LEO VIONGOZI WA MADHEHEBU TOFAUTI WAMESHIRIKI MAFUNZO HAPA BURUNDI
Pamoja na mvua nyingi na majukumu mengi ya viongozi
wa makanisa hasa siku za Jumamosi, bado wamejitahidi kushiriki. Wametamani
kipindi kingine tuwape fursa wengi zaidi kushiriki mafunzo kama haya.
Tumejifunza JINSI YA KUTUMIKA KATIKA WITO AMBAO MTU
AMEPEWA NA MUNGU. Tumeongozwa na andiko la 2 Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule
wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.” Mtumishi wa Mungu
asipojitahidi kuimarisha wito na uteule wake lazima atajikwaa. Bwana Yesu
aliwahi kuwauliza wanafunzi wake kama walipungukiwa na kitu alipowatuma.
Wakasema, La. Sisi leo tunapungukiwa kwa vile tunafanya huduma ambazo ziko nje
ya wito wetu. Baraka za mtumishi wa Mungu ziko katika kusimamia wito wake. Hata
katika kazi za ajira, mfanyakazi analipwa kwa ile kazi ambayo ana mkataba wake
tu. Akifanya zingine asitegemee kulipwa hata kama amefanya vizuri na kuchoka.
Lakini pia tumekumbushana jinsi ya kuwekeza katika
ndoa na familia zetu. Kuna watumishi wamezama katika huduma za kiroho mpaka
wamesahau ndoa na familia zao. Wamesahau kwamba Mungu alianzisha ndoa na
familia kabla ya Kanisa. Kanisa liliasisiwa kama njia ya kumrudisha mwanadamu
katika mstari lakini kamwe sio mbadala wa familia.
Maombi yako ni muhimu sana ili watumishi wengi zaidi
wajengewe uwezo kwa vile wanalisha waumini kiroho wakati wao wenyewe
wamepungukiwa. Mama anayenyonyesha anahitaji sana matunzo ili atoe maziwa mengi
na bora kwa mtoto wake.
Karibu sana uwe sehemu ya kuwatia moyo watumishi wa
Mungu bila mipaka ya kimadhehebu.
Dr. Lawi Mshana