MAFUNZO MAALUM KWA AJILI YA WAZAZI NA WALEZI
Ni ukweli usiopingika kwamba wazazi ndio walezi wakuu (primary
caregivers) wa watoto. Na wajibu huu wamepewa na Mungu mwenyewe. Kinyume chake tumeanza
kuhamishia wajibu huu kwa watu wengine ambao walitakiwa tu kuunga mkono juhudi
zetu. Kwa bahati mbaya wapo wazazi wanaodhani kuwa wajibu wa kulea watoto wao
ni wa mabinti wa kazi (house girls), walimu wa watoto katika nyumba za ibada,
walimu wa shule au hata shangazi na bibi. Wengine wameenda mbali zaidi
wanadhani ni kazi ya serikali kuwalea watoto wao waliowazaa wenyewe na wengine
wameamua wamuachie Mungu kana kwamba watoto wao walianguka kutoka mbinguni.
Tunataka kuwarudisha wazazi kwenye misingi. Tumeanza na mada
ya kujadili namna tulivyolelewa na jinsi hali hiyo inavyoathiri namna tunavyowalea
watoto wetu leo. Tulijifunza aina za uleaji (parenting styles) tukagundua
kwamba tuna mapungufu makubwa. Kuna vitu vingi watoto wanavikosa kwetu na ndiyo
maana wanageukia mitandao ya jamii na watu mbadala ili wawasaidie. Matokeo yake
wakiharibika tunalaumu utandawazi wakati hatujawahi kuwapa malezi yoyote. Tunadhani
tukiwapa chakula na kulipa ada za shule kwa uaminifu tumeshawalea tayari.
Hata maandiko yanasema kwamba maisha ya mtu kuanzia utoto hadi
uzee wake yanategemea alilelewaje na sio tu alivyoombewa au kusomeshwa shule. Mithali
22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”
Watoto wa wanyama wakishazaliwa tu wanaanza kujitegemea kwa vile
Mungu hakuwapa wanyama akili ya kulea kama sisi. Watoto wetu wanachukua muda
mrefu sana kwa vile tuna wajibu wa kuwasaidia wawe watu wenye tabia fulani. Huwezi
kuwafanya watoto wawe tofauti na wewe (labda Mungu mwenyewe aingilie kati).
Tenda yale unayotaka watoto wako wayaige. Usijidanganye kwa kuwaambia, “fanyeni
yale ninayosema, msiangalie matendo yangu.” Kanuni ya kupanda na kuvuna inasema
kila mti utazaa matunda yanayofanana na mti wenyewe. Mwanzo 1:12 “Nchi ikatoa
majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake
zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.”
Mpango huu utawafikia pia walimu, wahudumu wa afya na
viongozi wa dini kadiri tutakavyopata raslimali za kuwafikia.
Mlango uko wazi wa kushirikiana na wadau mbalimbali wenye
shauku ya kuona familia zikiwa imara kwa ajili ya taifa zima.
Dr Lawi Mshana, Beyond Four Walls, +255 712924234