemuokoa tajiri maarufu. Lakini amekuchagua wewe kwa vile WEWE NI ZAIDI YA PESA – UNA PUMZI NA ROHO WA MUNGU NDANI YAKO. Jifunze kumngoja Bwana kwa saburi atakuinua kwa wakati wake. Zaburi 40:1 “Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.” Yakobo 5:7 “Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho.” Usilazimishe ndoa wala mapenzi kabla ya wakati wake. Kilicho bora kwa ajili yako kinaandaliwa. Wimbo Ulio Bora 3:5 “…Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.”
Maombi ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba unihuishe tena kwa ajili ya kufanya kazi yako ili nikuzalie matunda ya kudumu.
2. Ee Mungu naomba unifundishe kuishi maisha ya aina zote uliyoruhusu kwangu ili nisitafute kuyabadilisha kwa maumivu.
3. Ee Mungu naomba unisaidie nitafute mafanikio kwa haki bila kudhulumu watu wala kusahau kwamba kuna kazi uliyonipa hapa duniani.
4. Ee Mungu naomba unifundishe kushiriki mateso kwa ajili yako ili baada ya maisha haya niingie katika raha ya milele.
Naomba Mungu akusaidie uwe na subira ili utafutaji wako wa kipato usikupeleke katika kujichoma kwa maumivu mengi. 1 Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”
Barikiwa na Bwana, mpendwa!
Lawi Mshana, 0712-924234; Tanzania