HATIMAYE NIKO BURUNDI KWA SEMINA. UNAJUA SADAKA YAKO IMEFANYA NINI?
Bilashaka baadhi yenu mliona tangazo langu mtandaoni la nia ya kufika DRC Congo na Burundi kwa ajili ya kujenga ufalme wa Mungu. Tumeeneza dini kwa muda mrefu. Sasa tujenge ufalme wa Mungu kwa kuwafikia watumishi bila hata kuuliza madhehebu yao.
Baadhi yenu mlichangia huduma hii. Pamoja na kwamba kwa kipindi hiki sitaweza kufika RDC Congo, hata hivyo nimeweza kufika Burundi. Hapa niko na mwenyeji wangu aliyenipokea ambaye nilikuwa sifahamiani naye na tumekutana leo kwa mara ya kwanza.
Sadaka yako imeniwezesha kufika nikiwa na nguvu ya kuanza huduma bila kuhitaji kupumzika kwanza kwa vile nilisafiri kwa ndege nikapunguza urefu wa safari. Lakini pia sadaka yako itawezesha siku moja kukutana na wachungaji na maaskofu kutoka madhehebu tofautitofauti ambapo watapata huduma ya Neno la Mungu tangu asubuhi pamoja na chakula na nauli.
Naamini siku ya kuvikwa taji utashangaa ukiambiwa kwamba uliwahi kumhudumia mchungaji wa Burundi. Pengine utasema mbona sijawahi kufika huko. Bwana atasema, 'Bila sadaka yako ujumbe muhimu haungemfikia mtumishi wangu wa Burundi.'
Nia yangu ni kufanyia kazi Agizo Kuu la kuanzia Yerusalemu hadi
mwisho wa nchi. Kwa muda mrefu tunafundisha Agizo Kuu kwa maneno lakini kwa
vitendo tumeamua kuishia Yerusalemu.
Nilianzisha mkakati wa kufikia hizi nchi zinazotuzunguka kwa kujipanga kibinafsi, kumuomba Mungu na kushirikisha wenye mzigo wa utume huu. Huwa naamini Mungu atanifanikisha nikiwa MWOMBAJI na sio OMBAOMBA. Nawashirikisha watu kama fursa tu ya kumtolea na sio kuwalemea. Kama wengine wanahamasisha sherehe na wanafanikiwa, hata mimi nitaweza kuwafikia wasiofikiwa kimkakati. Mungu aliyeniwezesha kufikia watumishi wa Malawi na Zambia ataniwezesha kwa nchi zingine pia.
Mungu akubariki sana kwa kuchagua fungu jema.
Dr. Lawi Mshana


