Mungu anataka kukurejeza katika ubora uliokuwa nao
Usiku
wa kuamkia jana niliona maneno haya:”RESTORATION, RESTORATION, RESTORATION.”
Maana ya RESTORATION ni UREJESHO. Kurejeshwa katika ubora uliokuwa nao awali.
Maana
yake: Ujumbe huu ni wa kwako wewe ambaye umepoteza hali yako ya kwanza. Shauku
yako imepotea, pesa zimepotea, amani imepotea, umepoteza furaha ya wokovu wako,
umepoteza upendo wako wa kwanza nk. Ufu 2:4 “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.”
Mungu anakwenda kukurudishia
furaha ya wokovu wako leo ili na wewe ucheke kuanzia moyoni. Zaburi 51:12 “Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.” Lakini pia Mungu anataka kukurudishia
miaka yako iliyopotea. Kuna matatizo mengi yamekula miaka yako lakini Mungu ni
mwaminifu. Yoeli 2:25 “Nami
nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na
tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.”
Hatua za kuchukua ili urejezwe
na Bwana:
1.
Funga saumu inayokubalika kwa Mungu
Usifunge ili kutimiza wajibu
tu. Maombi ya kufunga yana kanuni zake. Usilemee watu kazi kisa umefunga. Saumu
yako ikiwa sahihi, utakuwa baraka kwa wengi na utakarabati maeneo mengi
yaliyochoka badala ya kuyanyoshea kidole.
Isaya 58:6,12 “Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna
hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru
walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Na watu wako watapajenga mahali
palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye
kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.”
2.
Rudi kwa Bwana Mungu wako
Mungu anatafuta UKARIBU NA
WEWE (INTIMACY) kuliko utumishi wako kwake. Tafuta ushirika na Yeye kuliko
kumtumikia. Ukiwa karibu na Yeye utagundua anataka nini kwako. Kwa hiyo
hutafanya huduma ambazo hazina mguso kwake.
Yeremia 15:19 “Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi,
ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho
cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia
wewe, bali hutawarudia wao.”
Dada yetu Martha alidhani
anajua sana mahitaji ya Bwana Yesu. Hivyo Bwana alipofika numbani kwao hakumuuliza
chochote zaidi ya kukimbilia jikoni. Haikutosha kufanya hivyo bali alimlaumu
hata Bwana Yesu kwamba kwanini hamfukuzi Mariamu ili wasaidiane kuandaa
chakula. Luka 10:40-42 “Lakini Martha
alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni
vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie
anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika
kwa ajili ya vitu vingi;lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu
amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”
3.
Usipende kufanana na dunia hii
Chagua kuwa mwana wa mfalme
badala kuwa mtu wa dunia hii. Mathayo 13:38 “lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale
magugu ni wana wa yule mwovu.” Kumbuka hii dunia inapita na tamaa zake. 1 Yohana 2:17 “Na
dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.”
Huhitaji kuokoka roho peke
yake. Unahitaji pia mageuzi kwenye mtazamo wako (mindset). Mageuzi haya ni ya
KUFANYWA UPYA. Warumi 12:2 “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Mruhusu Roho Mtakatifu akufanye upya katika utu wa ndani ndipo hutalegea katika
maisha yako. 2 Wakorintho 4:16 “Kwa hiyo
hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani
unafanywa upya siku kwa siku.” Tito 3:5 “si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema
yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu.”
TAHADHARI
Hata hivyo ukitenda dhambi kwa
makusudi unaweza kufikia hatua hutengenezeki tena. Unafikia hatua ambayo mahubiri
hayakuchomi tena katika moyo wako. Badala yake yanateleza tu juu ya moyo wako
kama kama maji yanavyoteleza kwenye mawe ya mtoni. Haya mawe ya mtoni hayana
maji ndani ila yamechongwa kwa nje kiasi kwamba yanafaa tu kusugulia miguu. Usijifariji
kwamba utatubu wakati unakaribia kufa. Hakuna uhakika kama toba za aina hii
zote zinakubaliwa. Hebu soma maandiko haya:
Waebrania 6:6 “wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani
kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya
pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.”
Waebrania 10:26,27 “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.”
Maombi ya wiki hii:
1.
Ee Mungu naomba uondoe maombi ya kufunga ya mazoea ili nipate majibu yanayotia
moyo.
2.
Ee Mungu naomba uniwezeshe kutambua thamani ya kuwa karibu na wewe ilivyo kubwa
kuliko kupata vitu kutoka kwako.
3.
Ee Mungu naomba unitengeneze niwe mwana wa ufalme wako ili nisikimbizane tena
na dunia hii inayopita na tamaa zake.
Lawi
Mshana, 0712-924234