UNAJUA KUWA MSHINDI NI SIFA MUHIMU KULIKO KUITWA MKRISTO? (Video)
UNAJUA
KUWA MSHINDI NI SIFA MUHIMU KULIKO KUITWA MKRISTO?
Bwana Yesu hajawahi kutumia neno WAKRISTO. Alitaka kanisa lake liwe na watu waliofanywa kuwa WANAFUNZI WAKE (na sio washirika au washarika waliojiunga na dini). Mshirika anajiunga kama mwanachama anavyojiunga na chama au kikundi lakini mwanafunzi anatengenezwa. Mtu anaweza kuwa mshirika au msharika wa dhehebu la Kikristo na sio mwanafunzi wa Yesu. Mathayo 28:19 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.”
Kipindi cha kanisa la kwanza wale waliompokea Yesu na kujitenga na dini ya Kiyahudi waliitwa NJIA. Ukisoma katika Matendo ya Mitume utaona neno Njia lenye maana ya waliompokea Yesu likiwa limeandikwa kwa kuanza na herufi kubwa.
Mdo 9:2 “akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu.” Mdo 19:9 “Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano.” Mdo 19:23 “Wakati huo kukatukia ghasia si haba katika habari ya Njia ile.” Mdo 24:14 “Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.”
Wanafunzi hawa walianza kuitwa WAKRISTO huko Antiokia (hawakujiita wenyewe). Mdo 11:26 “hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.”
Baada ya Wakristo kuwa na michanganyo yakatokea majina mengine kama vile Wakristo waliookoka, walokole nk.
Ukifuatilia katika makanisa ya Ufunuo wa Yohana utaona kwamba neno lililotumika ni WASHINDAO na sio WAKRISTO. La msingi zaidi ni kushinda kuliko kuwa na jina. Ufu 3:1b “Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.”
Ufu 21:7 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye
atakuwa mwanangu.”
Ufu 2:11 “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.”
Mbinguni hakitaingia kinyonge chochote hata kama kinaitwa Mkristo. Ufu 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondo.”
Mungu atusaidie kufikia viwango vya kimbingu bila kasoro yoyote. Waefeso 5:27 “apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.”
Dr. Lawi Mshana, +255712-924234 (sms au whatsapp), Korogwe, Tanga, Tanzania