MATENDO MAKUU
YA MUNGU KATIKA UZINDUZI RASMI WA MAOMBEZI YA NYUMBA KWA NYUMBA
Leo nimeanza
rasmi kufanya huduma za maombezi katika nyumba ninazoalikwa. Nimeona uhitaji
mkubwa pale watu watano walipolipuka mapepo. Majirani walishiriki kwa ajili ya
maombezi ya afya na upenyo wa kiuchumi. Kesho saa 10.30 jioni tumetenga muda
maalum kwa ajili yao ili kubomoa madhabahu zilizokuwa zimewashikilia hao ambao
mapepo yalijidhihirisha pamoja na wahitaji wengine.
Matatizo mengi
hayaishi kwa vile hatuchukui muda wa kutosha kutambua yalivyoanza na mabadiliko
yanayotokea. Tusiwalazimishe watu kukiri ushindi hasa pale ambapo hakuna dalili
zozote za uponyaji.
Ingawa Yesu
aliponya kimuujiza, kuna siku alimfungua mtu kwa mchakato na sio papo kwa papo.
Mk 8:22-26 “22 Wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. 23 Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu? 24 Akatazama juu, akasema, Naona watu kama miti, inakwenda. 25 Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. 26 Akampeleka nyumbani kwake, akisema, Hata kijijini usiingie.”
Mchakato ulikuwa hivi:
1. Alimtoa nje ya chanzo cha matatizo yake – kuna watu wanahitaji kuombewa
mbali na nyumba zao kutokana na maagano yaliyopo hapo. Vinginevyo, tatizo
litarudi haraka.
2. Alipomwekea mikono alimuuliza kama anaona kitu – alitaka
kujua kama kuna mabadiliko yameanza. Mtu anapowekewa mikono anapaswa kusema
anavyojisikia ili mwombaji ajue anatakiwa kuombaje zaidi.
3. Alisema uhalisia kwamba anaona nusunusu (maruerue) –
hakuna haja ya kukiri umepona wakati maumivu yanaendelea. Sema ili uombewe
zaidi. Hata hivyo mwambie shetani kwa kupigwa kwake Yesu wewe umepona. Ila
waombaji waeleze uhalisia.
4. Yesu aliweka tena mikono yake – kutokana na maelezo yake
kwamba hajafunguliwa vizuri, Yesu aliweka mikono yake TENA.
5. Akatazama sana (akakaza macho) – mtu anapoombewa
aonyeshe bidii ya kufanya alichokuwa hawezi. Kwa kufanya hivyo, atasababisha
muujiza utokee na kutambua kama ameshapona.
6. Yesu akampeleka nyumbani kwake na kumzuia kurudi kijijini kwake – agano la shetani katika kijiji chake lingeweza kumsumbua kama hajaimarika zaidi. Kama hospitalini wanavyomlaza mtu, hata katika huduma kuna watu wanatakiwa kuzuiwa kurudi nyumbani hadi wakati fulani.
Tuombee ili huduma hii iwaguse wengi bila kujali wanaabudu au la kwa vile Mungu ana mpango na kila mtu aliyemuumba. Ni gharama kuwafikia lakini kwa maombi yako tutaweza kuwafikia bila kuwachangisha pesa.
Lawi Mshana, 0712-924234