Ticker

6/recent/ticker-posts

UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


 UZINDUZI WA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


Nimeweza kushiriki uzinduzi wa kampeni hii kwa mkoa wa Dodoma iliyofanyika uwanja wa Nyerere square, Jijini Dodoma kwa vile shirika letu limefungua ofisi katika kata mojawapo ya jijini Dodoma.

Mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma ambapo alisema kwamba asilimia 60 ya vitendo vya ukatili vinafanyika majumbani kwa maana kwamba vinafanywa na ndugu wa karibu. Jamii inahitaji kupewa elimu na kuweza kutoa taarifa na hatua za kisheria zichukuliwe bila upendeleo wowote. Athari za vitendo vya ukatili wa kijinsia ni nyingi ikiwa ni pamoja na mimba zisizotarajiwa, ulemavu, maambukizi ya UKIMWI na magonjwa ya ngono, matatizo ya kisaikolojia, hofu, kutafuta faraja kwa makundi hatarishi, kuacha shule na chuki. Watoto wanahitaji kujengewa uwezo katika kupinga ukatili kwa kutambua viashiria ili waweze kuripoti kwa wakati. Watendaji nao wanatakiwa kuwa na mfumo rafiki na wa haraka katika kutoa huduma na kushughulikia matatizo hayo.

Tuko katika hatua za mwisho za kukamilisha ripoti yetu ya tathmini ya awali (needs assessment) kwa ajili ya kata tuliyochagua kufanya kazi ambapo tumegundua kwamba ukatili wa kijinsia kwa watoto uko zaidi majumbani na njiani wakitoka na kwenda shule. Lakini pia upo mashuleni ingawa si kwa kiwango kikubwa.

Tunahitaji sana ushirikiano wako wa hali na mali ili tuwanusuru watoto na vijana katika uhatarishi huu maana baadhi ya watoto walitaja katika tathmini yetu kuwa wanabakwa na kulawitiwa na ndugu wa karibu na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa.

Dr Lawi Mshana, Mkurugenzi Mtendaji, Beyond Four Walls