Ticker

6/recent/ticker-posts

HAKIKISHA SIKU YA HUKUMU UNA MAJIBU YA MASWALI KUHUSU CHRISTMAS


HAKIKISHA SIKU YA HUKUMU UNA MAJIBU YA MASWALI KUHUSU CHRISTMAS

Christmas ni moja ya sikukuu kubwa ambazo zinasherehekewa duniani bila maswali yoyote. Hata hivyo kwa waungwana kama watu wa Beroya wanatakiwa KUHOJI kila jambo wanalolifanya wakijua kuna siku tutahukumiwa bila kujali katiba zetu, madhehebu yetu, maaskofu wetu nk.

 Mdo 17:11 “Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.” Kila mmoja wetu, mdogo kwa mkubwa atasimama mwenyewe mbele za Mungu. Ufunuo wa Yohana 20:12 “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.”

Hapa kuna maswali ya kujihoji na kuhakikisha una majibu yake siku ukiulizwa. Usigombane na ujumbe huu bali ubaki na majibu yako hadi siku ya hukumu.

1.     Je neno Christmas (Christ-mass) lenye maana ya misa ya Kristo/komunyo lina maana hiyohiyo ya kuzaliwa (birthday) kwa Yesu Kristo?

2.     Kwa nini Christmas haikusherehekewa kipindi cha Biblia kama ilivyo Pasaka hadi mwaka 325 ndipo ikaanzishwa na kisha Wakristo waliotaka kulitakasa Kanisa wakaipiga marufuku kati ya  mwaka 1659 na 1681?

3.     Kwanini hata wasiomtambua Yesu kama Kristo na wanaotukana wokovu aliouleta Yesu wanasherehekea Christmas? Mtu anawezaje kusherehekea siku ya kuzaliwa (birthday) ya mtu asiyempenda wala kumuamini na anayemkejeli?

4.     Kwanini mara nyingi mazingira ya sikukuu ya Christmas yanakuwa hatarishi kama ilivyokuwa sikukuu ya Saturnalia mpaka polisi waimarishe ulinzi? Wiki la Saturnalia tarehe 17-25 Desemba watu waliruhusiwa kufanya maovu bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Mahakama zilifungwa wiki hiyo. Katika karne ya 4 wapagani wengi walisherehekea Krismasi kwa kuahidiwa kwamba wataendelea kusherehekea Saturnalia kama wakristo.

5.     Father Christmas au Santa Claus (mwenye nguo nyekundu na ndevu nyeupe) ana uhusiano gani na kuzaliwa kwa Yesu wa Biblia? Bwana Yesu anajisikiaje anapoona inatajwa kama siku yake halafu picha ya father Christmas ndiyo inayotangazwa zaidi. Tunajua vizuri amri ya kwanza na ya pili? Kut 20:3,4 Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

6.     Mti wa Christmas una uhusiano gani na historia ya kuzaliwa kwa Yesu katika maandiko? Haufanani na kile kinachosemwa kwenye Yer 10:2-4 “Bwana asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka. Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike,”

7.     Je tarehe ya Christmas inashabihiana na msimu ambapo wachungaji wa nchi ya Israeli wanakuwa makondeni usiku wakichunga? Kwanini iliangukia tarehe ileile ya kuzaliwa kwa mithras, mungu jua?

 

Wagalatia 6:4 “Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.”

 

Ufu 22:18,19 “Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”

 

Jiridhidhishe na yale unayofanya katika maisha yako bila kutegemea mapokeo ambayo hayana maandiko ya kuthibitisha ukweli wake.

 

Narudia tena kwamba USIGOMBANE NA UJUMBE HUU bali jiridhishe tu kwamba unayofanya yako kimaandiko au kimapokeo. Tumpe Mungu utukufu wake na tusimdhalilishe kwa sababu tu kila mtu anafanya jambo fulani. Kipindi cha Nuhu watu 8 waliokolewa na gharika, Misri wanaume laki 6 (takriban milioni 3 pamoja na wanawake na watoto) walitolewa katika utumwa lakini waliofika Kanani ni wawili tu (pamoja na waliozaliwa njiani). Mungu hajali idadi bali utii Kwake. Kwa maneno yake Yesu mwenyewe amesema, WATAKAOIONA NJIA IENDAYO UZIMANI NI WACHACHE NA SIO WENGI. Mathayo 7:14 Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.

 

Tumegundua hili baada ya kuamua kusoma maandiko kwa miwani ya Mungu badala ya miwani ya mapokeo na kidini. Si rahisi kila mtu kuelewa hili lakini tukisoma maandiko bila misimamo binafsi (kuwa na open mind) ndipo tutaelewa bila kujali watu wanasemaje.