Tatizo lako unahudhuria ibada badala ya kushiriki ibada (Video)
Tatizo
lako unahudhuria ibada badala ya kushiriki ibada
Katika maono nilikutana na mpendwa akaniambia bado tatizo lake halijaisha. Nikamwambia, ‘Unajua tatizo lako unahudhuria ibada badala ya kushiriki ibada!’
Kwa kifupi Mungu anapenda tujue kwamba mtu anaweza kuhudhuria (kujaza namba kwenye ibada) lakini hajamaanisha na hana lengo la kukutana na Mungu kipekee.
Tukisoma maandiko tunagundua kwamba watumishi wa Mungu walimfanyia Mungu ibada na sio kuwafanyia watu ibada. Na ndipo Roho Mtakatifu akasema nao. Mdo 13:2 “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.”
Kwa muda mrefu umekuwa ukiwafanyia watu ibada badala ya kumfanyia Mungu. Ndiyo maana humsikii Mungu akisema na wewe.
Ukitaka Roho Mtakatifu akupe maelekezo ya wazi, MFANYIE MUNGU IBADA. Acha kufanya ibada ya kujionyesha kwa watu unavyojua kuimba, kuomba, kuhubiri, kutoa au ulivyovaa vizuri.
Lazima uwe na huduma fulani inayogusa kundi fulani la watu. Usipende kuishi kihasara katika Ufalme wa Mungu. Wajane walipofiwa na mfadhili wao waligoma kwamba hastahili kuondoka kipindi hicho. Wakamuita Petro ili afanye kitu. Hii inaonyesha jinsi huduma yake ilivyokuwa na mguso kwao.
Mdo 9:36-41 “36 Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. 37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. 38 Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. 39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. 40 Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. 41 Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.”
Sijui wangapi wanakumiss kanisani unapokuwa hupo! Sijui wangapi watakumiss siku ukiondoka duniani! Ziko huduma nyingi lakini unatakiwa uwe na huduma ambayo unaifanya bila kupangiwa wala kumwangalia mtu mwingine. Mfano, kushonea wajane nguo, kuhudumia wageni, kusafirisha watumishi wa Mungu, kulea wanandoa wapya, kushauri vijana, kuombea wameshenari, kusaidia watu waliopatwa na majanga au waliofanyiwa ukatili wa kijinsia nk
Si lazima ukifa ufufuliwe kama Dorkasi. Ila unaowagusa wanaweza kuzuia mabaya yasikupate. Ayubu 5:26 “Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.”
Anza kushiriki katika kumuabudu au kumtumikia Mungu na sio kuwapendeza wanaokutazama. Usipende tena kujionyesha kwamba unaweza kufanya huduma fulani. Kwa kufanya hivyo utakuwa unazuia kupata thawabu kutoka kwa Mungu. Utaishia kupata thawabu ya kusifiwa na wanadamu peke yake. Mathayo 6:5 “Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.”
Uwe na siku njema yenye baraka tele.
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au
whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania