Ticker

6/recent/ticker-posts

(Maswali na Majibu) Na 1. Baada ya kufanyiwa maombi ya kufunguliwa tufanyeje au tuepukane na mambo gani ili adui asitusumbue tena?


 Na 1. Baada ya kufanyiwa maombi ya kufunguliwa tufanyeje au tuepukane na mambo gani ili adui asitusumbue tena?

Jibu

1. Tutambue milango iliyosababisha shetani akapata nafasi na kisha tuifunge. Mfano, marafiki wabaya, sherehe mbaya, vijiwe, kazi zisizofaa nk

Waefeso 4:27 “wala msimpe Ibilisi nafasi.” 1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Kutoka 34:15 “Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.” Mf marafiki, vijiwe, kazi nk

2. Tufanye kitu fulani kwa ajili ya Mungu KILA SIKU (sio kila ibada) – mapepo yanarudi kama baada ya kutolewa yamekuta nafasi ni tupu (hujampa Yesu nafasi atawale maisha yako).

Luka 11:24-26 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.”

3. Tuepuke ibada za shetani na watu wenye maagano na shetani – hakikisha unaabudu mahali sahihi. Usiwekewe mikono na mawakala wa shetani na usitoe sadaka mahali ambapo sadaka yako inapelekwa kwenye madhabahu za shetani. Kuna makanisa ambayo waumini wanatolewa kafara kila mwaka.

Kum 12:14 “bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.” 2 Wakorintho 6:17 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.” 1 Wakorintho 5:11 “Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.”

4. Tujitiishe kwa Mungu na kumpinga shetani – shetani hawezi kukimbia kama unayemkemea huna uhusiano wa karibu na Mungu. Ukijaribu kumkemea wakati huna sifa anaweza kukuaibisha.

Yakobo 4:7 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”

Mdo 19:13-16 “Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo. Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo. Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani? Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.”

5. Tufunge na kuomba mara kwa mara – kuna mambo hayawezi kufanyika bila kufunga na kuomba. Hata hivyo usifunge (usishinde njaa) wakati huna muda wa kuomba. Hata wajumbe wa shetani wanafunga ili kupata nguvu za kiroho. Wanafunga hata siku 14. Je, wewe si zaidi?

Mathayo 17:19-21 “Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.”

Sababu ziko nyingi. Hebu ongeza zingine unazozikumbuka hapo chini kwenye POST A COMMENT.

Dr. Lawi Mshana, Freelance Facilitator & Public Speaker, 0712924234, Tanzania