ONGEZA THAMANI YA MAISHA YA WATU WENGINE NDIPO UTAFANIKIWA (Video)
ONGEZA
THAMANI YA MAISHA YA WATU WENGINE NDIPO UTAFANIKIWA
Hatukuletwa duniani kwa ajili ya maisha yetu binafsi. Saini ya dole gumba inathibitisha kwamba hufanani na mtu yeyote duniani. Hivyo kuna kazi maalum ambayo ni wewe tu unaiweza.
Wafilipi 2:4 “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”
Mungu alikusudia kumbariki Ibrahimu ili awe baraka kwa wengine. Mwanzo 12:2 “nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka.”
Hatukutumwa kuhubiri kwa maneno tu. Tumeagizwa KUWASAIDIA WANYONGE. Bwana Yesu mwenyewe amesema ANAYEBARIKIWA NI ANAYETOA KULIKO ANAYEPOKEA.
Mdo 20:35 “Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”
Swali: Unapokea vingapi na unatoa vingapi? Katika kutoa usihesabu majukumu yako na masuala ambayo una maslahi nayo. Hesabu watu ambao ukiwasaidia hawatakushukuru au hata hawajui ni wewe uliwasaidia.
Tunapogusa maisha ya wengine Mungu anaona sababu ya kutujaza baraka kwa vile tumekubali kuwa mkono wake wa kugusa maisha ya wengine. Lk 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”
Jitahidi kuwa na tabia ya Mungu. Mungu anawasaidia waovu na wema. Tabia ya mwanadamu ni kuwapa tu watu ambao ni wema kwake au marafiki zake.
Luka 6:35 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu.”
Mathayo 5:45 “ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.”
Naomba Mungu atutengeneze tuwe ‘mfereji’ badala ya kuwa ‘bwawa; ili tuguse maisha ya wengine.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au
whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania