Mwanzo 1:28 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”
Hili ni moja ya maandiko yanayotumiwa na wengi katika kuzungumzia mpango wa Mungu kuhusu uzazi. Hata hivyo kuna mambo kadhaa ambayo mimi binafsi ninajifunza kupitia andiko hilo.
1. Mungu alisema ZAENI MKAONGEZEKE kwa mume
na mke mmoja tu (Adamu na Hawa) wakati hakuna wenye dhambi duniani.
Ndiyo maana alitangulia kuwabariki kwanza kabla ya kuwaagiza kuongezeka. Mungu alitoa agizo la kuzaa na kuongezeka kwa Adamu na Hawa kabla ya anguko la dhambi halafu akarudia wakati wa Nuhu baada ya kuwaangamiza wenye dhambi katika uso wa nchi kwa gharika. Mwa 9:1 “Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi.” Kwa hiyo shauku kubwa ya Mungu ni kuona wenye haki wanaongezeka na sio wenye dhambi. Kwa tafsiri ya leo tunaweza kusema kwamba jambo la muhimu zaidi kwa Mungu ni kuona wengi wanazaliwa mara ya pili (wanaokoka) na kuingizwa katika Ufalme Wake ili waweze kulibeba Jina lake na kutangaza haki yake.
2. Mungu hakuishia katika kusema watu
wazae na kuongezeka bali alisema MKAIJAZE NCHI.
Mungu hakukusudia watu waongezeke kwa hasara. Alitaka wanapoongezeka watumie vizuri raslimali zilizopo. Kuijaza nchi sio kujaa kama mihogo iliyopangwa kwenye kikapu bali ni kuhakikisha hakuna maeneo ambayo yamekaa tu bila kutumika kwa faida. Mungu hakukusudia nchi ijazwe na watu wavivu ambao wamezungukwa na vichaka ambavyo wameshindwa kuviendeleza. Wapo watu wamezungukwa na vichaka lakini wameshindwa kupanda hata miti ya matunda huku wakitegemea kuomba ruhusa ya kuchuma matunda kwenye miti ya majirani zao kila siku.
3. Mungu alitaka baada ya watu wake
kuijaza nchi WAITIISHE.
Lazima tujiulize kiasi gani tumeitiisha au kuitawala dunia yetu. Kwa lugha nyingine kiasi gani dunia inatutumikia sisi. Kinyume chake watu wengi wanaitumikia dunia badala ya dunia kuwatumikia. Mungu alitaka tuwe na mamlaka juu ya dunia tunayoishi. Tunufaike na mali tulizo nazo na kuweza kuzitiisha roho zozote zinazoinuka kinyume na mpango wa Mungu kwetu. Mathayo 17:20 “Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.” Mungu ametupa uwezo wa kusema na milima iliyosimama mbele ya ndoto zetu na iweze kutusikia na kuhamia kule tunakotaka iende.
4. Baada ya kuitiisha dunia, Mungu
alisema MKATAWALE viumbe vya baharini, vya nchi kavu na vya angani.
La kusikitisha ni kwamba kazi ya kutunza mazingira tuliyopewa na Mungu tumeiachia serikali. Tumeshindwa kufanya hata vile ambavyo tunaweza kufanya. Tunafanya usafi wa mazingira yetu kwa kuogopa kuadhibiwa na serikali. Tunatakiwa kujua kwamba anayefuga kuku na kunufaika nazo kwa sehemu amewatawala ndege. Mtu mwenye imani kwa Mungu (Elohim) hawezi kutawala kwa kuongea tu bila vitendo. Yakobo 2:26 “Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.” Hatuwezi kuendelea kuhubiri tu kwamba Mungu anaweza mambo yote wakati sisi wenyewe tumeshindwa maisha. Tukiwa hivyo tutakuwa tuna shida mahali fulani.
5. Lakini pia tujue kwamba Adamu na Hawa
ni wawakilishi wa vizazi vyote vya wanadamu.
Hivyo Mungu alipowaambia zaeni
mkaongezeke hakumaanisha kwamba hiyo kazi ya kuongezeka na kuijaza nchi wataifanya
peke yao kama wanandoa katika kipindi cha uhai wao. Ukifuatilia sana katika
Biblia hakuna familia moja ilizaa watoto wengi kwa kisingizio cha kuongezeka na
kuijaza nchi. Hata Yakobo alipata watoto 12 kupitia wanawake wanne tofauti
ambao ni Raheli, Lea, Bilha na Zilpa (Mwa 29,30). Kwa hiyo ukizaa mtoto mmoja
au watoto kumi umechangia katika kuijaza nchi kwa vile hakuna idadi maalum
iliyotolewa. Ukweli ni kwamba HATA KAMA TAFSIRI YA KUIJAZA NCHI NI YA KUZAA
WATOTO WENGI, SI MPANGO WA MUNGU KWAMBA UIJAZE NCHI WEWE PEKE YAKO. Lazima
tusaidiane kupitia familia zetu mbalimbali.
Kwanini Wakristo tunaoa mke
mmoja
1. Tunafuata maelekezo
ya Bwana Yesu aliyosema tangu mwanzo Mungu aliumba mtu mume na mtu mke na
kwamba talaka haikuanzishwa na Mungu
Mathayo 19:4 “Akajibu,
akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu
mke.”
Alijibu Mafarisayo Mk 10:2-9 “2
Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe?
Huku wakimjaribu. 3 Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? 4 Wakasema,
Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. 5 Yesu akawaambia, Kwa
sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. 6 Lakini tangu mwanzo
wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. 7 Kwa sababu hiyo mtu
atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; 8 na hao wawili watakuwa
mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. 9 Basi
alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
Alijibu wanafunzi wake. Mk 10:11,12
“Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;
na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.na mke, akimwacha mumewe
na kuolewa na mtu mwingine, azini.”
Mt 19:8,9 “Akawaambia,
Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu;
lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha
mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye
amwoaye yule aliyeachwa azini.”
2. Baada ya Yesu kuja,
kufa na kufufuka hatuishi tena katika nyakati za ujinga
Matendo ya Mitume 17:30,31 “Basi,
zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu
wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka
siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye
amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.”
Kina Ibrahimu na Yakobo
waliishi kipindi cha ujinga kabla Bwana Yesu aliye hekima yake Mungu kuja
duniani. 1 Kor 1:24 “bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo,
nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.”
3. Hata hivyo mtu
akimwamini Yesu haruhusiwi kumuacha mkewe au mumewe na akiwa ana mke zaidi ya
mmoja atatakiwa kubaki na mmoja lakini hatakiwi kutelekeza familia yake kwa
mahitaji ya maisha.
1 Kor 7:9-16 “9 Lakini
ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.
10 Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke
asiachane na mumewe; 11 lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au
apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe. 12 Lakini watu wengine nawaambia
mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke
huyo anakubali kukaa naye asimwache. 13 Na mwanamke, ambaye ana mume
asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. 14 Kwa maana
yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa
katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa
ni watakatifu. 15 Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo
ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani. 16
Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe
mwanamume, kama utamwokoa mkeo?”
Maana ya neno ‘hafungiki’. Je
ina maana anaruhusiwa kuoa au kuolewa tena? Tutambue kwamba ndoa sio kifungo (bondage/dedoulotai).
Kwa hiyo alimaanisha hana sababu ya kumng’ang’ania (aheshimu uamuzi wake) bali
ajali amani (asitengeneze mazingira mabaya). Haina maana kwamba anaruhusiwa
kuoa au kuolewa. Kama itakuwa anaruhusiwa kuoa au kuolewa Paulo atakuwa
anajipinga mwenyewe na atakuwa anapingana na Bwana Yesu jambo ambalo sio kweli.
Lk 16:18 “Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye
yeye aliyeachwa na mumewe azini.”
Dr. Lawi Mshana, Tanzania