Semina hii imebebwa na kichwa kinachosema POKEA MWELEKEO
MPYA WA MAISHA ambapo andiko la msingi ni Kum 2:3 “Mlivyouzunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini.” Pengine
hata wewe umezunguka milima kwa muda mrefu. Sasa Mungu anataka upige hatua
kuelekea mbele kwenye hatima yako.
Maisha ya watu wa Mungu wengi yamekuwa duni kwa vile
wanajali roho zao tu na kusahau nafsi zao. Matokeo yake tunakuwa na watu waliojitakasa
vizuri rohoni lakini maisha yao kiuchumi hayana mwelekeo. Katika ‘nafsi’ ndipo
kuna KUHISI, KUFIKIRI NA KUAMUA. Hivyo mtu anaweza kuwa mzuri katika huduma za
kiroho (rohoni) lakini anafanya maamuzi mabaya katika maisha yake na kujikuta
akiwabebesha wengine lawama kwa matatizo aliyoyasababisha mwenyewe. Hata kama
uko vizuri kiroho, lazima UGEUZWE NA KUFANYWA UPYA NIA (MINDSET) YAKO ndipo
utajua vizuri mapenzi ya Mungu kuhusu maisha yako. Rum 12:2 “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Lakini
pia wengi wanaotaka baraka za Mungu hawamtumikii Mungu kwa lolote. Hivyo
mafanikio yao yanategemea juhudi zao tu bila mkono wa Mungu (God’s favour). Mafanikio
kutoka kwa Mungu yanahitaji mtu awe ANAMSIKIA NA KUMTUMIKIA MUNGU. Yaani,
asikie Mungu anamtaka afanye nini leo na awe na huduma fulani anayofanya kwa
ajili ya Mungu. Ayubu 36:11 anasema hivi “Kama wakisikia na kumtumikia, Watapisha siku zao katika
kufanikiwa, Na miaka yao katika furaha.”
Hata
hivyo mtu anatakiwa ajiridhishe kama kweli anamtumikia Mungu na sio dini peke
yake. Unaweza kuhatarisha maisha yako katika dini au dhehebu wakati hatari hizo
hazina uhusiano wowote na wito wako wala Ufalme wa Mungu. Kuna tofauti ya kufia
dini au dhehebu na kufa kwa ajili ya Kristo (kuwa shahidi Wake). Mdo 1:8 “Lakini mtapokea
nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu
katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Barikiwa na Bwana
Dr. Lawi Mshana, +255712924234, Tanzania