TUSIWE WATUMWA WA MADENI SABABU YA SHEREHE (Bofya hapa uangalie video)
TUSIWE
WATUMWA WA MADENI SABABU YA SHEREHE
Ndoto: Hivi karibuni nimeona waumini wakionywa kwamba
waepuke kuwa watumwa wa madeni kwa sababu ya sherehe.
Tumefika wakati ambapo sherehe zimeanza kupoteza lengo
lake. Zimeanza kuwa mzigo badala ya kuwa baraka. Watu wanakopa kwa ajili ya
kufurahisha watu na kisha wanajikuta ni watumwa wa madeni. Wengine wanauza
zawadi walizopewa kwenye harusi.
Mambo ya msingi kuzingatiwa na wacha Mungu katika sherehe
kwa mujibu wa Neno la Mungu:
1 Pet 4:2-5 “2 Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. 3 Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali; 4 mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. 5 Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.”
Ufafanuzi kuhusu huu ujumbe wa mtume Petro:
1. Kuacha
mapokeo ambayo yanapingana na Neno la Mungu – kwa vile mmeanza safari ya kiroho
msiishi kama zamani kabla hamjaamini – zamani mlienenda katika ufisadi (lewdness) – matendo ya zinaa/kingono
kv kuangalia watu ambao wako nusu uchi, kuvaa nusu uchi nk;
tamaa
(lusts) –
tamaa mbaya za mwili (kuwashana tamaa),
ulevi – watu wanajumuika
wakiwa wamelewa
karamu za
ulafi
– kufanya mambo ambayo si ya msingi. Mtu anakodi gauni laki 2-5 lakini hana
chakula cha wiki moja.
vileo (drinking parties) na
ibada ya sanamu isiyo halali (abominable idolatries) – kumtukuza mwanadamu badala ya Mungu. Mungu hapewi nafasi sherehe nzima.
Je hatujiulizi kwamba katika kumbi za sherehe nyingi tunalazimishwa kucheza dansi (miziki ya dunia yenye matusi), tunachangia pombe hata kama hatunywi, zinavaliwa nguo za makahaba (mtu huyohuyo aliyevaa vizuri kanisani, ukumbini anakuwa nusu uchi). Unadhani hatunajisiki katika mazingira hayo? Au ni mpaka mahali paitwe baa tu?
2. Kuwa tayari kutukanwa tunapoepuka ufisadi huo – mst 4 “mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana.”
Wasiomjua Mungu watakushangaa na kukutukana – Neno limesema wazi. Kwamba hutapongezwa bali utatengwa.
3. Wanaopinga msimamo wako watahukumiwa siku ya mwisho – mst 5 “Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.”
Kitendo cha kukupinga hakitawaacha salama siku ya hukumu.
Sasa ufanyeje kama mtu wa Mungu:
1. Changia na kushiriki sherehe ambayo utapata shangwe ya
moyo na sio maumivu na kulemewa.
Esta 8:17 “Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote
palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe,
karamu na sikukuu.”
2. Usiishi kwa kuwaogopa wanadamu. Mwogope Mungu na
kuisimamia imani yako.
Mithali 29:25 “Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali
amtumainiye Bwana atakuwa salama.”
3. Fanya sherehe za kiwango chako na maadili yako na
kuwajulisha watu mapema.
Warumi 12:16 “Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie
yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa
kujivunia akili.”
Ukichangisha kila mtu itabidi naye akuchangishe hata kama
ya kwake haina maadili kama ya kwako. Huna sababu za kukopa kwa ajili ya sherehe.
4. Usifanye sherehe ambazo unawaalika waliokuchangia tu –
kama unataka thawabu
Luka 14:12-14 “Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo
chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala
jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata
malipo.Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa
heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa
wenye haki.”
Kuna watu wengi wametoa mchango katika maisha yako kiasi
kwamba huwezi kuwaacha kwa sababu tu hawakuchangia fedha. Chakula kizuri ni
kile ambacho umemuandalia mgeni bila yeye kuchangia.
5. Epuka wanakamati na viongozi ambao hawatambui wala kuheshimu
imani na maadili yako. Amosi 3:3 “Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja,
wasipokuwa wamepatana?”
6. Epuka sherehe zinazoweza kukutoa kafara
Kutoka 34:15 “Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu
wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja
akakuita, ukaila sadaka yake.”
Maombi
ya wiki hii:
1. Ee Mungu naomba unipe ujasiri wa kukataa mapokeo
yanayopingana na Neno lako hata kama nitatengwa na dunia.
2. Ee Mungu naomba uniwezeshe kutambua kiwango cha maisha
ulichonipangia ili nisishindane na watu waovu.
UNAWEZA KUWASILIANA NAMI KWA MAOMBI NA USHAURI KWA SIMU NAMBA 0712-924234