TUMEKUWA WAPOKEAJI KWA MUDA MREFU, SASA NA SISI TUBARIKI WENGINE
Tunashukuru kwa
mara nyingine tumepokea nguo (suruali na mashati) kutoka kwa mpendwa kutoka
Singida. Nikuhakikishie kwamba umepanda kwenye udongo wenye rutuba. Nguo hizi
zitavaliwa na watu ambao huwajui kwa hiyo thawabu yako itakuwa kubwa zaidi
mbinguni. Wengi wetu tunasaidia zaidi watu tunaowajua na wanaotupa asante, kwa
hiyo thawabu yetu tunaipata hapahapa duniani. Hakuna mtu atapata thawabu
mbinguni kwa kitu ambacho dunia ilishamlipa. Mathayo 6:1 “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao;
kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.”
Mpendwa
uliyeguswa kutoa msaada huu, Mungu atimize mahitaji yote uliyoorodhesha kwamba
unahitaji Mungu akutendee kwa sababu Neno limesema anabarikiwa (ni heri) anayetoa
kuliko anayepokea.” Mdo 20:35 “Katika
mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia
wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni
heri kutoa kuliko kupokea.”
Nilipoenda nchi
fulani kufundisha viongozi wa dini takriban 40 hivi na kuwahudumia chakula cha
mchana. Mchungaji Mtanzania anayeishi nchi hiyo aliniambia jambo hilo
limewagusa sana kwa vile linafanywa na wahubiri wazungu tu. Nimejifunza kwamba
hatushindwi kuhudumia watu kama tungepiga mahesabu ya sherehe tunazochangia kwa
mwaka. Wazungu wanafanya mengi kwa vile wengi wao sherehe sio za lazima.
Wanapoona tunafanya sherehe za kifahari wanadhani zimeandaliwa na matajiri wakubwa
sana. Kumbe nyingi ni za watu maskini ambao sherehe ni kipaumbele kikubwa kwetu
kuliko hata kusomesha watoto.
Lakini pia
wengine wanapoona naenda kuhubiri nchi zingine wanadhani ni kama kwenda
kutalii. Hawajui ugumu wa huduma za kimisheni. Nilienda nchi fulani nikafika
katika kijiji ambacho nililala mazingira ya shida ambayo sijawahi kulala katika
mazingira kama hayo kwa hapa kwetu na mboga niliyoandaliwa ilikuwa ni panya na
sijawahi kumla. Unapochangia huduma hii unawezesha usafiri pamoja na kuwalisha
chakula washiriki ili walengwa wa hali zote wafikiwe.
Tangazo
Napenda
kuwakumbusha vijana wenye umri wa miaka 18-35 wenye ujuzi, uzoefu na ndoto
fulani wajitambulishe ili kupitia ofisi yetu ya kujenga uwezo (empowerment
office) chini ya Beyond Four Walls, tuwaunganishwe na fursa zinapojitokeza.
Hakuna mtu ataota kwamba kijana fulani ana elimu fulani, utayari fulani, maono
fulani na anapatikana katika mji au kijiji fulani. Nakumbuka tulipata tabu
kupata vijana wa kujitolea wenye ujuzi fulani tulipokuwa tunafanya tathmini ya
awali kwa vile hakuna mahali maalum pa kuwapata. Hapa tunajali ujuzi rasmi na
usio rasmi. Kuna vijana wanaweza kufanya mambo mengi ingawa hawana vyeti vya
mambo hayo. Kwa hiyo sisi tunahitaji kutambua wasifu wa kijana kwa ujuzi wake rasmi
na usio rasmi kuanzia waliomaliza darasa la saba hadi chuo kikuu.
Lakini pia
tunahitaji kufahamu taasisi zinazohitaji kutambulisha fursa walizo nazo na
masharti yao kwa ajili ya vijana ili mradi taasisi hizo ziwe zinafanya kazi za
halali, zinatambuliwa na serikali yetu na zinafanya kazi kwa mujibu wa
sheria.
Dr Lawi Mshana,
0712-924234 (Simu na Whatsapp)


