Ticker

6/recent/ticker-posts

UNAKWAMA KIMAISHA KWA VILE ‘UMEMALIZA SHULE’?


UNAKWAMA KIMAISHA KWA VILE ‘UMEMALIZA SHULE’?

Inasemekana kwamba kama mwanafunzi au mwanachuo atapewa mtihani uleule alioufanya wiki iliyopita, anaweza kufeli. Unajua kwanini? Alikuwa anasoma kwa ajili ya mtihani tu na kwa kiasi kikubwa alikariri kuliko kuelewa. Hivyo akishamaliza mtihani ni kama ametua mzigo ambao unafuta hata taarifa alizo nazo kichwani.

Hata hivyo tatizo hili ni kubwa zaidi. Watu wengi tangu wamalize shule au chuo hawajisomei tena kwa vile wanadhani kwamba hakuna shule wala chuo kitawapa tena mtihani. Wanasahau kwamba kuna mitihani mingi ya maisha ambayo tunakumbana nayo hata baada ya kutoka katika shule rasmi. Kusema kweli HAKUNA KUMALIZA SHULE. Shule inaendelea hadi tutakapoondoka duniani.

La kusikitisha ni kwamba maskini hawasomi vitabu hasa baada ya kutoka shuleni au chuoni lakini matajiri wanasoma vitabu vingi sana kwa mwaka. Watu wengi hawajawahi kusoma kitabu chochote kinachohusiana na shughuli ya kipato wanayoifanya. Matokeo yake wanakuwa watu wa kawaida ambao hawana jipya kwa wateja wao. Wengi wasio na elimu rasmi wanapenda kujifunza mengi kwa vile hawana cheti cha kuombea kazi. Matokeo yake wanajikuta wanajua vitu vingi na kufaa kufanya kazi nyingi katika mazingira tofauti tofauti.

Pamoja na masomo yangu rasmi niliyosoma hadi shahada ya uzamivu, nimeendelea kusoma kozi nyingi kila nilipoona kwamba nina upungufu katika maeneo fulani kv usimamizi wa miradi, kusaidia kanisa liweze kukabiliana na majanga nk. Ni mwezi uliopita tu nimepata cheti baada ya kufuzu mafunzo ya Business Development kwa kutumia teknolojia ya kidijitali. Tunakoelekea kazi nyingi zitatoweka na wengi watakuwa hawajajiandaa kuhitajika katika mfumo wa kidijitali.

Hatuwezi kupata mabadiliko chanya wakati mwenendo wetu ni uleule wa zamani. Ukitaka kufanya jambo kwa namna tofauti, lazima kwanza wewe uwe wa tofauti (If you want to make a difference, be different). Ndiyo maana ukitembelea ukurasa wangu wa Facebook utaona nimeandika, “You can never do more than you become.” (huwezi kutenda zaidi ya ulivyo au unavyojiendeleza). Lazima ujiongeze zaidi kama unataka kuona tofauti katika maisha yako.

Kusoma vitabu na kushiriki semina zilizoandaliwa na watu waliofanikiwa, kunakusaidia kujifunza kupitia makosa ya wengine badala ya kujifunza kwa makosa yako mwenyewe. Lakini pia unapata marafiki wapya wanaoweza kukupa hatua fulani ya kwenda mbele. Ukifuatilia sana kwenye simu yako unazungumza zaidi na watu wenye mawazo duni kuliko ya kwako. Jambo hili linakuzuia kwenda hatua nyingine kwa vile unajiamini kwamba uko vizuri na kumbe ni kwa vile hujawaona wenye vipaji na uwezo kama wa kwako waliofanya mambo makubwa zaidi. Mara nyingi eneo unalofeli ni lile ambalo huna ujuzi au taarifa mpya za kutosha kukabiliana na changamoto za sasa. Elimu ya zamani inaweza kushindwa kukabiliana na changamoto za wakati huu.

Hiyo hapo chini ni picha ya kipeperushi ambacho kinakupa mwongozo wa namna tunavyofanya semina zetu za kujenga uwezo wa maisha ya kiroho na kiuchumi katika jamii. Unaweza kuchagua semina za kiroho au za kijamii. Kipeperushi hicho kinapatikana kwa lugha ya Kiswahili na Kingereza.

Ninayafikia makundi mbalimbali ndani na nje ya nchi bila ubaguzi wa aina yoyote.

Karibu sana katika semina zetu za kujenga uwezo (empowerment seminars). Sio semina za kukufundisha peke yake bali kukusaidia kujigundua na kufikia ndoto zako.

Dr. Lawi Mshana, 0712-924234; Korogwe, Tanga, Tanzania.