Ticker

6/recent/ticker-posts

Wewe ni yupi katika hawa?


WEWE NI YUPI KATIKA HAWA?

Lk 23:26-28, 39-43  “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.  27 Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.  28 Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. 39 Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.  40 Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? 41 Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.  42 Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. 43 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

Leo wakati naandaa ujumbe wa Ijumaa Kuu, Roho Mtakatifu alisema name kipekee kuhusu andiko hili.

Kuna aina kadhaa ya watu ambao tunafanana nao bila kujua:

1. Simoni Mkirene – alilazimishwa kubeba msalaba wa Yesu.

Huyu ni yule mtu ambaye hajui maana ya msalaba wa Yesu ila anabebeshwa tu majukumu na watu wengine. Anaweza kufanya huduma nyingi za kidini lakini hata Yesu hamjui. Inawezekana huyu Mkirene alipofika mahali fulani aliachiwa akarudi nyumbani kwake bila kuomba rehema kwa Yesu. Hakujua Yesu ni nani ingawa alibebeshwa msalaba wake. Tafuta kwanza uhusiano na Yesu kabla ya kuamua kumtumikia.

2. Wanawake - Hawa walimlilia Yesu kwa uchungu sana. Walijiona kama watu waliofiwa na mpendwa wao.

Tunao Wakristo ambao wanachukulia kufa kwa Yesu kwa tafsiri ya kumuonea huruma badala ya kujionea huruma. Wakitazama hata igizo la maisha ya Yesu wanalia sana wakiona anapigiliwa misumari. Hawajui kwamba kufa kwa Yesu ni kwa ajili yao ili waokolewe. Unaweza kumkuta mtu analaumu sana Wayahudi kwa kumuua Yesu, lakini hataki kuokoka. Yesu aliwaambia wale wanawake kwamba laiti wangejua kwamba Yeye amemaliza kazi yake, sasa kazi ni kwao na watoto wao.

3. Mhalifu aliyemtukana Yesu msalabani – Watu wengi wanamlaumu huyu mtu lakini wanafanana naye. Alisema hivi, “Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Kimsingi alimtambua Yesu kama mtenda miujiza ambaye angeweza kumsaidia kushinda changamoto za duniani tu. Tuna watu wengi wanaomtafuta Mungu ili tu waponywe, wapewe pesa, wapate mwenzi mzuri nk lakini sio kwa ajili ya roho zao kuokolewa. Kufanya hivyo ni kumtukana Kristo kwa vile hilo sio kusudi lake kuu.

4. Mhalifu aliyeomba Yesu amkumbuke Paradiso – Huyu mtu alimtambua Yesu kama Mwokozi ingawa alikuwa hajaokoka au alikuwa mtenda maovu. Hivyo hakuishia tu kumsifia kwamba alikuwa mwema (“huyu hakutenda lo lote lisilofaa.”) Bali aliongeza jambo la msingi sana, alimgeukia Yesu na kumwambia, “Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Hapohapo Yesu akamuahidi kuwa atakuwa pamoja naye Paradiso. Kumtambua Yesu kama mtu mwema hakutoshi. Mgeukie na kumpa nafasi katika moyo wako.

Mhalifu wa kwanza anawakilisha wale watu ambao wanampenda Mungu kwa ajili ya mafanikio ya maisha ya hapa duniani tu. Na mhalifu wa pili anawakilisha wale watu ambao wanampenda Mungu kwa ajili ya umilele wao. Huyu wa pili alisoma vizuri nyakati akawaza ufalme ujao na kuomba usajili na kweli akasajiliwa bila kupitia mchakato wa Kikanisa uliozoeleka.

Mungu akujalie kujitambua kwamba wewe unafanana na yupi katika watu hawa na kisha uchukue hatua zinazostahili.

Barikiwa na Bwana.

Dr. Lawi Mshana, 0712-924234, Tanzania